Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: - Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa mradi wa kuzuia mafuriko katika Mto Msimbazi?

Supplementary Question 1

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Mradi huu umechukua muda mrefu kutekelezwa na majibu ya Serikali muda wote yamekuwa ni haya; na kipindi kutoka sasa hadi Julai, ambapo Mheshimiwa Waziri amesema mradi huu utakuwa umetekelezwa ni takribani miezi mitatu tu. Sasa swali langu, Mheshimiwa Waziri analihakikishia Bunge hili Tukufu kwamba kufikia kipindi hicho, taratibu zote ikiwa ni pamoja na kulipa fidia wananchi watakaoguswa na mradi zitakuwa zimekamilika?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Bonde la Mto Msimbazi ni chanzo kikuu cha mafuriko katika barabara iendayo Kariakoo eneo la Jangwani. Barabara hii inaelekea katika kitovu cha uchumi wa nchi. Sasa, swali langu kwa Serikali;

Je, ni mkakati gani wa dharura umeandaliwa kwa kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kwa kasi katika Jiji la Dar es Salaam?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, wa Viti Maalum, Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunapotaka kufanya jambo lolote, hasa jambo ambalo limezunguka kwenye maeneo ya makazi ya watu si kwamba tu tunaangalia kwenye fidia lakini kuna baadhi ya mambo ya msingi huwa tunaangalia. Kwanza katika mazingira kuna kitu kinaitwa EIA, Environment Impact Assessment; kwa hiyo kwanza tunaziangalia athari za kimazingira. Je, tutakapofanya hilo jambo tunaweza tukawaathiri vipi wananchi kwenye hilo. Lakini pia kuna kitu tunakiita PA property assessment, kwamba je, mali za wananchi wanavipando vyao, wana nyumba zao wana makazi mengine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa ufupi ni kwamba hili jambo tumeshalikali kitako na tayari tathmini inaendelea ni mtoe hofu Mheshimiwa, tunalithibitishia Bunge hili pamoja na hizo tathmini ambazo ambazo zinaendelea lakini bado tunaendelea na kama tulivyoeleza kwamba miezi michache inayofuata ujenzi huu unaanza.

Mheshimiwa Spika, lakini je, tunajuhudi au jitihada gani katika kuzuia mafuriko; nimwambie tu kwamba tumeshakaa pamoja, sisi Ofisi ya Makamu wa Rais, pamoja na maafisa wetu wa mazingira tumekaa na halmashauri tumekaa watu wa TARURA, tumekaa na watu wengine ili kuona namna ambavyo tunaweza tukapunguza angalau hizo athari za mafuriko, zikiwepo za kutengeneza vi-streams vidogovidogo vitakavyoyaondosha maji pale na kuyapeleka maeneo ya bahari ili pale yasituwame na yakapunguza athari kwa wananchi. Nakushukuru.

Name

Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: - Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa mradi wa kuzuia mafuriko katika Mto Msimbazi?

Supplementary Question 2

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mahiri kabisa kwamba ninaamini kabisa kwamba anafahamu changamoto hizi zilivyo. Kwa kuwa mradi huu wa Bonde la Mto Msimbazi ni hoja kuu ya Jimbo la Kinondoni, na kwa kuwa sasa Serikali inakwenda kuanza mradi huu Julai, 2022. Je, Serikali iko tayari sasa kutoa mpango wa utekelezaji, kwa maana ya program and planning of action, ili wananchi wale wa mto Msimbazi waweze wakajua ni lini wanatakiwa wanaondoke na ni lini kabisa watatakiwa waweze kupata fidia zao pale itakapobidi?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Abbas, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Abbas kwa kuwa Jimbo lake na yeye ni moja ya miongoni mwa Majimbo yaliyopita katika Mto Msimbazi lakini anafanya kazi kubwa ya kutusaidia kama Serikali kwa kuwaelewesha wananchi. Namwambia Mheshimiwa Tarimba Abbas kwamba aende akawaambie wananchi kwamba tathmini inaendelea. Imeshaanza kama miezi mitatu iliyopita na kwa kuwa inaendelea matokeo lazima wananchi tutawaambia. Kwa hiy,o naomba akawaambie wananchi wa Kata za Kinondoni, Kata za Mzimuni, Kata ya Magomeni, Kata ya Kigogo na maeneo mengine yaliyopita mto huu kwamba tathmini itakapotoka majibu watapewa na lazima tuwaambie kabla ili tusije tukawavamia tukaja tukatengeneza mivutano baina ya wananchi na Serikali. Nakushukuru.(Makofi)

Name

Simai Hassan Sadiki

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nungwi

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: - Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa mradi wa kuzuia mafuriko katika Mto Msimbazi?

Supplementary Question 3

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kuweza kunipa nafasi hii kuuliza swali dogo la nyongeza.

Je, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina mpango gani wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya kuandaa mradi utakaoenda kuzuia maji ya bahari kuendelea kumeza kingo kule maeneo ya Nungwi? (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simai, Mbunge na mtumishi wa wananchi wa Jimbo la Nungwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inayompango ama ilishakuwa na huo mpango na ndiyo maana tayari kuna baadhi ya kingo kwa upande wa Zanzibar ambazo tayari zimeshajengwa na hii ni kutokana na athari kubwa ya kimazingira ambayo ilifika wakati maji ya bahari yanaingia kwenye vipando vya wananchi ikiwemo mihogo, migomba ambayo haihimili maji ya chumvi. Pia maji haya yalikuwa yanaingia kwenye maeneo ya makazi. Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakaona kuna haja ya kushirikiana katika suala hili. Tayari yako baadhi ya maeneo kwa mfano Kisiwa cha Pemba maeneo ya Wete, Micheweni na maeneo ya Unguja pia tumeanza. Namwambia Mheshimiwa kwamba katika bajeti ambayo tumeisoma juzi tutajitahidi tutenge fungu kwa ajili ya kulipa kipaumbele Jimbo lako kwa ajili ya kujenga hizo kuta. Nakushukuru.

Name

Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: - Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa mradi wa kuzuia mafuriko katika Mto Msimbazi?

Supplementary Question 4

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, Wananchi wa Jimbo la Ubungo wameathirika sana na mafuriko ya mito Gide, Mto China na Mto Ng’ombe, ninavyoongea Mtaa wa Kibangu leo nyumba za wananchi 12 zimebomolewa na mto huo. Nauliza kwa nini Serikali isichukue hatua za dharula za kujenga gambiozi katika mito hiyo ili kuokoa maisha ya wananchi wakati tunasubiri mradi huo? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Profesa Kitila kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imefika wakati na imeona athari ambazo zinajitokeza hasa zinazosababishwa na mito hii mikubwa na hasa kipindi cha mvua kubwa kama hiki ambacho tukonacho. Namwambia Mheshimiwa Profesa kwamba wazo na fikra alilolitoa ni jambo ambalo tayari tumeshakaa na tumeshalifikiria, lakini kwa heshima ya wazo lake tunalichukua na tunazidi kwenda kulifanyia kazi. Nakushukuru.

Name

Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: - Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa mradi wa kuzuia mafuriko katika Mto Msimbazi?

Supplementary Question 5

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa ndani ya Jimbo la Kibamba kuna Mto Mbezi na Mto Mpiji ambao kwa muda mrefu wananchi wamedhurika sana na mafuriko, nyumba zao lakini pia na taasisi kama shule zimekuwa zikiondoka.

Je, Serikali ina mkakati gani sasa kukabiliana na hali hiyo katika mito hiyo miwili Mto Mbezi na Mto Mpiji?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunayo mikakati mingi kwa sababu tunafahamu athari za kimazingira zinazosababishwa na mito hii ni athari kubwa. Mwisho wa siku zinaharibu vipando, zinaharibu makazi lakini pia zinaweza kuleta hata maradhi kwa sababu maji yakija yanakuja na takataka, yakirudi yanarudi maji peke yake takataka zinabakia kwa hiyo tunajua hata maradhi yanatokea. Kwa hiyo iko mikakati mingi kama Serikali ambayo tumeamua kuifanya, ikiwemo kwanza kuhakikisha kwamba tunajenga hizo kingo lakini pia tunasaidia katika kuwaelimisha wananchi namna ambavyo wanaweza wakapunguza hizo athari na wakaepukana na hizo athari zinazosababishwa na mito hii. Nakushukuru. (Makofi)