Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Benaya Liuka Kapinga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Vijijini
Primary Question
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja linalounganisha Vijiji vya Kingoli – Litumbandyosi Wilaya ya Mbinga na Machimavyalafu Wilaya ya Ludewa katika Mto Ruhuhu?
Supplementary Question 1
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali yenye nia ya dhati kabisa kuondoa adha kubwa ambayo wananchi wa wilaya hizi mbili, mikoa hii miwili ya Ruvuma na Njombe, kwa sababu mto huu una mamba wengi lakini ni mto mkubwa sana. Kwa hiyo, ni hatari kubwa sana kwa wananchi pale, kwa hiyo kwa majibu nashukuru sana. Ombi tu kwamba waharakishe ili daraja hili liweze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ombi hili, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Barabara ya Unyoni kuelekea Maguhu inapitika kwa shida sana lakini ipo barabara kutoka hapo Maguhu Mapera kuelekea Kambarage, barabara hii iko hatarini kutoweka. Kuna korongo kubwa sana kutokana na mvua hizi zinazoendelea kunyesha.
Sasa je, Serikali ipo tayari kutoa fedha za dharura ili kuokoa ile barabara iweze kutumika kama inavyotumika siku zote? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu dogo la pili, jiografia ya Wilaya ya Mbinga hususan Jimbo la Mbinga Vijijini ni milima na mabonde hali ya kwamba inahitaji madaraja mengi lakini na barabara zinapitika kwa shida sana. Nahitaji commitment ya Serikali, je, iko tayari kuongeza fedha tofauti na ile hali ya kawaida katika Jimbo la Mbinga Vijijini? (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Liuka Kapinga Benaya, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, bahati nzuri nilifika jimboni kwake, niliona kazi nzuri anayoifanya na jinsi wananchi wanavyomkubali kwa kuwa anafuatilia kwa ukaribu zaidi matatizo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba swali la kwanza alilouliza ni kwamba je, tupo tayari kutoa fedha za dharula ili kusaidi hili korongo kubwa linapita katika hizi barabara ambazo ameziainisha. Niseme tu katika Bunge lako Tukufu baada ya agizo la Mheshimiwa Spika tumeshafanya tathmini ya awali ya kugundua maeneo yote ambayo ni korofi nchi nzima. Kwa hiyo, ambacho tutakwenda kuangalia tu katika eneo lako la Mbinga kama maeneo hayo yametengwa. Kama halipo maana yake tutamuagiza meneja wa TARURA katika halmashauri yako afanye tathmini ili tuone namna ambavyo tunaweza tukasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuhusu kuongeza fedha, tumewaagiza Mameneja wote wa TARURA Mikoa pamoja na katika Halmashauri. Katika mwaka huu wa fedha, watakavyoleta zile bajeti zao walete bajeti kulingana na uhalisia wa maeneo husika kwa hiyo, hilo ndiyo agizo. Kwa hiyo, naamini kwamba maeneo haya ambayo
Mheshimiwa Mbunge ameyaainisha yatakuwepo katika bajeti hizo. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Eng. Ezra John Chiwelesa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Primary Question
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja linalounganisha Vijiji vya Kingoli – Litumbandyosi Wilaya ya Mbinga na Machimavyalafu Wilaya ya Ludewa katika Mto Ruhuhu?
Supplementary Question 2
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Tatizo la madaraja katika Jimbo la Mbinga Vijijini ni sawa na tatizo la baadhi ya vijiji katika jimbo la Biharamulo. Kwa mfano; Kijiji cha Nemba kwenye Kata ya Nemba kuna Kijiji cha Kisenga kwenda Nyamazina, kuna makorongo makubwa sana watu hawawezi kupita na ni sehemu yenye mazao mengi Lusahunga, Midaho kwenda njia panda, Nyakahura kuna Kalukwete kwenda Msali B na Nyevyondo kwenda Ngara. Je, nini kauli ya Serikali kuhusu ujenzi wa madaraja ili wananchi hao waweze kuunganishwa na hatimaye waweze kupata huduma wanazostahili? (Makofi)
Name
Innocent Lugha Bashungwa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karagwe
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ambavyo TARURA inategemewa na Waheshimiwa Wabunge katika kutoa huduma kwenye majimbo yetu. Ofisi ya Rais, TAMISEMI, juzi tuliita wakandarasi wote nchini ambao wanahudumu kupitia TARURA, tuliita Mameneja wa Wilaya ya Mikoa ili kuweza kujipanga vyema kufanya kazi kwa weledi katika kuhudumia barabara za Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, Waheshimiwa Wabunge tuwahakikishie tunajenga TARURA mpya. Tumejifunza upande wa TANROADS kwa mfano kwenye masuala ya manunuzi, TANROADS huwa wanaanza mipango yao kuanzia Aprili kwa assumption kwamba haijawahi kutoka Wizara ikapata bajeti pungufu kwa mwaka fedha unaofuata pungufu ya asilimia 60 ya bajeti iliyopita. Kutokana na hilo TANROADS huwa wanafanya mipango ya manunuzi kuanzia Aprili ili inapoanza Julai 1 ya mwaka wa fedha wakandarasi wanakuwa wapo tayari kwenda site kuanza kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, utaratibu huo tunauleta ndani ya TARURA na tuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kupitia tozo kwa lita shilingi mia moja tayari TARURA kuna zaidi ya bilioni 322 kwa ajili ya kutoa huduma kwenye barabara kwenye wilaya zetu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha TARURA kuweza kupata Mifuko zaidi ya miwili ambayo tulikuwa nayo, Mfuko wa Tozo tumeona umeanza kutuletea fedha na Waheshimiwa Wabunge tutajipanga vizuri kuhakikisha huduma bora ya barabara za wananchi wetu vijijini na kwenye wilaya zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia kwenye mwaka wa fedha tutakaoleta Bajeti Bungeni hapa, Waheshimiwa Wabunge wataona mabadiliko na tumejipanga vizuri kuhakikisha tunafanya upembuzi yakinifu mapema badala ya kusubiri kupata fedha ndiyo TARURA ikafanye usanifu, sasa hivi tutakuwa tunafanya mapema, tunakuwa tuna database, fedha inapopatikana tunakwenda kwenye utendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye swali la Mheshimiwa Ndugu yangu Liuka Benaya, Mbunge wa Mbinga Vijijini, ametaja barabara ambayo inaunganisha mikoa miwili. Dhamira ya TARURA ni kuvipa vipaumbele barabara kama hizo ni kwa sababu ni barabara za kimkakati. Kwa hiyo, tutabainisha hilo kwenye jimbo lake pamoja na majimbo yote ili kuhakikisha tunapotekeleza fedha inavyokwenda basi hiyo barabara inaleta impact za kiuchumi kwa wanachi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Name
Yahya Ally Mhata
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Primary Question
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja linalounganisha Vijiji vya Kingoli – Litumbandyosi Wilaya ya Mbinga na Machimavyalafu Wilaya ya Ludewa katika Mto Ruhuhu?
Supplementary Question 3
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Naibu Waziri na Waziri wake kwa majibu mazuri ya Serikali. Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu kwenye Jimbo langu la Nanyumbu, sasa hivi kuna kadhia kubwa ya korongo kubwa ambalo limesababisha wananchi wa Kijiji cha Kiuve wawe kisiwani. Jambo ambalo limesababisha mama mmoja kujifungua kwa sababu ya kushindwa kufika hospitalini kutokana na korongo hilo.
Swali, je, Waziri atakuwa tayari kufuatana nami kwenda kuona kadhia kubwa iliyopo ambayo wananchi wa Kijiji kile cha Chiuve wanashindwa kufika hospitalini kutokana na lile korongo ili tutafuta majawabu sahihi ya wananchi wale? (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa hiyo changamoto ambayo Mheshimiwa Mbunge ameieleza hapa, alinieleza hata kabla hajauliza hili swali la nyongeza na akawa ananiomba kwamba twende wote pamoja. Kwa hiyo, nafikiri amelileta hapa ili nimthibitishie kupitia Bunge. Nipo tayari kuongozana naye ili tukashuhudie hili eneo na tuweze kupata majawabu ya haraka kuhakikisha tunawasaidia wananchi wa eneo la Chiuve. Ahsante.