Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Deodatus Philip Mwanyika
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Primary Question
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanzisha Special Economic Zone ili kuchochea viwanda vya uchakataji Njombe Mjini?
Supplementary Question 1
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali ambayo ni majibu ya kawaida (generic answers). Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, Mkoa wa Njombe na Halmashauri ya Mji wa Njombe ndiyo ina uzalishaji mkubwa sana wa zao la parachichi. Kwa bahati mbaya sana uzalishaji huo ni mkubwa lakini asilimia 90 mpaka 99 ya mazao ya matunda ya parachichi yote yanasafirishwa nje bila kuongezwa thamani kwa maana halisi ya uongezaji wa thamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu; Mheshimiwa Waziri anaweza kutoa commitment hapa leo kwamba watachukua suala la Mji wa Njombe na Mkoa wa Njombe kama special case ili waweze kuanzisha maeneo maalum kwa ajili ya uzalishaji na uchakataji wa parachichi tuache kupeleka maparachichi zikiwa ghafi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kama ataitoa commitment hiyo na atakubaliana nami na sioni kwa nini asikubaliane nami. Je, kuonesha umuhimu wa suala hilo, Waziri yuko tayari twende pamoja Njombe baada ya kusoma bajeti yake ili tukaanze majadiliano ya awali ya kuanzisha mchakato huo wa kuanzisha viwanda vya kuchakata parachichi badala ya kusafisha, kupaki na kusafirisha ambayo inatupotezea sisi mapato? Ahsante.
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli moja ya vigezo ambavyo vinatakiwa kwa ajili ya kuanzishwa maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya kuzalisha bidhaa kuuza nje (Special Economic Zones) ni uwepo wa malighafi; pili ni uwepo wa ardhi; zaidi ni miundombinu wezeshi kwa ajili ya kuzalisha bidhaa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe commitment ya Serikali na niwaagize Mamlaka ya EPZA waanze mchakato mara moja wa kuwasiliana na Mkoa wa Njombe, na kutafuta wadau wengine. Kwa sababu katika maeneo haya ya uwekezaji kwa ajili ya mauzo nje tunashirikiana pia na sekta binafsi ili kuhakikisha mkoa huu sasa unakuwa na eneo kwa ajili ya kuzalisha bidhaa au kuzalisha maparachichi ambayo yatauzwa nje ikiwa ni bidhaa zake au maparachichi yenyewe ili kuongeza uchumi wa Mkoa wa Njombe na azma ya kupunguza kuuza malighafi nje, yakiwemo na maparachichi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya commitment hiyo na EPZA wataanza kufuatilia, na mimi nikubaliane naye, nitakwenda Mkoa wa Njombe ili tuweze kuona namna ya kujadiliana na wadau ukiwemo mkoa, kupata ardhi na wadau wengine kwa ajili ya kuwekeza au kuanzisha maeneo huru ya uwekezaji katika Mkoa huo wa Njombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved