Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Halima James Mdee
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: - Je, Serikali ina kauli gani juu ya ushuru mkubwa wa bidhaa za ngozi unaotozwa bandarini na vikwazo vya kusafirisha bidhaa hiyo nje ya nchi?
Supplementary Question 1
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa majibu ya Waziri yanakiri kwamba ushuru mkubwa ulilenga kulinda viwanda vya ndani na ni asilimia 80 ya thamani ya mzigo ukiwa bandarini, sasa kuna ushahidi ulio dhahiri kwamba viwanda vya ndani vilivyokuwa vikilindwa vingi vimekufa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna kiwanda cha Himo ambacho na chenyewe kiko hai, lakini ngozi inayohitajika ni ya kilogram 12 ambayo inapatikana Bukoba. Sasa swali langu kwa Serikali, wafanyabiashara wa ngozi wamekwama ushuru mkubwa, viwanda vya ndani vimekufa, Serikali haipati mapato ya kutosha. Sasa, je, kwa kuzingatia kwamba hata Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki linapokuja suala la masilahi ya ndani na yenyewe wala haitekelezi makubaliano yenu, kwa nini Serikali isifanye tathmini upya, kuangalia uamuzi wake ili kulinda wafanyabiashara wa ndani wa Ngozi na kulinda nchi? Hilo swali langu la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tunaingia mwaka mpya wa fedha, tunaamini Wizara ya Mifugo chini ya Mawaziri akiwemo kijana makini, hivi bado hawajafikiria mwaka huu wa kikodi kuangalia hili eneo muhimu? Kwa sababu ni dhahiri shahiri kuna ngozi zinaoza huko mtaani kwa maelfu, hawajaangalia hili eneo ili wasaidie nchi? (Makofi)
Name
Abdallah Hamis Ulega
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Halima James Mdee, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni juu ya tathmini Serikali kutazama kulingana na hali halisi ya biashara ya Ngozi. Nimelipokea jambo lake hili la kusema tufanye tathmini ni jambo jema.
Vilevile nimshukuru amekiri na ndio ukweli wenyewe kwamba tumeweka viwango hivi vya kikodi ndani ya Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki kwa lengo la kulinda viwanda vyetu vya ndani. Hii 80 percent tuliyoiweka imewekwa makusudi kwa ajili ya ku-discarage kutoa ngozi ikiwa ghafi kwenda nje ya mipaka ya Taifa letu ili kulinda ajira na kupata kipato zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niseme ukweli bado ngozi nyingi inakwenda nje ikiwa ghafi, pamoja na ushuru huo mkubwa inakwenda Nigeria, Ghana ambako huko wanaitumia kama chakula, kwa hiyo hili lifahamike. Hii ngozi tunayosema kwamba iko vijijini inaharibika, inawezekana lakini kwa uhitaji wa ngozi wa sasa jambo la ngozi kuharibika ni kiasi kidogo sana, yawezekana wahitaji wanaohitaji hizi ngozi hawajaweza kuvifikia vile vijiji ambavyo vina hiyo ngozi inayoharibika. Hata hivyo, niseme tu kwamba tutaimarisha sasa mfumo wetu ili hata ile iliyoko kule vijijini iweze kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, amezungumza juu ya maboresho ya kikodi. Hili jambo pia vilevile nimelichukua, kwa ajili ya kuweza kuangalia maslahi mapana ya sekta hii ya ngozi.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved