Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: - Je, kuna mkakati gani wa kuiwezesha TTCL kuunganisha Wateja wengi kwenye Mkongo wa Taifa kwa punguza gharama za kuunganisha?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini niseme, tumejua kwamba uwekezaji kwenye TTCL unaweza ukageuka kuwa ni mkakati mzuri wa kuongeza mapato ya Serikali. Tatizo la kuunganisha watu linatokana tu na gharama hizo, njia mojawapo ya kupunguza gharama hizo ni kuiwezesha TTCL kupata mtaji au kupata mkopo kwa kupata dhamana au kwa kutumia dhamana ya Serikali ili iweze kuwaunganisha watu na kuwachaji polepole, kidogokidogo kwa miaka miwili mitatu, hizo gharama zitakuwa ndogo na watu wataomba kujiunga kwenye mkongo huu ambao ni cha msingi sana.

Mheshimiwa Spika, suala la pili ni kwamba siku za karibuni tumesikia kwamba TCRA inataka kugawa masafa ya spectrum za 5G na tunajua kwamba nchi hii zama hizi ni zama za internet of things na ni Artificial Intelligence tunaingia na inahitajika sana 5G. Naomba niiulize Serikali, je, imejipanga namna gani kuiwezesha TTCL kupata masafa ya kutosha ya 5G katika ugawaji wa spectrum hizo?

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Answer

WAZIRI WA HABARI MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza anauliza Serikali kama iko tayari kuliwezesha Shirika la Mawasiliano (TTCL) kupata mtaji. Majibu ni kwamba pamoja na kwamba tumeendelea kuwekeza hata Bajeti hii iliyopita hapa Serikali imetenga zaidi ya bilioni 150 kwa ajili ya kujenga mkongo. Huu mkongo tunaukabidhi sasa kwa TTCL ili waweze kuuendesha kibiashara ikiwemo kutafuta fedha kwenye vyombo vya fedha kwa ajili ya kujenga, kuimarisha na kuwahudumia wateja wao. Uamuzi huu utaboresha huduma na kuipa mtaji TTCL.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kama tuko tayari kutoa upendeleo maalum kwenye umiliki wa spectrum. Ni kweli kwamba internet of things ndio dunia inakokwenda na ni kweli kwamba 5G itakwenda kubadilisha matumizi hayo, lakini kama Serikali mauzo ya hizi spectrum tunayauza kwa uwazi na tunataka kila mmoja akashiriki na hatuna mpango wa kumpendelea mtu. Hivi juzi tumefanya mnada, tukapata zaidi dola milioni 187 kwa sababu mnada ulitenda haki, kila mmoja aliingia sokoni, akashindana akapata ambacho alikuwa anastahili kupata.