Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: - Je, ni lini Serikali italeta Muswada Bungeni ili kuboresha Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 kutokana na Sheria hiyo kupitwa na wakati?
Supplementary Question 1
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. pamoja na majibu ya Serikali, na kwa kuwa amekiri kwamba Muswada huu umeshasomwa kwa mara ya kwanza Bungeni, ni commitment gani anatoa kwa maana Muswada huu uweze kuja kwa mara ya pili, hatimaye mara ya tatu ili hii sheria iweze kuboreshwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ilikuwa haitambui usafiri wa pikipiki, almaarufu kama bodaboda, kama ni chombo rasmi cha kusafirisha abiria na chombo hiki sasa hivi kinatumika kwa Watanzania walio wengi nchini. Kama sheria hii itaendelea kuchukua muda, Serikali haioni umuhimu wa kuleta kwa hati ya dharura hata katika sheria ya mabadiliko mbalimbali ili jambo hili liweze kuwa katika sheria zetu za nchini?
Name
Sagini Jumanne Abdallah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu commitment ya Serikali, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika vikao vijavyo ambavyo tutaruhusu marekebisho ya sheria tutaangalia uwezekano wa kuileta sheria hiyo ili iweze kupitishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili suala la usafiri wa pikipiki, hili ni pamoja na mambo mengine ambayo yalijitokeza na hususan maoni ya Kamati ya NUU, yalibaini kwamba pana mambo mengine ya kuhitaji kuzingatiwa ukiwemo usafiri wa pikipiki. Kwa hiyo ni ahadi yetu kwamba muswada huo utakapoletwa humu utakuwa pia umezigatia masuala ya usafiri wa bodaboda. Ahsante. (Makofi)
Name
Tarimba Gulam Abbas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: - Je, ni lini Serikali italeta Muswada Bungeni ili kuboresha Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 kutokana na Sheria hiyo kupitwa na wakati?
Supplementary Question 2
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ni kweli kuna haja ya kuweza kuifanyia marekebisho sheria hii ya mwaka 1973, lakini kama ilivyo sheria hii, bado ina nguvu ya kuweza kusimamia matatizo ya usalama barabarani kama askari wa polisi wa usalama barabarani watakuwa wanafanya kazi yao inavyostahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu bodaboda zinapita taa nyekundu, zinapita no entry, zinapita barabara za mwendokasi; ni nini kauli ya Serikali wakati tunasubiri kwenda kurekebisha sheria kwenye suala hili linalohusiana na matumizi mabaya ya barabara? Ahsante.
Name
Sagini Jumanne Abdallah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba swali la nyongeza la Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana naye, kwamba sheria ilivyo bado inaweza ikadhibiti usalama barabarani ikisimamiwa ipasavyo. Lakini hawa vijana wetu wanaoendesha bodaboda matendo wanayofanya ni hatarishi, siyo kwao tu, bali hata wale abiria wanaowabeba kama wataendelea kutumia barabara kama wanavyofanya inavyozungumzwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie Bunge lako Tukufu kuviomba vyombo vyote vya dola vishirikiane na hawa polisi wa usalama barabarani kuwadhibiti vijana hawa, lakini pia kutumia nafasi hii kuwaelimisha wazingatie Sheria ya Usalama Barabarani kama ambavyo imeanza kufanyika kwenye maeneo mengine. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved