Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Martha Festo Mariki
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya upungufu wa Watumishi katika Mkoa wa Katavi?
Supplementary Question 1
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Serikali, lakini katika Mkoa wetu wa Katavi changamoto bado ni kubwa sana. Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika vituo vya afya pamoja na Hospitali za Wilaya, lakini hospitali hizo zinashindwa kufanya kazi kama hadhi ya Hospitali ya Wilaya na badala yake kufanya kazi kama zahanati kutokana na upungufu mkubwa sana wa watumishi katika hospitali zetu za Wilaya za Mkoa wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nijue, zipi hatua za haraka za Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Katavi wanaweza kupata watumishi ili waweze kupata huduma zilizo bora? Ahsante. (Makofi)
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Martha Mariki, Mbunge wa Katavi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inatambua upungufu uliopo katika hospitali ndani ya Mkoa wa Katavi, lakini katika kupitia utaratibu ambao Serikali imeuweka kupitia mifumo ambayo tumeianzisha ndani ya Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, ambapo mojawapo ni pamoja na HR Assessment System, tumeweza kugundua hilo tatizo. Pia kwa kupitia mifumo ya upangaji wafanyakazi, tumeshaliona jambo hilo na ndiyo tumeahidi kupitia bajeti hii inayokuja ambayo tutawasilisha mbele ya Bunge lako hapa, kwamba hilo jambo la upungufu wa watumishi katika Mkoa wa Katavi nalo pia ni moja kati ya jambo tunalokwenda kulishughulikia.
Name
Selemani Moshi Kakoso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Vijijini
Primary Question
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya upungufu wa Watumishi katika Mkoa wa Katavi?
Supplementary Question 2
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa watumishi wengi wanaojitolea wamefanya kazi ya ziada, na kila mara ajira zinapotoka hawa wanaojitolea huwa hawapewi nafasi ya kupewa ajira: Je, Serikali mna mpango gani wa kuwasaidia wale wanaojitolea katika nafasi za Ualimu na Unesi waweze kupewa nafasi hizo? (Makofi)
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Kakoso, Mbunge wa Tanganyika, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anayoyasema kwamba kumekuwa na watu wanaojitolea lakini wakati mwingine inapotokea ajira zimefunguliwa wanapata matatizo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mwongozo wa ajira katika nchi yetu unataka ajira zote ziwe katika ushindani. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama watafuata taratibu zilizowekwa, hatuna tatizo katika jambo hilo.
Mheshimwia Mwenyekiti, ni kweli kwamba tatizo la upungufu wa walimu na kada nyinginezo katika utumishi wa umma ni jambo ambalo tunalijua na Serikali imeendelea kulishughulikia jambo hilo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kufanya hivyo kama ambavyo tumeahidi na katika bajeti yetu tunakuja kusoma hapa hivi karibuni ya mwaka 2023/2024, majibu yote atayapata.
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya upungufu wa Watumishi katika Mkoa wa Katavi?
Supplementary Question 3
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Katika Halmashauri ya Lushoto yenye shule za msingi 180, ina uhaba wa walimu takribani 1,400, hali inayosababisha sasa angalau wastani wa shule moja kuwa na walimu wanne tu: Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kuhakikisha kwamba inakwenda kuboresha ikama katika Halmashauri ya Lushoto? (Makofi)
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Rashid Shangazi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba upungufu upo kama nilivyokiri katika jibu la msingi, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo la ikama la mahitaji ya walimu au madaktari au kada zozote katika maeneo yetu linaanza kwenye mchakato ndani ya Halmashauri zetu. Kwa hiyo, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Halmashauri yake ya Lushoto ilete mahitaji hayo, nasi kama Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, tutalichukua jambo hili na kwenda kulifanyia kazi na tutakapopata kibali cha ajira, basi tutahakikisha kwamba tunampelekea wafanyakazi kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anahitaji.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved