Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ritta Enespher Kabati
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: - Je, ni maeneo gani yametambuliwa kuwa na madini Mkoani Iringa?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri kwamba Mkoa wetu wa Iringa na sisi tuna madini ya kutosha. Mkoa wetu wa Iringa tunao Mgodi wa Nyakavangala uko katika Jimbo la Isimani. Na kwa kuwa taarifa ya jiorojia na utafiti, inaonesha kwamba eneo hilo limeshaonesha. Je, ni hatua gani sasa inayofuata ili wachimbaji wa eneo hilo waweze kuchimba kwa tija na ili Mkoa wetu wa Iringa uweze kupata mapato kutokana na madini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nipongeze sana wanawake waliothubutu kuanza uchimbaji wa madini nchini, na sasa wameanzisha chama cha TAWOMA. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha wanawake wengi zaidi waweze kuchimba madini nchini na ukizingatia sensa inaonesha kwamba wanawake tuko wengi zaidi na Mheshimiwa Waziri alisema tunalipa vizuri?
Nimpongeze Mheshimiwa Rais alifungua uwekezaji mkubwa sana wa mwanamke pale Geita, Sarah Masasi, ili wanawake wengi tuweze kuchimba madini na kuwekeza katika madini nchini. Ahsante sana.
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali lake la kwanza kwamba kwa kuwa utafiti wa awali umeshafanywa na taasisi zetu kubaini uwepo wa madini ya dhahabu katika eneo la Nyakavangala, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua zinazofuata sasa ni kufanya utafiti wa jiofizikia ambao ndio unaohitajika kwa sasa ili usaidie kutambua mikondo inayoweza kuwa na mashapo ya dhahabu, na kwa njia hiyo wale wachimbaji waweze kuchimba kwa tija. Aidha, GST kwa kushirikiana na STAMICO sasa wamepanga kwenda kuendelea na utafiti katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali lake la pili, ni kwamba Serikali ya Mama Samia kwa kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi unaotutaka tuwape wachimbaji wadogo wakiwepo wanawake maeneo ya kuchimba madini imetuagiza sisi tuendelee kuwa walezi wa sekta ndogo ya wachimbaji wakiwepo wanawake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kutekeleza hilo sisi Wizara ya Madini, kwanza tumeteua mabalozi wa madini ambao Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati ni moja wa mabalozi na vinara wa madini hapa nchini, kazi ambayo anaifanya kwa dhati, na mpongeza kwa kuleta swali hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi mamia kwa maelfu ya wanawake wanafaidika kupitia mnyonyoro wa sekta hii ya madini. Zaidi ya leseni 20 zimeshatolewa kwa vikundi mbalimbali vya wachimbaji wa madini. Na wanawake hawa wamekuwa wakichangia pia katika kukusanya maduhuli ya Serikali. Kwa mfano kikundi kimojawapo cha TAWOMA mshikamano kilichopo katika eneo la Nyamisiga, Halmashauri ya Msalala kule Kahama wamechangia ujenzi wa zahanati. Hizo ni juhudi kuonesha kwamba Wizara imezingatia suala hili la uchimbaji wa wanawake wadogo, na ninampongeza sana Mheshimiwa kwa kuleta swali hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kuwaomba wanawake popote walipo Tanzania kwenye madini wajiingize katika biashara hii maana ina tija na Serikali inawatambua na itawa-support.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved