Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Justin Lazaro Nyamoga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mgambalenga Wilayani Kilolo?
Supplementary Question 1
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ninayo maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza katika skimu hizi ikiwemo hii ya Mgambalenga lakini pia skimu za Ruaha Mbuyuni na nyingine gharama za ulipiaji wa vibali katika bonde zilipanda kutoka Shilingi 70,000 hadi Shilingi 150,000 zaidi ya asilimia 100. Sasa ningependa kujua ni mpango gani wa Serikali wa kupunguza hizi gharama maana gharama za kilimo zimeongezeka kwa hiyo inakuwa ni vigumu wakulima wale wa kujikimu kuweza kumudu kulipia vibali kwa ajili ya umwagiliaji? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili katika Kata ya Nyanzwa skimu ya umwagiliaji iliyoko pale ambayo ni ahadi ya Mawaziri Wakuu kadhaa bado haijatekelezwa, pamoja na juhudi kubwa za kuifatilia zilizofanywa na mimi mwenyewe hata Diwani wa kule amekuja kufuatilia. Sasa ningependa kujua kwa sababu ndiyo uhai wa watu wa kule kwenye kilimo cha vitunguu.
Je, ni lini Serikali itajenga ile skimu kwa kuzingatia pia mwaka huu hali ya umwagiliaji imekuwa ngumu na hali ni mbaya, ni lini Serikali itafanya ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Nyanzwa? Ahsante. (Makofi)
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza kuhusu gharama ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge gharama zimekuwa juu tofauti na ile gharama ya awali ambayo ilikuwepo. Tumeielekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kukutana na mamlaka ya bonde husika kukaa na kuangalia uhalali wa gharama hizo ili tumpunguzie adha mkulima.
Mheshimiwa Spika, pili ni kuhusu mradi wa Nyanzwa ni kweli mradi huu Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiufuatilia sana na ninampongeza sana kwa hili. Tayari pale tuna miundombinu ya hekta 300 na tunachangamoto kubwa ya uhaba wa maji ya umwagiliaji, katika bajeti ya mwaka 2022/ 2023 Tume itafanya usanifu wa kina wa bwawa kuvuna maji ya mvua na usanifu huo pia utahusisha eneo la hekta 9,000 ili kuwahudumia wakulima wengi zaidi na baadae tutajenga kama ambavyo usanifu utakuwa umeelekeza.
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)
Name
Fatma Hassan Toufiq
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mgambalenga Wilayani Kilolo?
Supplementary Question 2
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, skimu ya umwagiliaji iliyopo katika eneo la Chikopelo Wilaya ya Bahi imeacha kufanya kazi kwa muda mrefu baada ya mwekezaji kuondoka. Nini kauli ya Serikali katika kuifufua skimu hii ili kuwaondolea umaskini wananchi wa eneo hilo? (Makofi)
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Fatma Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tunafahamu ya kwamba moja kati ya eneo ambalo litasaidia sana kukuza kilimo chetu katika nchi yetu ya Tanzania ni kilimo cha umwagiliaji. Namuahidi Mheshimiwa Mbunge ya kwamba Wizara tumejipanga kuhakikisha tunazipitia skimu zote ili kuweza kufahamu status zake kwa maana tujue ni miradi ipi haifanyi kazi, ipi inafanya kazi lakini ipi imekwamishwa na nini, ili tuitatue na kuwafanya wakulima wetu walime kilimo cha umwagiliaji. Moja wapo ya maeneo ambayo tutayapitia ni pamoja na eneo la Chikopelo.
Name
Aloyce John Kamamba
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buyungu
Primary Question
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mgambalenga Wilayani Kilolo?
Supplementary Question 3
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Katika Wilaya ya Kakonko ambako Jimbo la Buyungu lipo zipo skimu za Katengera, Gwanumpu, Ruhwiti na Muhwazi ambazo miundombinu yake imeharibika na haifanyi kazi vizuri.
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu hiyo ili waweze kuendelea na kazi kama ilivyokusudiwa? (Makofi)
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika miradi aliyoisema Mheshimiwa Mbunge ukiacha mradi wa Ruiche hii miradi mingine miwili tutaiingiza katika mipango yetu kuhakikisha kwamba inafanya kazi katika utaratibu ambao nimeuanisha awali wa kuipitia nakuona changamoto ulizonazo.
Mheshimiwa Spika, mradi wa Ruiche tumeshapata no objection na hivi sasa tutaelekeza kazi ya usanifu ifanyike ili baadae tuanze kazi ya ujenzi.
Name
Lucy Thomas Mayenga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mgambalenga Wilayani Kilolo?
Supplementary Question 4
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika Kata ya Itilima, Wilaya ya Kishapu kuna Kijiji cha Mwamala na katika Kata ya Mwaduiluhumbo kuna kijiji cha Nyenze, katika Wilaya hii ipo miradi ya skimu za umwagiliaji ambayo Serikali ilitoa pesa lakini baada ya kutoa pesa zile hazikutosha, katika Jimbo hili la Kishapu wakinamama katika maeneo haya wanapata shida sana kutokana na hali halisi ya ukame katika maeneo haya.
Je, ni lini Serikali itatupatia pesa katika skimu hizi mbili za Nyenze pamoja na Mwamala ili wananchi waweze kufaidika? Kwa sababu skimu hizi za umwagiliaji endapo kama zikikamilika maji yatasaidia mifugo pamoja na binadamu. (Makofi)
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Mayenga, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji amekuwa akifanya ufuatiliaji mara kwa mara ofisini kwetu na ninamuahidi kwamba katika bajeti yetu ambayo tutaisoma mwezi ujao tutaainisha miradi ambayo itafikiwa na miradi hii pia tutaifikia. (Makofi)