Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jesca Jonathani Msambatavangu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Primary Question
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: - Je, kuna mkakati gani wa kutochelewesha vibali vya kuruhusu umeme kupita kwenye hifadhi za misitu ili kuwahisha usambazaji umeme vijijini?
Supplementary Question 1
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mepesi ya Serikali naomba nitoe ushauri mmoja lakini pia niwe na swali moja la nyongeza. Kwanza tuwaombe Wizara ya Maliasili, pamoja na dhamana kubwa waliyopewa ya kulinda maliasili za Taifa letu, lakini wajue wana wajibu pia wa kuruhusu Watanzania wahudumiwe bila wao kuwa kikwazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, eneo la Hifadhi ya Msitu Kihesa, Kilolo ni eneo ambalo limepitia mchakato mkubwa mpaka kutengwa kwa ajili ya kujenga Kituo cha Utalii Kusini. Nilikuwa nataka kuuliza, maana swali hili tunaliuliza tangu Januari, 2021 na tunapata majibu yasiyokuwa straight; naomba leo Mheshimiwa Naibu Waziri atuhakikishie hapa: Ni lini hasa ujenzi wa Kituo cha Utalii Kusini Kihesa, Kilolo utaanza chini ya mradi wa REGROW kwa sababu miradi mingine yote ya REGROW inaendelea na imeanza, kasoro Kituo cha Utalii Kusini cha Kihesa, Kilolo.
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Jesca kwa namna ambavyo anaendelea kufuatilia mradi huu wa ujenzi wa Kituo cha Information Center ambacho kitasaidia upatikanaji wa ofisi mbalimbali na pia kuwezesha masuala ya utalii ili yaweze kuendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba natambua kwamba wananchi wa Iringa wana hamu kubwa sana ya ujenzi wa jengo hili ambalo linatarajiwa kujengwa ghorofa tano pamoja na jengo lingine la Kituo cha Utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ujenzi huu unatarajiwa kuanza mwezi Mei na sasa hivi tulikuwa tuna mkandarasi ambaye alikuwa anaangalia michoro, na michoro tayari imeshakamilika, na kulikuwa kuna marekebisho kidogo na utaratibu sasa wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi umeshaanza. Hivi ninavyoongea, tunatarajia kumpata na mwezi wa Tano ujenzi unaanza. Pia nimhakikishie kwamba tuko ndani ya muda, na ujenzi huu unatarajiwa kukamilika mwaka 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine amesema ni ushauri, tunaupokea lakini nataka nimkumbushe tu kwamba utaratibu wa utoaji wa vibali kwenye maeneo ya misitu ambapo unatarajiwa miti kukatwa, unategemea hasa hasa mteja anayetarajia kupitisha nguzo za umeme awe amekamilisha kulipa tozo zote zinazotakiwa.
Mheshmiwa Mwenyekiti, misitu hii inasimamiwa na Serikali Kuu kupitia Wakala za Huduma za Misitu Tanzania, lakini kuna misitu mingine inasimamiwa na Halmashauri na mingine ni misitu ya vijiji. Kwa misitu ya Halmashauri na Vijiji, tuna kamati za uvunaji ambazo zinasimamiwa, ziko chini ya Wilaya. Kamati hizo pia zinatoa vibali baada ya kuwa mteja amekamilisha taratibu zote za ulipaji wa tozo. Tozo hizi zinasimamiwa na Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: - Je, kuna mkakati gani wa kutochelewesha vibali vya kuruhusu umeme kupita kwenye hifadhi za misitu ili kuwahisha usambazaji umeme vijijini?
Supplementary Question 2
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri amelieleza Bunge lako Tukufu hapa kwamba hamna ucheleweshaji wa kutoa vibali vya kupitisha umeme kwenda vijijini. Sasa nataka kujua, Wizara ya Nishati ilikuja kwenye Kamati ya Bajeti, wakaeleza kwamba moja ya kikwazo kikubwa cha kuchelewesha kupeleka umeme vijijini ni kuzuiwa au kucheleweshwa kwa vibali na TFS. Leo Mheshimiwa Waziri anaeleza kwamba hakuna huo ucheleweshaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua katika hizi Wizara mbili ambazo ni za Serikalini, ni yupi anaongea uongo katika kuhakikisha kwamba umeme unafika vijijini kwa wananchi? [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
MWENYEKITI: Mheshimiwa Matiko hilo neno la uongo naomba uliondoe.
MBUNGE FULANI: Uongo!
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua Wizara ya Nishati na Wizara ya Maliasili na Utalii ni Wizara ambazo ziko ndani ya Serikali...
MWENYEKITI: Imeshaeleweka, ipi ipo sahihi?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naondoa “uongo”, sasa nanyoosha vizuri swali.
MWENYEKITI: Eeeh, ndiyo.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaliambia nini Bunge na wananchi kinachochelewesha umeme kwenda vijijini wakati nyie ni Wizara mbili ambazo mpo ndani ya Serikali, siyo kwamba ni kutoka hata kwenye sekta binafsi? (Makofi)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kusema Wizara zote mbili; ya Nishati na ya Maliasili na Utalii zimesema ukweli. Nataka nimhakikishie tu kwamba Wizara hizi zinafanya kazi kwa ushirikiano. Kabla Wizara ya Nishati haijatekeleza miradi yake, ni lazima mteja awe amekamilisha taratibu zote ikiwemo malipo ya tozo. Kama hajalipa tozo, basi vibali hawezi kuvipata kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niliseme hili wazi kwamba wateja wengi wanasingizia kwamba vibali vinacheleweshwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, lakini ili nikupe kibali, ni lazima uwe umetekeleza masharti yote ikiwemo ulipaji wa tozo. Sasa kama tozo umeshamaliza kulipa, kwa nini mimi nikunyime kibali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndivyo utaratibu unavyotakiwa na wateja wengi wanataka tusamehe ulipaji wa tozo. Kwa hiyo, kama mteja anahitaji kusamehewa tozo, basi awasilishe kwenye mamlaka husika ambayo ni Wizara ya Fedha, na Waziri mwenye dhamana ataangalia kama kuna haja ya kutoa msamaha, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved