Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza: - Je, Serikali inawasaidiaje wajane ili kuondoa mila na desturi potofu zinazomkandamiza Mwanamke kwenye suala la mirathi?

Supplementary Question 1

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa maswali madogo mawili ya nyongeza.

Je, Serikali inampango gani kuajiri wanasheria ambao wanaweza kusaidia kuleta elimu ya mirathi katika ngazi ya kata?

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana na inatia huzuni wanawake wajane baadhi yao wamejikunja hawajui hatima yao kwasababu wanadhurumiwa haki zao za mirathi, hivyohivyo wanakuwa wanateseka kwa namna hata ya kusomesha Watoto wao;

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaleta sheria ambayo itasaidia kuleta mpango mkakati kwa ajili ya kunusuru ndoa na mirathi ili kuepusha changamoto za mirathi? Ahsante. (Makofi)

Name

Geophrey Mizengo Pinda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Answer

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kuajiri wanasheria katika ngazi ya kata, kimsingi kule tuna Mahakama ambapo shughuli zote za kimahakama zinafanywa katika maeneo yale, na wale mahakimu ni watalamu ambao wamehakikiwa. Tunakwenda kubadili Sheria ile ya Wazee wa Baraza na badaye kuruhusu wanasheria binafsi vilevile kwenda kusimama kwenye mahakama hizo ili kuwasaidia wananchi wengi ambao wangehitaji msaada wa kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo suala la ule mkandamizaji napenda nitumie nafasi hii kuanza kuwafahamisha wananchi wote; kumekuwa na mkanganyiko tu wa akili za wananchi wachache wenye tamaa, unapopewa nafasi ya kuwa msimamizi wa mirathi huko ndiko kunako anzia tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msimamizi wa mirathi si mrithi. Msimamizi wa mirathi kazi uliyopewa ni kukusanya mali za marehemu na kusimamia warithi kupata kwa kuzingatia haki zao na mrithi namba moja kwenye haki za mirathi ni mke wa marehemu, watoto wa marehemu ndilo kundi la pili na kundi la mwisho ni wazazi wa marehemu, kama wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kinachotokea sasahivi ni kwamba mtu akipewa tu nafasi ya kusimamia mirathi, anaanza kujirithisha yeye mwenyewe. Huyu ni mwizi na anastahili kushtakiwa kama mwizi wa kuaminiwa. Hili ndiyo jambo ambalo kimsingi linakera sana kwenye jamii zetu. Akina mama wengi wananyanyasika katika mazingira kwamba shemeji aliye aminiwa na ile familia kusimamia na kukusanya mali za marehemu yeye mwenyewe ndiye anabaki katika mazingira ya kurithi na kuila ile mali ya wale walengwa ambao kimsingi wanakuwa ni familia ile ya marehemu iliyoachwa baada ya kifo cha wazazi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili ni jambo tu la uelewa, hakuna mtu mwingine yeyote mwenye haki ya kurithi mali iliyoachwa na marehemu nje ya hao niliowataja. Kuna mila nyingine ni potofu sana; kwa mfano kuna mila ambazo zinamfanya mtu anaitwa mrithi awe na sauti asilimia mia kwenye mali zile. Ile si urithi wa kisheria. Urithi wa kisheria unaotambuliwa ni mke, watoto na mzazi wa marehemu; na katika mgao mzazi wa marehemu anapata kiasi kidogo sana kuliko watoto na mke wa marehemu kwasababu mke wa marehemu anakuwa bado anaendelea kuilea ile familia ambayo imeachwa na yule marehemu, ahsante.