Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abdallah Dadi Chikota
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya ulinzi kutoka Mtwara – Newala – Masasi hadi Songea kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 1
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili.
Swali la kwanza, kutokana na changamoto za kiulinzi zilizopo kwa jirani zetu Msumbiji kuna matumizi makubwa sana ya barabara hii hasa sehemu ya Mahurunga, Kitaya, Mnongodi hadi Mchenjele.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutafuta fedha za dharura na kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami Kilomita 70, wakati tunasubiri fedha nyingi za ujenzi wa Kilomita 358?
Swali langu la pili ni barabara sambamba ni hii ni barabara ya Mnivata Newala hadi Masasi tumeshaambiwa kwamba Serikali imeshapata fedha za ujenzi wa barabara hii.
Je, Serikali inawaambiaje wananchi wa maeneo haya, ujenzi huu utaanza lini? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tunajua barabara hii ni muhimu hasa kutokana na changamoto za kiulinzi katika Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Ruvuma, Serikali mpango wake wa kwanza ni kuifungua yote ili iweze kupitika kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, tukishaweza kwamba inaweza ikapitika na kujenga madaraja yote, Serikali sasa tunaona kutakuwa na haja ya kuijenga kwa kiwango cha lami kwani barabara hii siyo tu kwamba inaishia Masasi pia inakwenda Mkoa wa Ruvuma ambako pia kuna Kilomita 535. Kwa hiyo ni barabara ambayo tunaomba tuifungue kwanza halafu tuanze kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa lami.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu barabara ya kuanzia Mwinivata, Newala hadi Masasi yenye urefu wa Kilomita 160. Benki ya Maendeleo ya Afrika ilishakubali kuifadhili hiyo barabara na tunapoongea sasa hivi tunachasubiri ni no objection ya hiyo benki, baada ya hapo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge manunuzi yanachukuwa siku 90 ndiyo barabara hiyo itaanza.
Mheshimiwa Spika, hivyo baada ya kupata no objection kutakuwa na mchakato wa manunuzi ambao ni wa kisheria siku zisizopungua 90 na baada ya hapo tutaanza kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, kwa maana ya kuitangaza na kupata Mkandarasi. Ahsante.(Makofi)
Name
Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya ulinzi kutoka Mtwara – Newala – Masasi hadi Songea kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 2
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa hii fursa.
Mheshimiwa Spika, nataka kujua ni lini Serikali itajenga barabara ya kimkakati kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Kilomita 176 inayotoka Kitahi, kupita Amani - Makolo, Paradiso, Rwanda, Lituhi, Mbaha, Lundo, mpaka Mbamba Bay kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, ahsante.(Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jacqueline Msongozi Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ambayo inaanza Kitahi, kupitia Amani – Makolo, Rwanda hadi Lituhi ipo kwenye utangazaji kwa ajili ya kuijenga barabara yote. Kuanzia Kitahi kwenda Mbamba Bay usanifu umeshakamilika na Serikali inatafuta fedha kuijenga barabara hiyo ambayo pia ni sehemu ya barabara ya ulinzi hadi Mtwara. Ahsante.(Makofi)
Name
Maimuna Salum Mtanda
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Newala Vijijini
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya ulinzi kutoka Mtwara – Newala – Masasi hadi Songea kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 3
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nina swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANROADS ilikuwa na utaratibu wa kujenga kwa kiwango cha lami maeneo ya vilima korofi ili kurahisisha mawasiliano ya barabara hizo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kwa kiwango cha lami eneo korofi la kilima cha Miyuyu - Ndanda ili kurahisisha mawasiliano ya usafiri kwa wananchi wa Newala wanaoenda kutibiwa. (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tulishawaagiza Mameneja wote wa TANROADS na kazi hiyo imeshafanyika kuainisha maeneo yote korofi ikiwemo na maeneo haya ya vilima ambavyo viko katika Wilaya ya Newala. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vilima hivyo vitajengwa kwa kiwango cha lami ili isiwe tatizo la wananchi kupata mawasiliano kipindi cha mvua. Ahsante.
Name
Kabula Enock Shitobela
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya ulinzi kutoka Mtwara – Newala – Masasi hadi Songea kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 4
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara inayounganisha Hungumalwa - Ngudu Wilaya ya Magu, imekuwa ikiwekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi 2005, 2010, 2015 mpaka 2020 kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, sasa ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabula, Mbunge wa Viti Maalum Mwanza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ya Hungumalwa kwenda Ngudu ipo kwenye mpango na ipo kwenye bajeti kwa ajili ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami kama ambavyo Serikali imeahidi kuifanya. Ahsante. (Makofi)
Name
Katani Ahmadi Katani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tandahimba
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya ulinzi kutoka Mtwara – Newala – Masasi hadi Songea kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 5
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, kutoka Mpwiti, Mkonjoano kuelekea Tandahimba ni barabara ambayo upembuzi yakinifu imeshafanywa zaidi ya miaka minne.
Je, ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Katani Katani Mbunge wa Tandahimba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaji ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa usanifu ulishakamilika Serikali inajipanga kutafuta fedha ili iweze kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, azma Serikali ni kuijenga na tuna uhakika itajengwa fedha itakapopatikana. Ahsante.
Name
Simon Songe Lusengekile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya ulinzi kutoka Mtwara – Newala – Masasi hadi Songea kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 6
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Nyashimo Wilayani Busega kuelekea Dutwa Wilayani Bariadi imekuwa ikiahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami yenye takribani kilometa 47 kupitia Malili, Dutwa na pale Shigara.
Leo nataka commitment ya Serikali Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara hii ya kutoka Nyashimo kwenda Dutwa sasa hivi inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na itakapokuwa imekamilika barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
Name
Daniel Baran Sillo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Babati Vijijini
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya ulinzi kutoka Mtwara – Newala – Masasi hadi Songea kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 7
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, ninataka kujua, Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mizani katika Wilaya ya Babati - Kondoa hadi Dodoma.
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Sillo Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara hii amekuwa akiifuatilia sana Mheshimiwa Mbunge, nataka nimhakikishie kwamba kama tunavyomwelekeza na kumweleza kwamba Serikali ina mpango wa kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami kulingana na patikanaji wa fedha. Ahsante.
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya ulinzi kutoka Mtwara – Newala – Masasi hadi Songea kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 8
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, katika Ujenzi wa barabara za TANROAD huwa kunakuwa na package ya taa za barabarani kwenye barabara ambazo zimeanza kujengwa kuanzia mwaka 2019. Barabara kutoka Njombe kuelekea Makete ni barabara ambayo ilikuwa ni package ya nyuma.
Je, ni lini Serikali itaingiza package ya taa ya barabarani kwenye Mji wa Handara na Makete Mjini, angalau na sisi Makete tuanze kuona taa za barabarani kama maeneo mengine. (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Sanga Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara hiyo aliyoitaja ndiyo kwanza inakamilishwa kwa kiwango cha lami na Meneja wa Mkoa wa Njombe ameshatoa tathmini ya barabara, kwa maana ya gharama ambapo tutaweka taa za barabarani Mji wa Ramadhani, Ikonda na Makete yenyewe. Ahsante.