Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Masache Njelu Kasaka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Primary Question
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itafikisha umeme kwenye vijiji ambavyo bado havijafikiwa Wilayani Chunya pamoja na Makao Makuu ya Kata za Nkung’ungu, Lualaje, Mafyeko na Kambikatoto?
Supplementary Question 1
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake hayo. Nami nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Wilaya ya Chunya katika REA Awamu ya Pili tumepata vijiji 12; lakini katika vijiji 12, vijiji 10 vinapita kwenye misitu ambayo iko chini ya TFS. Sasa mradi huu unapopita, TFS imekwamisha huu mradi inasubiri mpaka iweze kupata malipo ya fidia ili mradi uweze kuendelea, kitu ambacho kinashangaza sana.
Je, ni lini sasa Serikali itakaa na taasisi nyingine ya Serikali TFS waweze kujadiliana ili malipo yaweze kufanyika na mradi huu uweze kutekelezeka na wananchi waweze kunufaika kama ambavyo wanategemea? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwenye kila kijiji kitapata transfomer ya KVA 50 ambapo usambazaji wake wake wa umeme ni wastani wa kilometa moja ambayo inahudumia takribani watu 68: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza transfomer yenye ukubwa zaidi ya KVA 50 ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na huduma hii ya umeme?
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia masuala ya wananchi na hasa kwenye hili eneo la fidia. Kwanza naishukuru Serikali kwamba ilishirikiana na wananchi na kuwaomba miradi yote ya REA isiwe miradi inayohitaji fidia katika maeneo ambayo miradi inapita. Nawashukuru wananchi kwa niaba ya Serikali walikubali ombi hilo kwa sababu umeme ni kwa mahitaji yetu sote.
Mheshimiwa Spika, kwanza niseme kwamba mradi wa REA hauna fidia kwa wananchi. Ila kwa wenzetu wa TFS wamekuwa wanazo kanuni ambazo zinaelekeza kwamba maeneo yao yakitaka kutumika kwa shughuli nyingine, basi fidia itolewe. Nasi mara kadhaa tumefanya mazungumzo nao ili eneo hili liondoke na kikao cha mwisho kimefanyika wiki hii na tunatarajia kabla ya mwezi huu tutakuwa tumekamilisha jambo hili, ili sasa kama ambavyo tunapeleka miradi ya umeme katika maeneo ya wananchi bila kuwafidia na TFS ambayo ni taasisi ya Serikali pia, isifidiwe kwa kutumia eneo kwa ajili ya shughuli za wananchi. Tuna uhakika jambo hili litakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika awamu hii ya pili eneo la Mbeya lakini pia Katavi, Simiyu na Morogoro yapo maeneo yanahitaji attention ya namna hiyo na tayari tunayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye jambo la pili, ni kweli kwamba wateja ambao wamefikishiwa umeme kwa kipindi hiki, siyo wote wanaouhitaji, lakini Serikali imejitahidi sana kwa hizo shilingi trilioni moja na bilioni 250 kupeleka angalau kwa wateja wa awali katika maeneo ya mijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wengine wote kwamba Serikali inayo mradi mwingine wa densification ambayo ni jazilizi; inayo mradi mwingine wa Peri-Urban wa kupeleka miradi ya umeme huko na pia TANESCO wanaendelea, kila mtu atapata umeme kwa kadiri Serikali inavyojitahidi kufikisha umeme katika maeneo hayo. (Makofi)
Name
Anton Albert Mwantona
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rungwe
Primary Question
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itafikisha umeme kwenye vijiji ambavyo bado havijafikiwa Wilayani Chunya pamoja na Makao Makuu ya Kata za Nkung’ungu, Lualaje, Mafyeko na Kambikatoto?
Supplementary Question 2
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza katika Wizara hii ya Nishati. Jimbo la Rungwe lina vijiji 99. Katika vijiji 99, vijiji 66 vilikuwa kwenye mradi wa REA II na vijiji 33 viko kwenye mradi wa REA III; lakini katika vijiji 66 ni vijiji 41 tu ndiyo vilikamilishiwa umeme, lakini vijiji 25 havikukamilishiwa umeme katika awamu ya pili ya REA.
Mheshimiwa Spika, Waziri alikuja kufanya ziara kule kwetu kwenye ufunguzi wa REA III tarehe 28 mwezi wa Nane akasema kuna fedha ilibaki kwenye REA II, shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya kupeleka umeme kukamilisha mradi wa umeme kwenye REA II. Akasema, ndani ya miezi miwili huo mradi utakamilika na wananchi watapata umeme.
Mheshimiwa Spika, la kusikitisha, mpaka leo umeme bado haujafika na kazi bado haijaanza. Nilikuwa naomba Waziri atoe kauli hapa, ni lini mradi wa umeme REA II vijiji 25 katika Jimbo la Rungwe utaanza? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mbunge wa Rungwe kwa swali lake. Naomba kutoa majibu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwenye mradi wa REA III round ya kwanza zilikuwepo lots 29 na lots 8 bado hazijakamilika katika eneo hilo la Rungwe na maeneo mengine. Kama tulivyosema, kulikuwa na kuchelewa kwa sababu ya kuchelewa kupatikana kwa vifaa na maeneo kama hayo, lakini Serikali tayari imeiagiza REA kuhakikisha inakamilisha miradi hiyo na wakandarasi kabla ya mwezi wa tatu mwaka huu. Kwa hiyo, vile viporo vyote ambavyo vilibakia kwenye mradi wa REA II, REA III round one, vyote tunatarajia viwe vimekamilika kabla ya kwisha kwa mwezi wa Tatu mwaka huu 2022 eneo la Rungwe likiwemo. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved