Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Michael Mwita Kembaki
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Mjini
Primary Question
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: - Je, kwa nini darasa la saba wanafanya mtihani wa Taifa mwezi Septemba, wakati mtaala unaelekeza masomo yakamilike mwisho wa mwaka?
Supplementary Question 1
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi Wizara imekuwa ikitoa tamko la kuzuia masomo ya ziada katika Shule za Msingi na ilhali wakijua kwamba muda wa ukamilishaji wa mtaala unakuwa hautoshi. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inatenga muda ambao watoto hao watasoma wakamilishe mtaala wao kwa wakati?
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba Walimu wanapaswa kutafuta muda wa kukamilisha mtaala huu kwa mpango kazi ambao wanao. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapa motisha Walimu hawa ambao wanafanyakazi hii ngumu ya kuhakikisha kwamba elimu inatolewa kwa wakati? Ahsante. (Makofi)
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kembaki Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishajibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba katika mwaka tunazo siku 365, kati ya siku hizo 365 tunatumia siku 194 kwa ajili ya kukamilisha mitaala katika mwaka husika wa masomo. Najua maono ya Mheshimiwa Mbunge kwenye eneo hili, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa vile hivi sasa tunapitia Sheria yetu ya Elimu tunapitia mitaala pia tunapitia sera ya elimu, bado hatujaona changamoto kwa hizi siku 194 kwenye utekelezaji wa mitaala hii kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, kwa vile bado tunaendelea kubeba au kuchukua maoni tunaomba tubebe vilevile maelezo yake haya tuweze kuyaingiza kwenye rasimu yetu ya mitaala inayokuja ili tuweze kuangalia kama hizi siku 194 zitatosheleza au hazitatosheleza au kama kutakuwa na changamoto yoyote tuweze kufanya marekebisho. Hilo eneo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili la motisha, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imekuwa ikitoa motisha au kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria. Kama tunavyofahamu katika kipindi kilichopita Mheshimiwa Rais aliongeza mshahara siyo tu kwa watumishi kama walimu, lakini kwa watumishi wote. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kufanya hivyo kwa kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu ili watumishi wote waweze kupata stahiki zao kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved