Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hamida Mohamedi Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Lindi Mjini

Primary Question

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Lindi?

Supplementary Question 1

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, kwa kutuwezesha fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa mapenzi yake mema, lakini naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Lindi Mjini tuna kata 20 lakini kata 13 ziko katikati ya Mji, lakini ukiangalia wananchi wale, katika kata 13 zaidi ya watu 70,000 wanakosa mahali pa kukimbilia kwa maana ya kituo cha afya. Sasa ninaomba kuiuliza Serikali watatusaidiaje kuhakikisha kwamba tunapata Kituo cha Afya Lindi Mjini kuwasaidia wakazi wa kata 13 waishio Lindi Mjini?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili katika Kata ya Kitumbikwela upande wa pili wa bahari pana kituo cha afya lakini bado hakijakamilika, wanawake wanapata changamoto wakati wa kujifungua na wanapolazimika kufanyiwa upasuaji, kivuko wakati mwingine kinakuwa kina changamoto.

Kwa hiyo, ninaomba kuiuliza Serikali ni lini wataweza kutusaidia kuboresha Kituo cha Afya cha Kitumbikwela ili wanawake wajawazito waweze kuhudumiwa pale? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Hamida Mohamed kwa kuwasemea kwa dhati kabisa wananchi wa Lindi Mjini na mimi nimhakikishie kwamba Serikali hii sikivu ya Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan tutaendelea kushirikiana naye na kuhakikisha kwamba wananchi wa Lindi wanapata maendeleo ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na vituo vya afya katika Jimbo la Lindi Mjini; ni kweli kwamba wana vituo vya afya vichache. Lakini Serikali tumeshatoa fedha kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Mnazimmoja, lakini tumepeleka fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali kubwa ya kisasa ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini bado tutaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea kujenga vituo vya afya katika kata za kimkakati ambazo hazina vituo vya afya.

Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba Serikali inafahamu changamoto hiyo na mipango inaandaliwa kuhakikisha Manispaa ya Lindi tunapata vituo vya afya.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Kituo cha Afya cha Kitumbikwela ni kweli Kata ya Kitumbikwela ipo upande wa pili wa bahari na njia kuu ya kuvuka pale ni kwa kutumia mapantoni lakini pia na boti. Kwa hiyo, kwa kweli tunahitaji kuboresha kituo kile cha afya ndio maana tulianza ujenzi kwa awamu ya kwanza, sasa tutakwenda kujenga miundombinu iliyobakia zikiwemo wodi na majengo mengine kwa awamu ya pili ili kuhakikisha huduma zinakwenda vizuri. Ahsante. (Makofi)

Name

Mwantumu Mzamili Zodo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Lindi?

Supplementary Question 2

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa kuwa Serikali inajenga Hospitali za Wilaya na Vituo vya Afya nchi nzima na kwa kuwa baadhi ya hospitali za Wilaya ni kongwe.

Je, Serikali haioni haja ya kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati hospitali za wilaya ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Pangani? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantumu Zodo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumekuwa na Hospitali za Halmashauri kongwe ambazo zilijengwa miaka mingi. Zipo ambazo zimejengwa baada ya uhuru mapema, lakini zipo ambazo, zilijengwa hata kabla ya uhuru na kwa kweli miundombinu yake sasa ni chakavu. Lakini pia haziendani na kiwango cha hospitali za halmashauri ambazo sasa tunazihitaji. Kwa kutambua hilo Serikali tumefanya tathmini ya hospitali zote za Halmashauri kongwe na tumekwisha ziainisha. Tunaweka mpango, baada ya kukamilisha hospitali za Halmashauri 28, sasa tutakwenda kukarabati na kupanua hospitali zile kongwe ikiwepo Hospitali hii ya Pangani. Ahsante sana. (Makofi)