Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwantumu Mzamili Zodo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha Wakulima wa zao la Mwani ili kuongeza tija?

Supplementary Question 1

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Tunaishukuru sana Serikali kwa kutenga hizi fedha milioni 400 kwa ajili ya wakulima wa mwani, lakini fedha hizi bado ni chache, hazitoshi. Wanawake wa pembezoni mwa ukanda huu wa bahari wamehamasika sana kulima mwani;

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wanakwenda kuwaongezea fedha ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mwani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili, pamoja na akina mama kuhamasika kulima mwani bado kuna changamoto kubwa ya soko;

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuunganisha wakulima wa mwani pamoja na masoko? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwantumu Zodo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ni kweli, na ndiyo maana katika jibu la msingi nimesema hii ni ya awamu ya kwanza; lakini awamu ya pili ambayo tayari maandalizi yake yamekwisha kukamilika ni jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 2.5 zitaongezwa. Na kwa hili tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kwenye program hii iongezwe fedha ambayo itakawenda kuongezeka kwa vikundi kadhaa vya kina mama watakao nufaika na mkopo huu usio na riba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni changamoto ya soko. Upande wa soko unakwenda sambamba na upande wa uzalishaji. Kwa hatua tunayoiendea ya kuongeza uzalishaji imevutia wanunuzi wakubwa wengi. Hivi ninavyozungumza, ushindani juu ya ununuzi wa zao la mwani umeanza. Kampuni zimekwishafikisha bei ya mwani aina ya spinosum shilingi 900 na kwa upande wa aina ya cottonii ni shilingi 200. Kwa hiyo tunakwenda vizuri. Kwa upande wa Serikali tumejipanga kujenga maghala lakini pia vile vile kutengeneza mashine kwa ajili ya ukaushaji wa mwani, ahsante.

Name

Juma Usonge Hamad

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chaani

Primary Question

MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha Wakulima wa zao la Mwani ili kuongeza tija?

Supplementary Question 2

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana namimi kunipatia fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Tumekuwa tukishauri sana hususan sisi Wabunge ambao tunatokea mwambao wa Pwani kuhusiana na bei ndogo ya mwani.

Je, Serikali haioni haja sasa kufungamanisha mfumo huu wa ununuzi wa mwani na mfumo wa stakabadhi ghalani ili kupunguza utitiri wa wanunuzi ambao wamejipangia bei ndogo na kumuumiza mkulima wa mwani?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu la msingi nimeeleza, mkakati wetu ni pamoja na kujenga maghala. Hili la kujenga maghala ni kuelekea katika kile alichokishauri Mheshimiwa Mbunge, ya kwamba tunaweza pale mbele kwenda katika mfumo wa kuliingiza zao la mwani katika stakabadhi ghalani. Tukijenga maghala na tukaongeza uzalishaji tutafanikiwa kufika katika hatua ile aliyoishauri Mheshimiwa Juma.

Name

Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Primary Question

MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha Wakulima wa zao la Mwani ili kuongeza tija?

Supplementary Question 3

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Bagamoyo Kata ya Zinga, Kijiji cha Mlingotini, kuna wakulima mahiri kabisa wa mwani.

Je, ni lini Serikali itawapatia vifaa hususan boti ili waweze kufika katika maeneo ya uzalishaji kwa urahisi zaidi?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Muharami Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna chama kikubwa na cha mfano cha ukulima na uchakataji wa mazao yatokanayo na mwani, kinaitwa Chama cha Ushirika cha Msichoke kilichopo Mlingotini – Bagamoyo kimeomba jumla ya fedha shilingi milioni 40. Chama hiki kitapata fedha hizi hapa karibuni kwa lengo la kununua boti itakayowawezesha kina mama wale kuingia baharini kwenda kuchukua mazao yale na vile vile kamba na taitai na zana zingine. Hongera sana Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Bagamoyo, ahsante sana.

Name

Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Primary Question

MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha Wakulima wa zao la Mwani ili kuongeza tija?

Supplementary Question 4

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wizara ya Mifugo imekuwa ikitoa ahadi kwa wananchi wa Ushetu kwa ajili ya kuwajengea majosho. Hata Mheshimiwa Mpina wakati akiwa Waziri alishafika Kaya za Nyankende, Ulewe na Ubagwe akaahidi lakini utekelezaji wake mpaka sasa hivi hakuna. Nataka nipate kauli ya Serikali.

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Serikali imefanikiwa kupeleka jumla ya fedha shilingi milioni 540 kwa ajili ya ujenzi wa majosho katika halmashauri mbalimbali nchini, na bado kiasi cha shilingi takribani milioni 100 zipelekwe pia. Ninaamini Wilaya ya Ushetu ni miongoni mwa Wilaya ambazo ni wanufaika. Naomba mara baada ya hatua hii ya Bunge nikutane na Mheshimiwa Mbunge Cherehani aweze kunipatia orodha ya vile vijiji vyake ili niweze ku-cross check kwa ajili ya ufuatiliaji wa ujenzi wa majosho haya ya wananchi wa Ushetu.

Name

Asya Mwadini Mohammed

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha Wakulima wa zao la Mwani ili kuongeza tija?

Supplementary Question 5

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa mwani unatambulika duniani kwamba ni zao kubwa ambalo linawasaidia akina mama kulima lakini linaweza kutupa bidhaa kama vipodozi, vyakula na vitu vingine.

Je, Serikali haioni sasa kuanzisha kiwanda ama viwanda nchini vya kuchakata mwani ili tuweze kuzalisha bidhaa hizi ndani ya taifa letu?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asya Mwadini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mwani hutumika kwa ajili ya kutengeneza kimiminika kizito ambacho hutengenezea vipodozi, na pia vile vile hutumika kama sehemu ya kutengenezea vyakula hususan kama ice cream na vinginevyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tunao mpango wa kukutana na wazalishaji wa ndani ya nchi wanaotumia malighafi hii kwa lengo la kuwahamasisha kuingia katika utaratibu ambao utapelekea wakulima wetu waweze kuchakata na kuwauzia wao wanaotumia ndani ya nchi kama vile kampuni za utengenezaji wa vipodozi na kampuni za utengenezaji wa vyakula. Ndiyo maana katika mkakati wetu tumeweka mashine za ukaushaji na hatimaye kutengeneza mpaka katika kufikia hatua ya kuwa kimiminika kizito kitakachokwenda kutengeneza colgates na vipodozi kama vile lotions lakini vile vile kwa ajili ya kutengenezea ice creams.