Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanja cha Michezo katika Wilaya ya Hai?
Supplementary Question 1
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; kwa kweli majibu haya sioni kama yatatusaidia kuinua michezo nchini, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, Jimbo la Hai tayari pale Half London tayari tumetenga eneo kwa ajili ya kujenga kiwanja cha michezo.
Je, Serikali ipo tayari sasa kufanya mabadiliko kwenye Sera ya Michezo ili jukumu la kujenga uwanja liwe ni la Serikali Kuu na siyo Halmashauri? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili; Jimbo la Hai tuna vikundi vya sanaa vingi, tuna wasanii wazuri wengi na tayari tumeshaunda jukwaa la wasanii Jimbo la Hai na walezi wetu Mheshimiwa Taletale na Mheshimiwa MwanaFA.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri upo tayari kuambatana na mimi kwenda Hai kukaa na jukwaa la wasanii wa Hai ili kusikiliza changamoto walizonazo?
Name
Pauline Philipo Gekul
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mafuwe, Mbunge wa Hai.
Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Saasisha amehitaji kubadilishwa kwa sera hii ili jukumu la kujenga viwanja liwe ni jukumu la Serikali Kuu na si vinginevyo kama ambavyo sera imesema.
Mheshimiwa Spika, Niliarifu Bunge lako tukufu kwamba sera hii imeshawahi kupelekwa kwenye Kamati yetu ya Huduma za Jamii ikidhaniwa kwamba Sera hii imepitwa na wakati na mara nyingi tumekuwa tukiangalia miaka ya sera imetungwa lini lakini siyo validity ya sera hiyo.
Mheshimiwa Spika, sera hii imepitiwa na imeonekana kwamba inashirikisha wadau wote. Serikali Kuu ina jukumu lake, Serikali za Mitaa ina jukumu lake, wadau wana majukumu yao; kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba tushirikiane. Kwa upande wa Serikali Kuu tuna-deal na viwanja vikubwa ambavyo timu zetu za Kitaifa na kimataisa wanaweza wakafika. Lakini Halmashauri zetu zikitenga fedha, Mheshimiwa Mbunge tukishirikiana katika Halmashauri zetu kwa own source zetu, nina hakika kwamba viwanja vitajengwa na wananchi wetu watashiriki katika michezo. Lakini sisi hatukatai kushirikiana na Serikali za Mitaa na nishukuru Bunge mlitupatia shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Michezo, kama bajeti itaendelea kuongezeka sisi tutaendelea ku-support pia huko chini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameomba tuambatane kwenda Hai kwa ajili ya jukwaa la wasanii, ninakuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaambatana kwa sababu ndiyo maelekezo tuliyopewa tuwahudumie wasanii na mimi nipo tayari tutakwenda tarehe ambazo utakuwa tayari tutafika tutawasikiliza wasanii. Ahsante. (Makofi)
Name
Abubakar Damian Asenga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Primary Question
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanja cha Michezo katika Wilaya ya Hai?
Supplementary Question 2
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru; kwa kuwa mmoja wa Wabunge mwenzetu aliwahi kuuliza humu Bungeni kuhusu ukarabati wa viwanja vya michezo na Serikali ikachukua jukumu la kukarabati.
Je, ni lini Serikali itafanyia kazi ombi la ukarabati wa Uwanja Mkuu wa Tanganyika - Ifakara ambao unatumika na Wilaya tatu?
Name
Pauline Philipo Gekul
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na naomba nijibu swali la Mheshimiwa Abubakari kuwa sisi kama Wizara hatuna tatizo kabisa kushirikiana na Serikali za Mitaa, atakapotuletea maombi haya kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Michezo pale tutakapoweza pia tunaweza tuka-support. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaendelea kutoa rai kwa Halmashauri zetu kwamba hili jambo ni serious, tumekuwa tukitenga asilimia 10 ya mikopo, ujenzi wa hospitali, shule zetu, lakini suala la michezo imekuwa siyo kipaumbele. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane na ninawapongeza kwa dhati Wabunge ni wadau wakubwa sana wa michezo. (Makofi)
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanja cha Michezo katika Wilaya ya Hai?
Supplementary Question 3
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge Mheshimiwa Rais na Bunge tulipitisha kuondoa kodi kwenye nyasi bandia na hii ilikuwa ni kulenga kuboresha viwanja vya michezo kama sera inavyosema, lakini hali ya miundombinu ya viwanja nchini ni mbaya. Hatuoni mpango wowote wa maksudi wa Serikali kuongea ama na taasisi binafsi ambao wanamiliki viwanja au Halmashauri kuhakikisha tunatumia fursa hii ambayo Mheshimiwa Rais ametupa ya kuweka nyasi bandia nchini.
Je, ni upi mkakati wa Serikali wa makusudi wa kuboresha hali ya viwanja nchini ili Simba na Yanga ziache kulalamika kutokana na viwanja kama uwanja wa Manungu? (Makofi)
Name
Pauline Philipo Gekul
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, sisi tunalishukuru Bunge kwa kutupitishia exemption kwenye nyasi bandia ya VAT na Baraza letu la Michezo la Taifa (BMT) linaratibu zoezi la Halmashauri zetu wanapohitaji hizo nyasi bandia za grade gani wanaweza wakapata, tunaweza tukaratibu, tutakuunganisha, utapata hizo nyasi Mheshimiwa Mbunge kwa sababu viwango tunavyo vya class A, B, C na bei zake. Kwa hiyo, tushirikiane ili pale mnapohitaji muweze kuzipata.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa kuboresha viwanja vyetu sasa hivi TFF imeingia mkataba pia na Chama cha Mapinduzi ambacho kina viwanja vikubwa katika mikoa yetu. Viwanja kumi tunaenda kuviboresha kupitia mkataba huu ambao tutakuwa tumemaliza kukubaliana nao. Ahsante. (Makofi)
Name
Tarimba Gulam Abbas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Primary Question
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanja cha Michezo katika Wilaya ya Hai?
Supplementary Question 4
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; mwaka 2017 Kampuni ya SportPesa ilikarabati uwanja wa Benjamin Mkapa kwa thamani ya shilingi bilioni moja na nusu na mwaka 2019 machinery zote tulizotumia kwa ajili ya ukarabati wa uwanja ule ikiwemo seeding tractors, tractors pamoja na special grass cutting machines.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kutumia machine zile kupeleka katika viwanja vyenye uhitaji ili waweze kutumia machine zile? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Pauline Philipo Gekul
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, Wizara hatuna kizuizi chochote pale ambapo tunapata ombi la kuboresha viwanja vya michezo. Mheshimiwa Mbunge utakapotuletea pia tuta-consider ombi lako. Ahsante. (Makofi)