Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kavejuru Eliadory Felix
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Primary Question
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi katika Ziwa Victoria na Tanganyika?
Supplementary Question 1
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Moja, kwa kuwa upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya uvuvi vimepungua; mazao hayo ya uvuvi na malighafi yanapungua, hayakidhi mahitaji ya viwanda: Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha vyombo na zana za uvuvi ili kuongeza ufanisi na tija? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna upotevu mkubwa wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa: Je, Serikali itasaidiaje kusambaza teknolojia rahisi za usindikaji wa mazao ya uvuvi ili kuyaongezea thamani kwa wavuvi wadogo wadogo? (Makofi)
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Jimbo la Buhigwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli moja ya changamoto tuliyonayo katika sekta ya viwanda ni ukosefu wa malighafi ambazo zinahitajika katika viwanda ambavyo vimepelekea baadhi ya viwanda kufungwa. Moja ya mikakati ya Serikali ambayo inatekelezwa kwenye mipango hii niliyoitaja ni kuwawezesha wavuvi na wenye viwanda kutumia teknolojia nzuri ya kisasa ambayo itapelekea kuvuna Samaki wanaohitajika katika viwanda badala ya kuvuna na wale madogo kwa maana ya makokoro ambayo yanatumika kuvuna hata mazalia.
Mheshimiwa Spika, pili, tuna mikopo mbalimbali, moja ni hii ya Halmashauri na pia kupitia taasisi zetu kama SIDO ambayo inawawezesha wavuvi kupata mikopo hiyo ili waweze kupata teknolojia za kisasa za kuvuna au kuvua samaki katika maeneo hayo. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kuwawezesha wavunaji au wavuvi ili waweze kupata teknolojia za kisasa kupitia mikopo.
Mheshimiwa Spika, pili, kwenye upotevu; ni kweli moja ya changamoto iliyopo ni upotevu wa mazao yanayotokana na uvuvi baada ya kuvunwa. Mara baada ya kuvua Samaki wanapotea au wanaoza. Moja ya maeneo, tunajenga industrial pack au kongani ambazo zitasaidia kuwa na maeneo maalum ya kutunzia Samaki ikiwa pamoja na kuvutia wawekezaji wa viwanda ili kuhakikisha mavuno yanayotoka baharini au kwenye maziwa yanaenda moja kwa moja kwenye viwanda ili kuchakatwa kabla ya kuharibika.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi katika Ziwa Victoria na Tanganyika?
Supplementary Question 2
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Jimbo la Bunda Mjini, limetenga eneo la Kata ya Mgeta kwa ajili ya Ukanda wa Uwekezaji, mpaka sasa hivi hawajawekeza; na Bunda pia tunavua: Kwa nini sasa Wizara isione kwamba kuna haja ya kujenga kiwanda kwa ajili ya vifaa vya uvuvi? (Makofi)
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi moja juu ya changamoto tulizonaao: Kwanza, ni mazao yenyewe yanayotokana na uvuvi kupungua; pili, kukosekana kwa viwanda ambavyo vinazalisha vifaa vya uvuvi ambavyo ndiyo teknolojia mahususi ambayo itapelekea kuvua kwa ubora zaidi mazao ya samaki.
Mheshimiwa Spika, katika mikakati ambayo tunaendelea nayo ni kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya kuchakata, lakini pia naamini tukifanikiwa hilo, hatua inayofuata nadhani ni kuweka sasa viwanda ambavyo vinazalisha vipuri vitakavyoweza kuzalisha zana za kuvuali Samaki katika sekta hii ya uvuvi. Kwa hiyo, nachukua hili kama sehemu ya changamoto na juhudi zetu kama Serikali, kuvutia zaidi wawekezaji katika viwanda vya kuzalisha vifaa vya kuvulia samaki katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved