Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Primary Question

MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: - Je Serikali ina mkakati gani wa kushughulikia soko la ndani la maziwa kwa kuhimiza na kuhamasisha unywaji wa maziwa shuleni kabla ya kutafuta masoko ya nje?

Supplementary Question 1

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Ni dhahiri kwamba ndani ya nchi hii nzima wameshahamasisha shule 39 tu, sasa unaweza ukajua nchi hii ina shule ngapi na sasa zimehamasisha shule 39 tu kunywa maziwa na watu waliohamasisha ni 90,000. Sasa swali langu la nyongeza ni hili.

Mheshimiwa Spika, kwakuwa Mikoa yote iliyotajwa bahati mbaya sana ni kama Mikoa mitatu, minne na Mikoa tunayo mingi tu na hasa Mkoa ninaotoka mimi Mkoa wa Geita haukutajwa.

Ni nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha maziwa mengi yanayopotea huko vijijini kwa sababu yamekosa hifadhi yanaweza kupata hifadhi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili nini mkakati wa Serikali kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuchakata maziwa ili tuwe na uelewa kwamba wafugaji ambao wanafuga sasa wana uwezo wa kufuga kwa tija zaidi? (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bryceson Tumaini Magessa Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mikakati yetu kama Wizara ni pamoja na kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa maana ya TAMISEMI ili kuweza kutanua wigo zaidi wa kuongeza idadi ya shule. Ni kweli kwamba shule hizi tulizozisema ni chache na kwa hiyo kwa kushirikiana na wenzetu tunayo imani ya kwamba tutaongeza idadi ya shule.

Mheshimiwa Spika, namna gani ya mkakati wa kuweza kuyakusanya maziwa ya vijijini, ukitazama katika bajeti yetu ya mwaka 2021/2022 tunayoimaliza, Serikali iliondoa kodi ya vikusanyio kwa maana ya cans zile za stainless steel ambazo zilikuwa zikiuzwa takribani Shilingi 260,000, hivi sasa zinauzwa Shilingi 219,000. Hii imerahisisha kuongeza idadi ya cans za kukusanyia maziwa.

Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine ni juu ya nini tulichonacho sasa kwa ajili ya kuongeza viwanda vidogo vya kutengeneza maziwa na kukusanyia maziwa kule vijijini. Katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023 katika vitu vikubwa tutakavyokwenda kuvifanya ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunatatua zile changamoto zinazowakabili wafugaji wetu na kupelekea kushindwa kusindika maziwa yao, ikiwa ni pamoja na kuondoa tozo zile ambazo ni kikwazo.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo naomba nimuahidi Mheshimiwa Magessa yeye na Wabunge wengine wakereketwa wa viwanda vidogo wakae tayari katika kutushauri na kuweza kufikia lengo hili.