Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Primary Question

MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika Kata za Ikoma, Roche, Gobire na Bukura zilizopo mpakani mwa Tanzania na Kenya?

Supplementary Question 1

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Kata ya Roche pamoja na Ikoma kujumuishwa katika Kata 763 ambazo utekelezaji wake kwa maana ya zabuni kutangazwa mwezi Oktoba, lakini kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa sana wa ujenzi wa minara maeneo mengi nchini hata pale panapokuwa no objection imetoka, lakini bado ujenzi wa minara mingi nchini unakuwa umechelewa.

Nilitaka nipate kauli ya Serikali juu ya hili kwamba ni nini kinasababisha pamoja na kwamba no objection inakuwa imetoka lakini ujenzi wa minara inachukua miaka miwili mpaka mitatu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ni mara ya tatu nauliza swali hili Kata ya Bukura, Kata ya Ikoma, Goribe pamoja na Roche ni kata ambazo ziko mpakani, lakini haziwasiliani hakuna mawasiliano ya Kitanzania.

Nilitaka nijue kwa sababu hiyo ya kukosa mapato pamoja na usalama wa Kata zile nini kauli ya Serikali juu ya ujenzi na utekelezaji wa minara maeneo ya mpakani kwa dharura na kwa haraka ili kusaidia maeneo yale ya kimpakani ndani ya nchi yetu? (Makofi)

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Answer

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ni kweli kwamba imekuwa inatuchukua miezi tisa mpaka 12 kujenga mnara ambayo ndio ilikuwa hali iliyokuwa imezoeleka na sababu yake ni moja tulikuwa tunatumia miezi sita kutafuta vibali mbalimbali vya kujenga hiyo minara kwenye maeneo husika, lakini tunashukuru Wizara ya Mazingira chini ya kaka yangu Mheshimiwa Jafo sasa wamerahisisha badala ya kutumia kwa miezi sita tumeweza baadhi ya maeneo ikiwemo Zanzibar kupata vibali ambavyo tulikuwa tunatumia miezi sita tumepata kwa mwezi mmoja na hivyo muda wa kujenga minara umepungua sana. Uzoefu uliotokea Zanzibar tumejenga kwa siku 90 kwa hiyo, tunaamini hata eneo hili tutakapopata no objection mradi huu utachukua miezi isiyozidi minne na tuna hakika kwamba utakuwa umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kata husika alizozitaja ni kweli ziko mpakani na yeye na Mkuu wake wa Wilaya wamekuwa wakiwasiliana na sisi mara kwa mara. Changamoto iliyotupata ni kwamba tulipotangaza tender ya kujenga minara kwenye maeneo haya, hawakupatikana wajenzi tukarudia kutangaza mara ya pili na bado mkandarasi hakupatikana.

Tulichoamua tumeamua kuchukua miradi kwenye kata hizi na kuingiza kwenye Tanzania ya Kidigitali ambayo package yake kidogo ni nzuri. Kwa hiyo, wakandarasi watapatikana, nimtoe shaka nia yetu ni kuhakikisha maeneo ya mipakani inapata mawasiliano ya kutosha na hasa kwa sababu biashara ya mpakani ni kubwa na sisi tunapenda kufanya biashara kwenye maeneo hayo. Nimhakikishie kwamba minara hii itajengwa na itajengwa kwa wakati. (Makofi)