Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Sylivia Francis Sigula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Bandari Kavu katika Mkoa wa Kigoma?
Supplementary Question 1
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwanza kwa majibu mazuri ya Wizara, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Katosho wamepisha eneo la ujenzi wa bandari ya nchi kavu kwa zaidi ya miaka sita sasa na majibu haya ya usanifu yamekuwa yakitolewa kwa zaidi ya miaka sita na kuwaumiza sana wananchi: Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuharakisha huu upembuzi yakinifu ili eneo hilo lifanyiwe kazi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ili bandari ya nchi kavu iweze kuwa na tija kwa Taifa lazima kuwe kuna miundombinu wezeshi ikiwemo uwepo wa reli, uwepo wa meli, uwepo wa mabehewa ya kutosha na barabara za uhakika. Ukizingatia Mkoa wa Kigoma bado tuko nyuma sana kimiundombinu: -
Mheshimiwa Spika, nini mpango wa Serikali kuhakikisha miundombinu wezeshi inatekelezeka ili bandari hii iwe na tija?(Makofi)
Name
Atupele Fredy Mwakibete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba bandari hii imechukua muda mrefu, lakini tangu mwaka 2019 tulijenga uzio ama ukuta wa eneo hili. Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Kigoma kwamba ifikapo Aprili mwakani 2023 upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unakwenda kukamilika na tayari tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bandari hii.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili angependa kufahamu miundombinu wezeshi katika kufanikisha bandari yetu kavu na miundombinu hiyo wezeshi ni pamoja na reli, barabara na kupata mzigo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, bandari hii kavu tayari ipo karibu kabisa na bandari nyingine ya Kigoma, pia ipo karibu kabisa na barabara kuu inayokwenda Kigoma Mjini. Pia tumewaelekeza mamlaka ya bandari nchini pamoja na TRC, wapo kwenye majadiliano kwa ajili ya kupeleka reli ili iwe rahisi kupeleka mzigo utakaokuwa unahudumiwa na nchi rafiki na nchi jirani kati ya Congo, Rwanda, Burundi pamoja na Zambia. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved