Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Omari Mohamed Kigua
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Primary Question
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kilindi?
Supplementary Question 1
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nimshukuru pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani kwa majibu yenye kutia matumaini kiasi, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Wazari kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi imetenga eneo kwa ajili ya Kituo cha Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa sababu eneo hilo limetengwa takribani miaka ishirini iliyopita je, ni utaratibu upi au mipango ipi au ni parameter zipi ambazo zinatumika kuhakikisha kwamba mnajenga Vituo vya Polisi kwa kuangalia uhalisia wa mahitaji ya eneo husika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye sasa hivi ni Waziri wa Mambo ya Ndani alikwishatembelea Wilaya ya Kilindi na kujionea uhalisia wa changamoto ya Kituo cha Polisi jinsi kilivyo.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kutoa commitment kwa wananchi wa Wilaya ya Kilindi kwamba mwakani watajenga Kituo cha Polisi? Ahsante.
Name
Sagini Jumanne Abdallah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwa na ahadi zinatolewa na zimechukua muda mrefu, hususan kituo hiki, eneo limetengwa muda mrefu kama alivyosema miaka 20, na ametaka tuseme tutazingatiaje uhalisia wa maeneo husika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, tunapotaka kujenga eneo lolote lazima tuzingatie uhalisia wa eneo. Ndiyo maana wataalam wetu wanakwenda kule kufanya tathmini ya udongo ili kuweza kujiridhisha vifaa na kiwango gani cha ujenzi utakaohitajiwa. Kwa hiyo, watakapokuwa wanaanza ujenzi, mahitaji halisi ya eneo la Mheshimiwa Mbunge yatazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hili la commitment nimesema, tutatenga kwenye bajeti ya 2023/2024. Sasa bajeti yetu ikishapita hapa, namwomba Mheshimiwa Kigua asome maeneo yatakayojengewa vituo, atajiridhisha kwamba eneo lake litakuwa na mpango huo wa ujenzi. Nashukuru. (Makofi)
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kilindi?
Supplementary Question 2
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Jimbo la Mlalo, Vituo vya Polisi vya Mlalo na Mtae vipo katika majengo ambayo ni ya Serikali za Vijiji: Je, Serikali ina mpango gani sasa kujenga majengo ya Polisi katika tarafa hizi mbili?
Name
Sagini Jumanne Abdallah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shangazi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Shangazi, moja, kwa kujenga mahusiano mema na Serikali za Vijiji hata wakapata majengo ya kuazima. Pia, nikiri kwamba majengo yale hayakidhi haja ya vituo vya kisasa vya Polisi. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa vile yeye analo fungu kidogo kwenye Mfuko wa Jimbo, nimshauri aweze kutenga kidogo kwa sababu, tumesema vituo vilivyoko kwenye maeneo ya kijamii kadiri wanajamii wanavyoanza kutoa na Serikali inawaunga mkono kumalizia. Kwa hiyo, akianza tu anipe taarifa na sisi Wizarani tutajipanga ili Jeshi la Polisi liweze kuongezea, vituo hivi vya Mlalo na Mtae viweze kukamilika, nashukuru.
Name
Salma Rashid Kikwete
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mchinga
Primary Question
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kilindi?
Supplementary Question 3
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba niulize swali la nyongeza kwa niaba ya Jimbo la Mchinga. Kituo cha Polisi cha Mchinga kina ukubwa wa kilometa 30 kwa 40 na bahati nzuri kiwanja kimepimwa, lakini kinakabiliwa na changamoto kadhaa nyingi tu. Changamoto ya kwanza ni uchakavu wa jengo, ikiwa na maana kwamba, paa linavuja kabisa, ukosefu wa usafiri na nyumba za watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, nini kauli ya Serikali juu ya kuboresha Kituo hiki cha Jimbo la Mchinga? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Sagini Jumanne Abdallah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba vipo Vituo vya Polisi vina hali mbaya sana. Kwa kuwa tulishatoa ahadi hapa ya kutembelea Jimbo lile na Wilaya ya Lindi kwa ujumla ili kuangalia uchakavu wa vituo vya Magereza, niahidi kwamba baada ya Bunge hili, nitatimiza ahadi hiyo ya kutembelea Lindi, Mchinga kwa madhumuni ya kuona kiwango cha uchakavu na hatimaye Mkuu wa Jeshi la Polisi aelekezwe kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kama atapata nafasi niko tayari kuongozana naye, ahsante.
Name
Selemani Moshi Kakoso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Vijijini
Primary Question
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kilindi?
Supplementary Question 4
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi. Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa Wilaya ambazo hazina Kituo cha Polisi, wanatumia Kituo cha Polisi kwenye jengo la Ofisi ya Kata. Halmashauri ya Wilaya la Tanganyika kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wameomba wadau kuchangia, nami nikiwa miongoni mwa wadau kujenga Kituo cha Polisi. Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi ambao wamejitolea ili waweze kukamilisha hicho Kituo cha Polisi ambacho kipo katika hatua ya awali ya msingi?
Name
Sagini Jumanne Abdallah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja tumpongeze kwa kazi nzuri aliyofanya kama mmoja wa wadau na wadau wengine walioanza ujenzi wa Kituo hiki cha Polisi pale Tanganyika. Kwa niaba ya Waziri wangu, niahidi tu kwamba, tunamwelekeza IGP kupitia Makamanda wake waweze kufanya tathmini ya kiwango kilichofikiwa na kiasi gani kinatakiwa kama pungufu ili waweze kuingiza kituo hiki cha Tanganyika kwenye mpango wao wa ujenzi, nashukuru.
Name
Emmanuel Adamson Mwakasaka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Primary Question
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kilindi?
Supplementary Question 5
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Katika kata 29 zilizopo katika Jimbo la Tabora Mjini kuna upungufu mkubwa kwenye vituo vya Polisi vilivyoko kata za nje. Kata ya Kazima haina kabisa Kituo cha Polisi na uhalifu mwingi unafanyika maeneo yale katika Jimbo la Tabora Mjini: Ni lini Serikali itaweza kuweka mkakati wa kujenga Kituo cha Polisi katika kata hiyo? (Makofi)
Name
Sagini Jumanne Abdallah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge Mwakasaka kwa dhamira yake ya kujenga vituo vya Polisi kwenye maeneo ya Tabora. Unajua Tabora wakati fulani ilikuwa na wimbi kubwa sana la uhalifu, hapo katikati wakapoa sana, tukaamini pamekuwa eneo lenye utulivu. Sasa kama wameanza matukioya uhalifu, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tabora, waangalie maeneo yanayoweza kuwekwa vituo vya kimkakati kama Kazima, basi wayaingize kwenye mpango wao ili Serikali Kuu kupitia Jeshi la Polisi iweze kuwasaidia kukamilisha vituo hivyo. Wakifanya hivyo, tutawaunga mkono, nashukuru sana.