Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: - Je, ni lini wastaafu ambao waajiri wao walikuwa hawatoi michango katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii watalipwa haki zao?

Supplementary Question 1

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, swali langu la kwanza, je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na wale wastaafu ambao wanapigwa danadana wakati wakifuatilia mafao yao ambayo ni difference au utofauti ya kile kipindi ambacho makato yamepelekwa kwenye mifuko na kile kipindi ambacho hayajapelekwa kwenye mifuko na madai ni kwamba Maafisa Masuuli wamehama au hawakupata uteuzi?

Swali la pili, ningependa kujua kama Serikali itakuwa tayari sasa kuwataka waajiri au kuwahimiza watekeleze masharti ya mifuko haraka iwezekanavyo ili wale wastaafu waweze kulipwa haki zao? Ahsante.

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwa kipindi cha nyuma kulikuwa na changamoto ya wazee wetu waliotumikia Taifa kwa nguvu zao lakini pia kwa uadilifu na utumishi uliotukuka, walikuwa wakipata usumbufu katika kupata mafao yao aidha kwa kuambiwa kuleta barua na changamoto nyingine nyingi ambazo zilikuwepo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako pamoja na mimi na wasaidizi wengine kulikuwa na mpango kabambe wa kuweza kupita katika mikoa yote, kukutana na wastaafu na kutatua changamoto hizo na zoezi hili lilifanikiwa na kwa hatua ya sasa tayari tumekwisha kuanza kutatua changamoto hizo na kama kuna specific case ambayo bado haijafanyiwa kazi, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aweze kutufikishia ili tuchukue hatua haraka sana iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la pili pia kwamba kutokana na waajiri sasa kutokutekeleza wajibu; ni tamko la Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba waajiri wote nchini wanao wajibu wa kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini lakini sambamba na hilo Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii yaani National Social Security Fund Act ambayo inamtaka mwajiri kuwasilisha michango ya mwajiriwa wake bila usumbufu wowote na wajibu huu upo kwa mwajiri kwa mujibu wa sheria na kama atakiuka, kama jinsi ambavyo tumefanya kwa hawa 123 kuwapeleka mahakamani.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo hata mahakama kwa mujibu wa Bunge lako tukufu lilitunga sheria ambayo mwajiri ambaye atakuwa amekiuka kupeleka michango ya mwajiriwa wake akienda mahakamani anatumia procedure ya summary suit, kwa hiyo hana hata wajibu wa kuweza kujitetea na hatua tunachukua.

Kw ahiyo, niwaombe na kuwataka waajiri wote nchini kutimiza takwa hilo la kisheria ili tusije tukafikishana mahakamani na kuchukuliwa hatua kali zinavyostahili kwa mujibu wa sheria, ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, malalamiko haya ni mengi, hebu tusaidie, ni kazi ya nani kuhakikisha mwajiri anapeleka makato anayoyatoa kwenye mshahara wa mfanyakazi na ile anayotakiwa kulipa yeye kuhakikisha inaifikia Mifuko ya HIfadhi ya Jamii; ni kazi ya nani?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante kwa swali zuri; kwa mujibu wa sheria ambayo ilipitishwa na Bunge lako tukufu Sheria ya National Social Security Fund inasema wajibu ni wa mwajiri kufikisha, lakini sambamba na hilo ni wajibu wa mfuko pia kuweza kufanya ufuatiliaji wa michango hiyo kuhakikisha inafikishwa. Kwa hiyo ni pande zote mbili; mwajiri anao huo wajibu kwa mujibu wa sheria lakini mchango wanao ma-compliance officer kwa mujibu wa sehria katika utekelezaji nao NSSF au PSSF au mifuko hii ya hifadhi inapaswa kuendelea kumkumbusha mwajiri na kumpa notice. Na kwa sasa tayari kumekwishachukuliwa utaratibu wa kufungua akaunti ya kimtandao ya moja kwa moja, kila mwanachama sasa anapewa taarifa yake kupitia simu ya kiganjani. Kwa hiyo, kama michango haiendi kwa sasa tunawakamata.

Mheshimiwa Spika, kwa hili kwa kweli tunaendelea na operation kali kuweza kufanya ukaguzi ili kuweza kuhakikisha takwa hili la kisheria linatimia na wastaafu wetu wasisumbuliwe. Ahsante.

SPIKA: Nawaona Waheshimiwa nataka kwenda nalo vizuri, kwa sababu Ofisi za Wabunge zina malalamiko mengi sana ya wastaafu wa nchi hii na tukisema kwamba tutaliacha liendelee mtu anafuatilia mafao miaka miwili anaambiwa michango yako haikuja, kama ni kazi ya mwajiri kupeleka na mfuko unajua mwajiri hajapeleka, ni kazi yao, mfuko umlipe huyu mafao yake wao wakatafute fedha zilipo kwa sababu sio kazi yangu mimi kama mwajiriwa kuanza kusema fedha kama zilikuja ama hazikuja sio kazi yangu halafu huyu mwajiri mimi naweza kumuadhibu asipopeleka? Siwezi. Kwa hiyo, ni kazi ya mifuko kufuatilia fedha ambazo hazijalipwa na ndio maana sheria imeweka isipolipwa kuna riba inayotakiwa kulipwa.

Kwa hiyo, sidhani kama wananchi wanatakiwa kuteseka baada ya kuwa wamelipa kwenye mifuko na mwajiri ameshakata fedha. Ninyi Serikali mtengeneze utaratibu mzuri wa kuisimamia mifuko izitafute hizo fedha iwalipe wastaafu, wasataafu wasiwe wanaseka. (Makofi)

Waziri nakuona umesimama, nadhani tutapata tamko zuri hapo ili wastaafu wetu wawe na utulivu. Ahsante sana karibu Mheshimiwa Waziri wa Nchi.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri kuhusiana na hatua ambazo Serikali inafanya kuhakikisha kwamba wastaafu ambao wamelitumikia Taifa letu kwa uadilifu mkubwa hawapati usumbufu wa kupata mafao.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto ya baadhi ya waajiri kutopeleka michango yao katika mifuko na hivyo kusababisha wasataafu ambao michango haikupelekwa ama kutopata mafao yao kwa wakati au kupata mafao ambayo yana mapunjo.

Mheshimiwa Spika, nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba Serikali imeliona suala hili na tunalifanyia kazi ili kuweza kupata ufumbuzi kwa wale waajiri ambao madeni yao yameshakuwa ya muda mrefu yako ambayo yanafika miaka kumi, bado hajaleta hizo fedha. Kwa hiyo, nilihakikishie Bunge lako kwamba tayari Serikali inafanyia kazi, na niahidi kwamba ndani ya miezi miwili mitatu, tutakuja na muafaka wa kutatua tatizo hili ambalo limekuwa la muda mrefu.