Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Primary Question

MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: - Je, hali ya upatikanaji wa vitabu vya kufundishia na kujifunza katika shule za msingi na sekondari ipoje?

Supplementary Question 1

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa majibu mazuri nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ukisoma ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 utaona kwamba kuna upungufu mkubwa wa upatikanaji wa vitabu mashuleni licha ya kwamba Serikali imepeleka fedha katika wizara husika. Kwa mfano ukiangalia Halmashauri Biharamulo ilikuwa na upungufu wa asilimia 45 katika ripoti ya CAG. Ukiangalia Halmashauri ya Bunda takriban vitabu 194,000 havikuwasilishwa mashuleni pamoja na kwamba Serikali imetoa fedha. Sasa je, Serikali haioni kuna haja ya kuzipatia fedha hizi shule husika ili wao wakagiza moja kwa moja kwa wazabuni badala ya utaratibu uliopo sasa hivi fedha hizi kwenda kwenye wizara ambao umekuwa na mlolongo mkubwa sana?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; uwiano kati ya kitabu na mwanafunzi sasa hivi ni kati ya kitabu kimoja wanafunzi watano tofauti kabisa na malengo ya Serikali moja kwa moja. Je, Serikali ina mpango gani wa dharura hasa katika zile halmashauri za pembezoni kuondokana kadhia hiyo katika hoja ya vitabu?

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahya Ally Mhata Mbunge wa Nanyumbu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya swali la msingi, kwamba Serikali hainunui vitabu badala yake Serikali kupitia TET inaratibu zoezi zima. Kwanza inatunga, inachapa na baadaye kusambaza. Gharama zinazotumika ni zile za kuhakikisha kwamba vitabu vinatungwa, vinachapwa na baadaye kusambazwa kwenye maeneo mbalimbali. Kwa hiyo naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kuwa zoezi hili kupitia mamlaka yetu ya elimu TET tutaendelea kuliafanya kwa uaminifu na uadilifu mkubwa kwa sababu ni jukumu letu la msingi kuhakikisha kwamba vitabu vinafika shuleni kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili amezunguzia suala la uwiano wa vitabu ni kweli uwiano wa vitabu bado hatujafikia katika ile ratio ya moja kwa moja lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea na zoezi hili na hivi sasa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa pale Mamlaka ya Elimu Tanzania kwa kununua mitambo ambayo yenye uwezo wa kuzalisha vitabu vingi kwa siku ambao utatuhakikishia sasa maene yote ambayo yenye upungufu wa vitabu tunaenda kuwafikia ili kuweza kufikia ile ratio ya moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo sasa hivi tumeanzisha maktaba mtandao ambayo katika yale maeneo ambayo mtandao upo au TEHAMA ipo vitabu hivi vinaweza kuwa accessed na wanafunzi pamoja na walimu kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.