Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hawa Mchafu Chakoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza: - Je, ni wanafunzi wangapi waliokuwa wajawazito na wangapi wamerejeshwa shuleni baada ya agizo la Mheshimiwa Rais?
Supplementary Question 1
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa sababu zilizopelekea wanafunzi wengi kupata ujauzito wakiwa mashuleni ni mazingira ya ukatili, unyanyasaji na umaskini uliokithiri kwa maeneo wanayoishi.
Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuwaweka wasichana hao katika shule za mabweni ili waweze kupata kusoma kwa utulivu na kuondokana na mazingira yale?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, agizo la kurejesha wasichana waliopata ujauzito mashuleni linatekelezwa chini ya Waraka wa Elimu Na. 2 wa mwaka 2021.
Kwa nini sasa Serikali isitunge sheria juu ya suala hili ili asije kutokea Kiongozi mwingine akataka kubadilisha jambo hili lenye dhamira njema?
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uthubutu wake wa kuhakikisha kwamba wanafunzi hawa waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo na hii ya ujauzito wanarudi shuleni. Nini mikakati ya Serikali kwa hivi sasa?
Mheshimiwa Spika, mikakati ya Serikali kwa hivi sasa, Mheshimiwa Rais ameridhia ujenzi wa shule 26 za wasichana katika kila Mkoa ambapo ujenzi huu tunajenga kwa awamu, tayari ujenzi wa shule 10 umeshaanza kwenye Mikoa 10 mbalimbali katika awamu ya kwanza kwa lengo la kuhakikisha kwamba tunapata mabweni kwa ajili ya wanafunzi hawa kukaa katika mazingira mazuri na salama ya kujifunza na kujisomea.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni ujenzi wa hostel kwenye maeneo ambayo tunaona kwamba kuna umuhimu wa kujenga hostel kwenye maeneo hayo pamoja na mabweni katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa tatu ni kuanzisha vitengo vya elimu, unasihi pamoja na ushauri kwenye shule zetu kwa lengo la kuhakikisha kwamba vitendo hivi havijitokezi kwenye maeneo hayo. Hatua ya mwisho ni kuchukua hatua kwa wale wote waliothibitika kujihusisha kwa namna moja ama nyingine kunyanyasa wanafunzi wetu na kuwakatizia masomo, hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi yao. Hiyo ndiyo mikakati mikubwa ya Serikali ili kuhakikisha jambo hili tunakwenda kulikomesha kabisa katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili amezungumzia waraka namba mbili wa mwaka 2021. Ni kweli urejeshaji wa wanafunzi katika shule waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali ni waraka ambao umetoka mwaka 2021 na ni mwaka mmoja tu hivi sasa toka waraka huu tuweze kuanza kuutekeleza.
Ninamuomba Mheshimiwa Mbunge aridhie Serikali inaendelea kufanya tathmini ya utekelezaji wa waraka huu ili kuweza kubaini changamoto zilizopo, lakini vile vile na mafanikio yaliyopo katika waraka huu. Ikiwa tutaona kwamba kuna haja ya kutengeneza sheria maalum na kwa vile sasa tunafanya mapitio ya sheria pamoja na sera yetu ya elimu, tunaweza kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved