Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, ni nini mkakati wa Serikali kuondoa kero ya ukatikaji wa umeme nchini hasa katika maeneo ya biashara kama Kariakoo?

Supplementary Question 1

MHE. HAWA S MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nisikitike sana sijui kama swali langu lilieleweka vizuri kwa sababu mimi nilitaka kufahamu kwa nini umeme unakatika katika kwenye maeneo ya biashara, sikutaka kujua kwanini umeme unakatika kwenye nchi nzima kwa sababu najua tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo ningetamani kufahamu nini mkakati wa Serikali kuacha maeneo ya biashara nyakati za mchana yaweze kufanya kazi kwa kutokukata umeme na umeme huo wakakata nyakati za jioni ili kama kuna matengenezo yoyote yaweze kuendelea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, umeme umekuwa ukikatika mara tano kwa siku katika siku saba katika Soko la Kariakoo, sehemu ambayo wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifanya biashara zao. Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa mgao wa umeme katika Soko la Kariakoo na maeneo mengine ya biashara wakati wa mchana ili watu waweze kufanya biashara zao na usiku waendelee na utaratibu wao? Ahsante.

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza yla Mheshimiwa Mwaifunga, kama ifuatavyo: -

Mwenyekiti Mheshimiwa, nianze na la kwanza la jumla kwamba umeme unapokatika hauchagui sehemu za kukatika kwa sababu njia inakuwa ni ndefu sana. Hata hivyo, kwa sababu Serikali inafahamu kuna changamoto hiyo, ndio sasa imetengeneza huu mradi ambao unakwena kuondoa matatizo ya ukatikaji wa umeme katika maeneo yote nchini. Hata hivyo kwa umaalum wa maeneo ya biashara kama ambavyo Mheshimiwa Mwaifunga amesema, Mwezi Februari katikati mbele ya Mheshimiwa Rais tunatarajia kusaini miradi ya kupeleka umeme kwenye maeneo maalum ya kibiashara ambayo imeanzishwa project inayoitwa Project Mapato katika Shirika letu la TANESCO na ikilenga hasa kwenye maeneo haya hasa ya kibiashara ili yapate umeme wa uhakika muda wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umahsusi wa soko letu la Kariakoo, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba soko la Kariakoo linapokea umeme kutoka kwenye Vituo vya Kupooza Umeme vinne, vya Ilala, Posta, Mnazi mmoja na Station na inapokea umeme kwa njia za kuleta umeme tunazoziita feeders 13 kutoka kwenye haya maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ilikuwa ni kuhakikisha kwamba haya maeneo yanasaidiana katika kupeleka umeme kwenye eneo hili. Ni kweli kwamba eneo la Kariakoo linapata shida ya umeme mara kwa mara lakini ni kwa sababu ya shughuli ambazo zinaongezeka pale na pengine tunakuwa hatuna taarifa. Hata hivyo, tulichokubaliana ni kuongeza uwezo wa transformer zilizoko kwenye eneo lile ili kuhakikisha kwamba umeme unapatikana muda mwingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kugawana umeme huyu apate mchana, huyu apate usiku ni kulingana na maeneo ya uhitaji. Kwa sababu kuna maeneo mengine ya biashara yanahitaji umeme mchana na kuna maeneo mengine yanahitaji usiku na pengine muda wote. Ninachoweza kuwahahikishia Waheshimiwa Wabunge ni kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha meneo yote ya kibiashara yanapata dedicated lines maalum kwa ajili ya kuhakikisha umeme unapatikana muda wote katika maeneo hayo. Hivyo hilo litafanyika kupitia Project Mapato lakini na TANESCO itaendelea kulitazama eneo la kariakoo kama eneo maalumu la kimkakati kwa ajili ya kuhakikisha umeme unapatikana muda wote. (Makofi)

Name

Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, ni nini mkakati wa Serikali kuondoa kero ya ukatikaji wa umeme nchini hasa katika maeneo ya biashara kama Kariakoo?

Supplementary Question 2

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ngara. Jimbo la Ngara ni miongoni mwa majimbo ambayo bado yana kata hazijawahi kuona hata nguzo moja ya umeme. Mathalan kata ya Bugarama, Keza, Kibogora pamoja na Muganza wananchi hawa hawajafikiwa na miundombinu ya umeme. Naomba sasa kuiuliza Serikali, je, ni lini wananchi wangu hawa watapelekewa huduma ya umeme? Ahsante sana.

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote ya kata na vijiji ambayo hayajapata umeme yako katika mpango wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa pili ya upelekaji wa umeme katika maeneo hayo na mradi huo tunatarajia mwishoni mwa mwaka huu uwe umekamilika. Ni kweli kuna maeneo yamesuasua kwa muda mrefu katika upelekaji wa umeme na Mkoa wa Kagera ikiwa ni mmojawapo. Tumechukua jitihada za makusudi za kukaa na Wakandarasi hao na kuwasimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika muda mfupi sana ataona Wakandarasi wakirudi kwenye maeneo hayo kuweza kufanya kazi na kutimiza ndani ya muda na tulipeana hadi muda mfupi wa miezi mitatu kuhakikisha maeneo ambayo hayajafikiwa kabisa sasa miundombinu imefika. Kwa hiyo tutapeana taarifa na Mheshimiwa Mbunge ya ufikaji wa Mkandarasi kwenye maeneo hayo na utekelezaji wa mradi kwa mujibu wa mkataba.

Name

Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, ni nini mkakati wa Serikali kuondoa kero ya ukatikaji wa umeme nchini hasa katika maeneo ya biashara kama Kariakoo?

Supplementary Question 3

MHE. KUNTI Y MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna changamoto kubwa ya umeme nchini lakini wamekuwa wakikata umeme bila kuwapa taarifa wateja wao na kusababisha uharibifu mkubwa wa vifaa vya majumbani, lakini pia na miundombinu ya viwandani. Je, Serikali sasa iko tayari kuanza kuwalipa fidia wateja wao wanaoathirika na kukatika kwa umeme?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Majala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukatikaji wa umeme ni wa aina mbili, kuna kukata kwa vile tumepanga kukata ili tufanye matengenezo, lakini kukatika kwa sababu ya hitilafu ambazo ziko hata nje ya uwezo wa binadamu. Katika vitu ambavyo Shirika letu la TANESCO limejitahidi sana kufanya ni kutoa taarifa ya makatizo ya umeme yale ambayo tumeyapanga. Kiukweli katika hilo Myonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Tumewaelekeza na wamejitahidi katika siku za hivi karibuni matengenezo ambayo yanafanyika tunahakikisha tunayaratibu na taarifa zinatolewa kwa wateja wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye yale makatizo ambayo hatukuyatarajia, ni mashine imezidiwa kama ndugu zetu wa Kariakoo. Juzi tarehe 23 transformer moja ilipata hitilafu kwa sababu ilipokea mzigo mkubwa kuzidi ilivyotarajia, mvua zimenyesha, waya zimekatika na vitu kama hivyo. Tunaendelea kuhakikisha kwamba matukio hayo hayatokei. Hata hivyo tunaweza kufika kwenye utaratibu wa kawaida kuona namna gani ambayo sheria inaweza ikachukuliwa ili sasa ambaye anastahili kupata haki fulani anaweza kuipata kwa mujibu wa sheria tulizonanzo.

Name

Asia Abdulkarim Halamga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, ni nini mkakati wa Serikali kuondoa kero ya ukatikaji wa umeme nchini hasa katika maeneo ya biashara kama Kariakoo?

Supplementary Question 4

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Umeme Wilaya ya Hanang kwa kuwa kwa sasa kituo kinachotumika ni cha Babati na hivyo inaendelea kuleta changamoto kubwa kwa watumiaji wa umeme ndani ya Wilaya ya Hanang?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifanya utafiti na kubaini maeneo yanayohitaji Vituo vya Kupoza Umeme na vimetengwa katika awamu tatu. Kuna wale ambao wana mahitaji makubwa sana tumewaweka kwenye group la kwanza; kuna wale ambao mahitaji yao kidogo yanaweza kuvumilika wako group la pili; na kuna wale amabo wananaweza wakasubiri mpaka baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mradi ambao niliotangulia kuutaja wa Grid Imara ambao unakaribia jumla ya trilioni moja na bilioni 900 unatekelezwa kwa miaka minne. Kwa kuanzia tumepewa bilioni 500 na tutajenga Vituo vya Kupoza Umeme 15 katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda kuangalia kama eneo la Hanang ni eneo mojawapo ambalo limeoneka lina uhitaji wa kituo cha kujengwa haraka namna hii au kitakuja baadaye kidogo. Hata hivyo, nitoe taarifa njema kwa Waheshimiwa Wabunge, mradi huu utakapokamilika 2025/2026, tunatarajia kila wilaya itakuwa ina Kituo cha Kupoza Umeme cha Gridi katika wilaya husika ili kuzuia waya kuitembea kwa muda mrefu na hivyo umeme kupotea.