Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hamida Mohamedi Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Lindi Mjini

Primary Question

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatoa fedha kutekeleza mradi wa ujenzi wa soko kuu na stendi ya mabasi Lindi Mjini?

Supplementary Question 1

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu hayo ya Serikali, majibu ambayo sasa yanaleta matumaini kwa maana mradi huu umekuwa wa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina swali la nyongeza, lakini nina maombi kwa Serikali. Mheshimiwa Waziri Innocent Bashungwa alikuja Lindi tarehe 29 Julai, kwenye Maadhimisho ya Sherehe ya Kumpongeza Mheshimiwa Rais. Katika mambo ambayo tulimwomba ni suala zima la utekelezaji wa mradi huu wa TACTIC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Lindi tuna mapokeo ya mradi wa LNG, tunahitaji sasa kuboresha miundombinu mbalimbali. Kwa hiyo, naiomba Serikali kuhakikisha kwamba wanatuharakishia huo mwezi Januari ambao wameuahidi katika utekelezaji wa mradi huu.

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nampongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde kwa kujibu kwa ufasaha, pia na Mheshimiwa Hamida Abdallah kwa ufuatiliaji wa mradi huu ambao Waheshimiwa Wabunge kutoka miji 45 wamekuwa wakiufuatilia kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni maelekezo ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwamba baada ya Serikali kusaini na benki ya dunia Juni, 16 mwaka huu 2022, Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan alituelekeza kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya TACTIC unaanza mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Waheshimiwa Wabunge, kwenye tier one, miji 12 kwa maana ya majiji tayari kama nilivyosema, mkataba ulisainiwa na Serikali na Benki ya Dunia Juni 16 na usanifu wa miji 12 umeshakamilika. Sasa hivi kazi ya kutangaza kwa ajili ya kupata wakandarasi itafanyika muda wowote ili kazi zianze Machi, 2023 kwa ile miji 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini tunafanya kwenye miji 15 ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameisema? Tunafanya kila aina ya jitihada kuhakikisha tier one na tier two zina-overlap katika utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Hamida Abdallah, pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwenye miji 45 msiwe na wasiwasi, ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan baada ya kusaini Mkataba na Benki ya Dunia mwaka huu 2022, utekelezaji wake wa tier one, tier two na tier three viweze Kwenda kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu tuna group la TACTIC na mnafuatilia kwa karibu sana, tutakuwa tunaandaa vikao ili kuwapa mrejesho wa utekelezaji wa miradi hii utakavyokuwa unaenda. Ahsante sana. (Makofi)