Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Khatib Said Haji
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Konde
Primary Question
Kwa mujibu wa Ibara ya 45(1)(a) na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano Rais anayo mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa waliopo magerezani. Je, Rais anayo mamlaka kisheria ya kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchunguzi/upelelezi au mahakamani?
Supplementary Question 1
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nikueleze tu kuridhika kwangu na majibu ya Kaimu Waziri Mkuu, majibu yamekwenda shule na yana viwango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majibu hayo, kwamba Rais hana mamlaka ya Kikatiba kusamehe watuhumiwa ambao mashauri yao yako katika hatu za kiuchunguzi; katika uongozi wa Awamu ya Nne tulimshuhudia Rais Jakaya Kikwete akitoa msamaha kwa watuhumiwa wa EPA na kutaka walipe na hakuruhusu wapelekwe mahakamani. Je, kutokana na kitendo hicho Rais Kikwete alivunja Katiba ya nchi kwa kutumia madaraka yake vibaya?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa mujibu wa majibu yako ni dhahiri kwamba watuhumiwa wa EPA bado wanastahiki kupelekwa mahakamani kwa sababu msamaha walioupata haukuwa wa Kikatiba, je, Serikali inatoa kauli gani juu ya kuwafikisha watuhumiwa wale wa wizi wa EPA mahakamani ili kukabiliana na tuhuma zao? Ahsante sana.
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali linaloulizwa hapa, lililoletwa mbele ya WIzara yangu ni je, Rais ana mamlaka ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyetuhumiwa? Na jibu langu ni la Kikatiba, na ninalolisema ndivyo Katiba inavyosema, na mimi si mwanasheria tu lakini vilevile ni mwalimu wa sheria. Ninasema, chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 45 Mheshimiwa Rais madaraka yake yako katika kumsamehe mtu ambaye tayari amehukumiwa na amepewa adhabu, inaitwa constitutional…(Makofi)
Kwa hiyo, naomba basi nikueleweshe...
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba makofi yapungue kidogo ili nieleweshe vizuri. Huu msamaha hana Rais wa Jamhuri ya Muungano tu, hata Rais wa Zanzibar chini ya Ibara ya 59 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambapo Rais pale ambapo kuna makosa anaweza akasamehe. Sasa umenitolea mifano miwili, mitatu ambayo Rais aliyepita unasema aliwasamehe watuhumiwa. Mimi kwa taarifa nilizonazo Mheshimiwa Rais hakutumia kifungu cha 45 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Name
Joseph Roman Selasini
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Rombo
Primary Question
Kwa mujibu wa Ibara ya 45(1)(a) na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano Rais anayo mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa waliopo magerezani. Je, Rais anayo mamlaka kisheria ya kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchunguzi/upelelezi au mahakamani?
Supplementary Question 2
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba wingi wa wafungwa magerezani unakwenda sambamba na wingi wa mahabusu waliopo magerezani. Na mara nyingi ni kwamba baadhi ya mahabusu wanakamatwa kwa kupakaziwa makosa na askari wa Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, napenda kuiuliza Serikali, ni hatu zipi ambazo Serikali inazichukua za dhahiri, kukomesha kitendo hiki ambacho kinawatesa wananchi lakini kinaitia Serikali hasara kwa kuwashikilia watu ambao hawana hatia?
Name
Eng. Hamad Yussuf Masauni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nilikuwa nataka nijaribu kuweka kauli yake sawa ambayo ameizungumza kuhusiana na shutuma dhidi ya Jeshi la Polisi. Amezungumza kana kama kwamba Jeshi la Polisi lote kazi yake ni kubambikia watu kesi, ninachoweza kusema ni kwamba kuna matukio machache ya baadhi ya polisi ambao wamekuwa wakilichafua Jeshi la Polisi, lakini ni wachache mno, ambao Jeshi la Polisi limekuwa likiwachukulia hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, na wote ni mashahidi, juzi wakati wa bajeti kuna hoja ilizungumzwa kuhusiana na yule kijana ambaye alibambikiwa kesi pale gerezani. Ninachotaka kulithibitishia Bunge lako Tukufu mpaka sasa hivi ni kwamba askari waliohusika na jambo lile watatu wameshafukuzwa kazi na bado wanaendelea kuchukuliwa hatua za kijinai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo si kweli kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likizembea kwa kuwachukulia hatua askari wachache sana ambao wamekuwa wakifanya matendo haya ambayo yanakinzana kabisa na taratibu za sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kimsingi ni kwamba hayo ambayo ameyazungumza Mheshimiwa Selasini kuhusiana na tuhuma dhidi ya Jeshi la Polisi niliona niyaweke sawa kwa statement hiyo.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved