Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaugawa Mkoa wa Tanga ili kuongeza ufanisi katika eneo la Utawala Bora?
Supplementary Question 1
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali ambayo sisi kule mkoani katika hatua ya RCC tulikaa, sasa sijui yalikwamia wapi? Nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza: Kwa kuwa mchakato huu huwa unaandaliwa na wataalamu na ambao wako chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Je, kama alivyoeleza kwamba hawajapokea wasilisho, hawaoni tu kwamba Mkoa wa Tanga ndiyo mkoa pekee nchini ambao una wilaya nane na una Majimbo ya Uchaguzi 12 na Halmashauri 11? Sasa ni lini Serikali yenyewe tu itaweza kufanya maamuzi ya kuugawa mkoa huu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tunaposema utawala bora ni pamoja na upelekaji wa huduma kwa wananchi. Sasa wataalamu hawa katika ngazi za elimu na afya wanapata taabu kubwa sana kwa sababu wanatumikia eneo kubwa la kiutawala: Ni lini sasa Serikali itatenda kama inavyosema kuhusu eneo zima la utawala bora?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi Mbunge wa Jimbo la Mlalo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tunafahamu Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa yenye Halmashauri nyingi na ni mkoa mkubwa na maana yake kunakuwa na changamoto za aina yake katika uendeshaji. Ila kwa mujibu wa sheria, uanzishaji ni lazima uanzie ngazi ya mkoa wenyewe kama ambavyo sheria hii inaelekeza. Kwa hiyo, pamoja na kwamba Serikali kwa maana ya Serikali Kuu inaona, lakini wajibu wa Halmashauri, mkoa wenyewe, na vijiji utekelezwe ili tuweze kuanzisha mkoa huu kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, pili, kuhusiana na changamoto ya ukubwa wa mkoa ambao unapelekea wataalamu wa afya na elimu kushindwa kutekeleza majukumu yao ya utawala bora, tunaendelea kuwezesha kwa kadri ya ukubwa wa mkoa kwa maana ya miundombinu, usafiri na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, jambo la msingi ni kuleta hoja hiyo ili Serikali iweze kuchukua maamuzi stahiki. Ahsante.
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaugawa Mkoa wa Tanga ili kuongeza ufanisi katika eneo la Utawala Bora?
Supplementary Question 2
MHE. DUNSTAN KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; naomba niulize swali moja la nyongeza. Ugawaji wa Mkoa wa Tanga ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alipokuja kwenye Mkoa wa Tanga, na hii ilikuwa ni baada ya Wabunge wa Mkoa wa Tanga kumuomba kwamba jambo hili tumeshalijadili kwenye RCC.
Je, hata baada ya ahadi ya Mheshimiwa Rais bado tunatakiwa jambo hili tena kulijadili kwenye mkoa kwa mara nyingine?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dunstan Kitandula kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kadri ya majibu yangu ya jibu la msingi, kwamba kuna taratibu ambazo zipo kwa mujibu wa sheria, na Mheshimiwa Rais alitoa ahadi hiyo, na sisi ahadi hiyo na sisi ahadi za viongozi wetu, Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Makamu Rais, Waziri ni maelekezo ni maelekezo tutafanya kazi hiyo. Hata hivyo niwaombe tufuate utaratibu ule kwa kadri sheria ilivyo.
Name
Priscus Jacob Tarimo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaugawa Mkoa wa Tanga ili kuongeza ufanisi katika eneo la Utawala Bora?
Supplementary Question 3
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Waziri ni lini Serikali itakamilisha mpango wa kupanua Mji wa Moshi na hatimaye kuwa Jiji kama ilivyokuwa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe 15 Julai, 2016?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Priscus Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, narejea kwenye jibu langu la msingi, kwamba Halmashauri ya Moshi, inahitaji kuleta mapendekezo kwa mujibu wa taratibu zilizoelekezwa na sheria na sisi ofisi ya Rais TAMISEMI, tutafanya tathmini na baadaye kuwasilisha kwa mamlaka husika kwa ajili ya maamuzi husika.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved