Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Primary Question

MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kusaidia Halmashauri zinazozunguka Mbuga na Hifadhi kwa kutoa CSR kwenye mapato ya utalii?

Supplementary Question 1

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa nia ni kuleta unafuu kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo; na kwa kuwa halmashauri ndio zinazojua zaidi mahitaji ya watu wale, hatuoni kwamba ni muda sasa tuzipeleke fedha hizo kwenye halmashauri badala ya kutekeleza miradi kama inavyofanyika migodi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa katika Mkoa wa Kilimanjaro suala la uoteshaji miti ni hiari, lakini ukataji miti ni suala ambalo lazima upate kibali na miti hiyo wanatumia kwa ajili ya nishati ya moto. Je, Serikali haioni kutafuta namna nyingine ya kuwapatia nishati mbadala kupitia CSR?

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufatilia hizi CSR katika eneo lake analowakilisha. Katika swali lake ambalo ameuliza Serikali haioni haja kupeleka fedha katika halmashauri. Kwenye jibu langu la msingi nimesema kwamba halmashauri pia zinapata asilimia na pia wananchi wanapata asilimia. Lengo ni kufikisha hii miradi kwa jamii ambao ndio hasa walinzi wa haya maeneo ambayo tunayahifadhi.

Mheshimiwa Spika, jamii ikijisikia kwamba ni sehemu ya uhifadhi sisi kama Serikali tunafarijika kwamba wanaona uthamani wa eneo lile na ni rahisi sasa hata unapowaelezea uhifadhi namna yake ni nini na thamani ya uhifadhi ni nini. Kwa hiyo kupeleka kwenye jamii ni muhimu zaidi kuliko kwenye halmashauri.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwamba uoteshaji wa miti Serikali kupitia hifadhi ya TANAPA ilianzisha mradi wa majiko banifu katika eneo linalozunguka Mlima Kilimanjaro. Majiko haya yalikuwa ni fanisi na walienda kufundishwa kaya mbalimbali katika maeneo hayo na pia tumeingia kwenye mpango wa kuanzisha upandaji wa miti katika maeneo yanayozunguka hifadhi hiyo.

Mheshimiwa Spika, upandaji huu ulianza toka mwaka jana na sasa hivi ni endelevu. Hivyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu utatekelezwa ambapo wananchi wengi wanaozunguka maeneo hayo watapata miche ambayo itapandwa katika maeneo ya vijiji nje ya hifadhi ili irahisishe kupata nishati mbadala. Ahsante.

Name

Leah Jeremiah Komanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Meatu

Primary Question

MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kusaidia Halmashauri zinazozunguka Mbuga na Hifadhi kwa kutoa CSR kwenye mapato ya utalii?

Supplementary Question 2

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nusu ya Wilaya ya Meatu imepakana na Hifadhi ambazo ni Ngorongoro, Serengeti na Maswa Game Reserve. Je, ni lini Serikali itaendelea kunufaisha miradi katika Wilaya ya Meatu, miradi ile ilikuwa inatolewa na ujirani mwema kutokana na utalii unaofanywa katika Hifadhi ya Serengeti na Ngorongoro ikiwemo ujenzi wa mabweni?

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimwambie tu kabisa Mheshimiwa Mbunge kwamba, asiwe na wasiwasi na niendelee kumpongeza kwa sababu wananchi wanaozunguka yale mapori ya akiba tunatambua umuhimu wa namna ya kunufaika na CSR. Hata hivyo, kwenye eneo hili Mheshimiwa Leah amekuwa akileta maombi katika ofisi zetu, lakini tutambue tu kwamba katika kipindi cha miaka miwili hii iliyopita tulikuwa tuna changamoto ya UVIKO 19 ambapo hifadhi zetu ziliathirika sana. Hivyo Serikali ilichukua jukumu la kuzisaidia hizi hifadhi ili ziweze kujiendesha.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumeshaanza kuimarika vizuri, CSR zitarudi kama ilivyokuwa mwanzo na pengine zaidi hasa ukizingatia Royal Tour imeibua mambo mengi, ahsante sana. (Makofi)

Name

Ally Mohamed Kassinge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kusini

Primary Question

MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kusaidia Halmashauri zinazozunguka Mbuga na Hifadhi kwa kutoa CSR kwenye mapato ya utalii?

Supplementary Question 3

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA), imefanya maboresho makubwa Kilwa Kisiwani ambao ni mji wa kitalii na Kilwa Kisiwani imetangazwa kuwa ni sehemu ya urithi wa dunia, lakini makubaliano yalikuwa kwamba wananchi wa Kilwa Kisiwani wapate CSR kupitia kujengewa shule pamoja na zahanati, lakini mpaka sasa hawajajengewa shule wala zahanati.

Mheshimiwa Spika, swali langu, je, Waziri yuko tayari kufuatilia kuona kwamba shule na zahanati inajengwa Kilwa Kisiwani?

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuliona hili, lakini kama ambavyo nimeeleza mwanzo kwamba kabla ya UVIKO-19 tulikuwa tunatekeleza kupeleka haya maeneo CSR, lakini hii changamoto ya UVIKO-19 ndio iliyoturudisha nyuma lakini kwa sasa hivi tumeshaanza kuimarika vizuri. Hivyo nimwahidi Mheshimiwa Mbunge katika eneo lake nitaenda pia nitaenda kuongea na wananchi wa jimbo hilo ili kuwaambia umuhimu wa kupata CSR pia umuhimu wa utunzaji wa maeneo ya hifadhi. (Makofi)