Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kunti Yusuph Majala
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza kulipa fidia Wananchi wa Makole waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege na Mkonze waliopisha ujenzi wa SGR?
Supplementary Question 1
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba pamoja na hayo majibu ambayo hayaridhishi, nina maswali mawili madogo ya nyongeza: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja wa ndege, awali upanuzi ulikuwa ni mita 300 na upanuzi huo umeanza mwaka 2016. Mpaka tunavyozungumza sasa, ni miaka saba, wamepanua mita 150. Mita nyingine 150 waliwazuia wananchi wa Kata ya Makole kutokuendeleza maeneo yao, na mpaka sasa tunavyoongea nyumba zile zimekuwa ni magofu, watu walihama mle: Je, Serikali haioni wana sababu ya kuwalipa wananchi wa Kata ya Makole, kaya 50 zilizobaki kifuta jasho, ili waweze kufanya ukarabati wa nyumba zao na warudi kwenye makazi yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Ni sera ya Serikali kwamba, inapotwaa maeneo ya wananchi, inatakiwa ilipe fidia kwanza ndipo iendelee na utekelezaji wa miradi. Imekuwa ni kawaida ama ni tabia ya Serikali kuendelea kutwaa maeneo ya wananchi bila kuwalipa fidia na kuendeleza utekelezaji wa miradi, na matokeo yake wananchi wengi wamekuwa wakidhulumiwa. Hivi tunavyoongea…
MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa Kunti?
MHE. KUNTI Y. MAJALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, watu 46 walioko Mkonze hawajafanyiwa uthamini na Waziri hapa anasema waendelee kuvuta subira. Ni lini wananchi 46 waliobaki Mkonze watalipwa fidia yao kwa sababu tayari maeneo yao yameshachukuliwa na mradi umeshatekelezwa? (Makofi)
Name
Atupele Fredy Mwakibete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti Yusuph Majalla, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mwaka 2016 Serikali ilikuwa na nia kwa ajili ya ujenzi ama upanuzi wa uwanja wetu wa ndege wa hapa Dodoma, lakini Serikali ilipoanza ujenzi mwingine mpya, hususan katika kiwanja cha Msalato, ikaona haina sababu ya kuendelea kupanua uwanja mkubwa zaidi wakati uwanja mkubwa wa Kiwanja cha Msalato unaendelea kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, ilipofika mwaka 2018 na kupitia Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo pamoja na timu yake na wataalamu wetu kutoka TAA walipewa taarifa wananchi hawa kwamba eneo hilo, na kusudio la Serikali kuendelea kuupanua uwanja huu halitakuwepo tena, bali tutalipa zile fidia za mita 150 ambazo tayari tumeshalipa kwa kiasi cha Shilingi 1,900,000,000/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, kuhusu Mkonze, ni kweli kwamba, katika ujenzi wa TRC, kawaida unapojenga SGR, tunasema ni Design and Build, maana yake huwezi kufanya tathmini yote na ukalipa wananchi wote. Maana yake, inafanyika tathmini na wakati huo huo ulipaji unaendelea. Kwa maana hiyo basi, ifikapo tarehe 17 ya mwezi huu wa Aprili, wananchi wote wa eneo la Mkonze ambao hawajalipwa fidia zao tukutane eneo la SGR Station hapa Mkonze na waje na nyaraka zao, ahsante.
Name
Hawa Subira Mwaifunga
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza kulipa fidia Wananchi wa Makole waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege na Mkonze waliopisha ujenzi wa SGR?
Supplementary Question 2
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Jimbo la Tabora Mjini ni moja kati ya majimbo ambayo reli ya SGR imepita kwenye maeneo ya Ndevelwa. Wananchi wamefanyiwa tathmini ndogo, lakini pamoja na udogo wa tathmini hiyo, bado hizo fedha mpaka sasa tunavyozungumza wananchi hao hawajalipwa fedha zao: Ni lini Serikali itawalipa wananchi hawa fedha zao ili watafute maeneo mengine ya kuweza kujihifadhi? (Makofi)
Name
Atupele Fredy Mwakibete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namwomba Mheshimiwa Mbunge kwa suala la fidia katika eneo hili la SGR mara baada ya maswali na majibu tuonane ili tuweze kuwasiliana na wale wote ambao wanafanya zoezi hili la ulipaji kwa sababu, tunaendelea kulipa katika eneo hili, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved