Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na kupanda kwa bei za pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea?

Supplementary Question 1

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza na pia napenda nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa jibu lake zuri na pia kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa kutoa ruzuku kwenye pembejeo za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mikakati mizuri iliyowekwa na Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, hiyo mikakati hasa utoaji wa ruzuku utakuwa ni endelevu kiasi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa sababu ruzuku ilikuwa kwenye mbolea lakini kuna pembejeo zingine kama mbegu hasa za nafaka, je, Serikali ina mkakati gani pia wa kutoa ruzuku kwenye pembejeo aina ya mbegu pamoja na viatilifu kwa ajili ya kilimo? (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa ruzuku ya mbolea unategemeana sana na bei ya mbolea duniani na namna ambavyo wakulima wetu wataweza kumudu gharama hizo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango huu ni endelevu kwa muda wa miaka mitatu na tutakuwa tunaendelea kuangalia bei za dunia na kama ikitokea kwamba wakulima wanazimudu gharama, mpango huu pia hautaendelea kwa sababu ni mpango wa kumsaidia kumlima kuondokana na machungu ambayo ameyapata kutokana na kupanda kwa bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu mbegu za nafaka. Moja kati ya mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba, tunawafikia wakulima na kuwafanya wakulima wetu waweze kuzalisha kwa tija na eneo mojawapo ambalo tumekuwa tukiliangalia ni ruzuku kwenye eneo la mbegu na katika mwaka huu wa fedha tumefanya katika zao la ngano. Vilevile katika mahindi kupitia Wakala wa Mbegu Kilimo Tanzania, tumefanya hivyo kwa kushusha bei ambayo ni tofauti na bei iliyoko sokoni. Kwa mfano Mbegu za OPV za STUKA M1 zinapatika kwa Sh.2,750 tofauti na bei ilivyo sokoni, lakini mbegu za high breed za UH 6303 inauzwa kwa Sh.4,000 tofauti na bei iliyoko sokoni ya Sh.7,000, kwa hiyo ni sehemu pia ya ruzuku.

Name

Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na kupanda kwa bei za pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea?

Supplementary Question 2

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Benki ya Kilimo Tanzania imekasimu madaraka yake kwa Benki mbalimbali ikiwemo CRDB pamoja na NMB kwa ajili ya utoaji mikopo, lakini masharti yaliyokuwepo katika ukopaji huo ni magumu sana ikiwepo na kutoa asilimia ishirini na tano ya kile unachotaka kukopa, kutoa dhamana ya nyumba pamoja na cash flow ambayo inaelea katika benki ya mwaka mmoja. Je, ni lini sasa Serikali itapunguza masharti haya ili wakulima wapate nafuu kwa ajili ya kilimo na hasa wakulima wangu wa Bagamoyo ambao ni maskini? (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikiri ni kweli kumekuwa na changamoto ya wakulima wetu kukopesheka kirahisi na ndiyo maana Serikali tumechukua hatua madhubuti za kuhakikisha kwamba tunakaa na taasisi za fedha waelewe mfumo wa ukopeshaji katika kilimo ambao ni tofauti na maeneo mengine. Kwa hivi sasa tumekuja na mfumo mzuri ambao tumeu–design mikataba ya utatu ambayo imetusaidia sana kupunguza masharti mengi ambapo anakaa mkulima, anakaa off taker, anakaa na benki kwa upande mmoja ili mkulima aweze kukopesheka kutumia mikataba aliyonayo pasipo kutumia hati za nyumba na sababu zingine ambazo zinamfanya asiweze kufikia kwenye ukopeshwaji huo. Kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kama Serikali tumeliona hilo na tunaendelea na mikakati hii kuhakikisha kwamba mkulima wetu anakopesheka kirahisi. (Makofi)

Name

Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na kupanda kwa bei za pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea?

Supplementary Question 3

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naipongeza sana Serikali, naishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kutupatia mbolea ya ruzuku kipindi hiki. Hata hivyo, mbolea ile Jimboni kwangu ilifikia tu kwenye Makao Makuu ya Jimbo na wananchi wote kwenye Jimbo zima walikuwa wanasafiri kuifuata Mbungu. Je, Serikali ina mpango gani wa uhakika kwamba kipindi kijacho mbolea hii itafika sehemu zote ambako wananchi wanalima? Ahsante.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wakati tunaanza mfumo huu kwa mara ya kwanza, tumepitia changamoto hizo, lakini kama Wizara tumekaa, tumetafakari na kuzipitia changamoto zote na kuja na mkakati wa kudumu wa kuhakikisha kwamba mbolea hizi zinawafikia wakulima katika maeneo yao pasipo kutembea umbali mrefu. Mkakati huo ni kama ifuatavyo: -

(i) Hivi sasa tumeshawaagiza TFRA kuendele kusajili vituo vya mawakala karibu na maeneo ya wakulima;

(ii) Tutatumia pia Vyama vya Ushirika kwa ajili ya usambazaji wa mbolea; na

(iii) Tunatumia maghala ya Serikali yaliyoko katika maeneo mbalimbali kuhakikisha kwamba mbolea inafika katika maeneo ya uzalishaji ili wakulima wasitembee umbali mrefu. (Makofi)