Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Justin Lazaro Nyamoga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kuigawa Wilaya ya Kilolo kuwa na Halmashauri mbili?
Supplementary Question 1
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ni zaidi ya miaka 10 sasa tangu Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ilula imeanzishwa, ningependa kujua ni tathmini gani au ni utaratibu gani unatumika ili kupandisha hadhi kutoka kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo kwenda kuwa Halmashauri?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ningependa kujua katika ugawaji wa halmashauri kipo kigezo cha idadi ya watu na katika maeneo yenye hifadhi kubwa ya misitu na maeneo yaliyohifadhiwa na mbuga kama Kilolo kigezo hiki kinakuwa tishio kusababisha kuchelewa kugawa kwa halmashauri pamoja na ukubwa wake. Je Serikali iko tayari kuangalia kigezo hiki na kuangalia zaidi ukubwa ili wananchi waweze kufikiwa na huduma?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishaji wa mamlaka mpya zikiwepo halmashauri za miji zinategemea kukidhi vigezo vilivyowekwa ili halmashauri iweze kupewa mamlaka halisi ya kuwa halmashauri kutoka malmaka ya mji mdogo. Ni kweli kwamba Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ilula ina zaidi ya miaka 10 lakini taratibu za kuomba kuwa Halmashauri ya Mji ni zilezile ambazo zinatumika kuomba Halmashauri ya Wilaya. Kwa maana vikao vya kisheria katika vijiji na mitaa, kata ngazi ya wilaya pamoja na DCC na RCC. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na kuomba Wilaya igawiwe kuwa wilaya mbili lakini pia wafuate utaratibu huo kwa Halmashauri ya Mji wa Ilula ili tathmini ifanyike kuona kama kama inakidhi vigezo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na ukubwa wa kijografia wa Wilaya ambayo ina misitu mingi lakini wananchi wachache. Kigezo cha wananchi ni kigezo muhimu sana kwa sababu tunapeleka mamlaka mpya kuhudumia wananchi kwa hiyo idadi ya wananchi ndio sababu ya msingi zaidi ya kutenga halmashauri mpya badala ya eneo la misitu, lakini pia kwa maana ya ukubwa ambao hakuna idadi ya watu. Kwa hiyo, suala hilo ni muhimu na tutaendelea kuhakikisha kwamba, tunalizingatia katika kugawa mamlaka mpya. Ahsante.
Name
Kilumbe Shabani Ng'enda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Primary Question
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kuigawa Wilaya ya Kilolo kuwa na Halmashauri mbili?
Supplementary Question 2
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Tatizo la kugawa maeneo ya utawala lililokuwa limetolewa na Mheshimiwa aliyemaliza, linafanana sana na tatizo lililopo katika Jimbo langu la Kigoma Mjini na hasa kugawa maeneo ya utawala ya kata. Maombi tayari yamekwishapelekwq kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo kwenye Wizara husika. Je, ni lini Serikali itafikiria kufanya kazi hii ya kugawa kata. Zipo kata ambazo zina wakazi wengi, zina mitaa mingi, Kata kama za Mwanga Kaskazini, Mwanga Kusini, Buzebazeba na Kibirizi huko Kigoma. Je, ni lini Serikali itachukua hatua hii ili kuwarahasishia watu huduma za kiutawala?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe N’genda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Halmashauri zimeendelea kuwasilisha maombi ya kugawa maeneo mapya ya utawala kwa maana ya kata na nikiri kwamba Serikali tumepokea zikiwepo Kata za Kigoma Mjini, tathmini zinaendelea na baada ya tathmini hizo na kuangalia mazingira hayo, tutashauri mamlaka husika kwa maana ya mamlaka inayoweza kugawa maeneo hayo ili tuweze kufikia hatua ambayo inahitajika. Kwa hivyo nimhakikishie Mbunge kwamba, suala hilo lipo linafanyiwa kazi. Nashukuru.
Name
Kasalali Emmanuel Mageni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sumve
Primary Question
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kuigawa Wilaya ya Kilolo kuwa na Halmashauri mbili?
Supplementary Question 3
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru. Kwa kuwa taratibu za kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kulipatikana Halmashauri ya Sumve ambayo ndio ina Jimbo la Sumve zimeshakamilika katika ngazi zote mpaka ngazi ya mkoa na tunasubiri tamko la ngazi ya juu kupatikana kwa Halmashauri ya Wilaya Sumve. Je, nini tamko la Wizara kuhusu upatikanaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumve ambayo ni tamanio kubwa la watu wa Sumve na itasaidia sana kusogeza huduma kwa wananchi?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasalali Mageni, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za kugawa maeneo mapya ya utawala tayari zimepokelewa kwa halmashauri zote ambazo zimewasilisha kupitia utaratibu wa kisheria na kanuni na tathmini inaendelea. Mara baada ya kukamilisha tathmini hizo mamlaka husika itafanya maamuzi ya kugawa ama kutoa muda kwa ajili ya kuboresha maeneo ambayo yatakuwa na upungufu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hilo lipo na linafanyiwa kazi. Niwaombe kuwa na subra ili muda ukifika basi mtapata majibu ya maamuzi ya Serikali.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved