Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Yahya Ally Mhata
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Primary Question
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: - Je, ni wananchi wangapi wa Jimbo la Nanyumbu wamefidiwa kutokana na uharibifu uliofanywa na tembo katika mashamba yao?
Supplementary Question 1
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba niulize maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; takwimu ananzozieleza Naibu Waziri sio sahihi. Takwimu ambazo ninazo za waathirika wa wanyama waharibifu ni zaidi ya watu 200.
Je, Waziri yupo tayari kumwagiza Afisa wake aliyopo pale Masasi aende akafanye mapitio mapya ya waathirika wote walioathirika na Wanyama waharibifu hasa tembo katika Kkata ya Sengenya, Kijiji cha Mkumbaru, Chinyanyera, Igunga; Kata ya Nangomba Kijiji cha Chihuve; Kata ya Luimesule; na Kata ya Masugulu? Takwimu hizi sio sahihi kwa hiyo namuomba Waziri afanye hayo kama nilivyomwelekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; fidia wanazolipwa waathirika ni ndogo kuliko hali halisi ilivyo. Waathirika hawa wanaopoteza maisha yao fidia ni ndogo, wanaopata ulemavu fidia ni ndogo na wanaoharibiwa mashamba yao fidia ni ndogo. Je, Waziri yuko tayari kuleta Muswada hapa wa kurekebisha viwango hivi ili wananchi walipwe haki sawa kulingana na hali halisi? (Makofi)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwenye hili suala la takwimu nitazichukua kutoka kwake, lakini pia tutaenda kuhakiki upya katika maeneo hayo ili wananchi waweze kulipwa stahili yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande huu wa fidia sheria ya mwaka 2011 iliyopitisha kifuta machozi na kifuta jasho ilikuwa na madhumuni ya kumshika mkono mwananchi, lakini ukiangalia namna ya kufidia mfano maisha ya mwananchi ambaye amepoteza maisha ni ngumu sana kufidia au mtu ambaye amepata ulemavu, hivyo sheria hii ilipitishwa kwa ajili ya kumshika mkono mwananchi kumwonesha kwamba Serikali iko pamoja naye.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo katika Bunge lako hili mwaka jana tulipewa maelekezo ya kuzipitia upya Kanuni zake zinazohusiana na masuala ya kifuta machozi na jasho na hivi karibuni tutaileta katika Bunge lako hili kwa ajili ya kuipitia ili tuweze kuongeza kiwango hiki na Kanuni zirekebishwe, ahsante.
Name
Cecilia Daniel Paresso
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: - Je, ni wananchi wangapi wa Jimbo la Nanyumbu wamefidiwa kutokana na uharibifu uliofanywa na tembo katika mashamba yao?
Supplementary Question 2
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Endapo ikitokea mwananchi ameua tembo au gari limegonga tembo au mnyama yoyote faini anayotozwa ni kubwa sana, lakini ikitokea vinginevyo kwamba mnyama amemuua mwananchi au ameharibu mazao yake, sheria haimpi haki mwananchi. Je, nini kauli ya Serikali ku-balance haya mambo ili kuhakikisha kwamba Mtanzania anapata haki yake ndani ya nchi yake? (Makofi)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tutambue kwamba hawa wanyama ambao tunao katika nchi yetu ni rasilimali za Taifa na wanalindwa kisheria kama ambavyo tunawalinda wanadamu na tutambue kwamba changamoto hii ya wanyamapori wakali na waharibifu imeanza hivi karibuni. Miaka ya nyuma wanyama hao walikuwa wanaishi kwa uhuru na salama kabisa na hatukuwahi kuwa na changamoto hizi. Kwa hiyo ukiangalia mahitaji ya ardhi, ongezeko la watu tumeendelea kusogea katika maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukisema leo hii changamoto hii tuielekeze kwenye faini, mzigo ni mkubwa sana kwa Serikali hautaweza kugharamia hasara ambayo itaweza kujitokeza. Kwa hiyo tunaendelea kuhamasisha wananchi kwamba tusiendelee kuyasogelea maeneo haya na ndio maana kanuni hii ilitungwa kwa wale ambao Wanyama wamewafata basi tunawashika mkono ili kuhakikisha kwamba Serikali inaonesha kwamba iko nao.
Name
Mussa Azzan Zungu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ilala
Primary Question
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: - Je, ni wananchi wangapi wa Jimbo la Nanyumbu wamefidiwa kutokana na uharibifu uliofanywa na tembo katika mashamba yao?
Supplementary Question 3
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri kuna kero ya popo Kata ya Kivukoni Jimbo la Ilala. Hawa popo ni waharibifu, wanachafua mazingira na wananchi walishalalamika mpaka leo bado. Hebu tueleze mnachukua hatua gani kwa upande wa popo Kata ya Kivukoni? (Makofi/Kicheko)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Naibu Spika, ni kweli kuna changamoto ya popo ambao wamezunguka katika maeneo ya Dar es Salaam hususan maeneo yanayozunguka Ikulu. Serikali imeshaanza kuyafanyia kazi tulishawahi kufanya kazi ya kuwapuliza kwa maana ya kuwapunguza, lakini changamoto tunayoipata ni kwamba tunapowaondoa wanaruka wanaondoka, lakini kuna muda ambao wanarudi. Sasa tumeshaanza utaratibu na Taasisi ya TAWIRI kutafuta mbinu mbadala kuhakikisha tunawaondoa kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuahidi kabla ya Bunge lako hili la bajeti kwisha, tutakuwa tayari tumeshakamilisha utaratibu wa kuwaondoa.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved