Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Aida Joseph Khenani
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Primary Question
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: - Je, kwa nini wanufaika wa TASAF wasilipwe mkononi badala ya kupewa kwa njia ya simu na benki?
Supplementary Question 1
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nimesikia majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali langu la kwanza, lengo la kuwapelekea hizi fedha lilikuwa ni kuwasaidia tukiamini ni masikini, kwa hiyo hawana uwezo wa kununua simu. Kwenye simu kuna makato na benki kuna makato. Hatuoni kuweka hilo jambo ni kuondoa lile lengo la kuwasaidia hawa wanufaika ambao hawawezi hata kununua simu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mchakato wa kuwapata wanufaika uligubikwa na mambo mengi sana ikiwemo ubaguzi wa kivyama, kwa maana ya vyama vya siasa. Nini kauli ya Serikali kupitia upya tena mchakato huu ili tuwapate wenye sifa wanaostahili kuwa wanufaika wa TASAF?
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nataka nirejee tena maelezo ambayo nimeyatoa katika swali la msingi.
Mheshimiwa Spika, malipo ya pesa hizi yako katika njia kuu tatu, ni choice ya mhusika mwenyewe njia gani aitumie. Kama akiona kwamba njia ya simu ni ngumu kwake kwa sababu hana simu hiyo inayopokea, anaweza kwenda katika njia nyingine ya benki. Kama akiona njia nyingine ya benki ni ngumu kwa sababu benki iko mbali, upo utaratibu wa kulipa fedha taslimu kupitia madirisha yetu. Kwa hiyo, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge option hizi zote zinawezekana katika maisha ya kawaida ya ubinadamu wetu na Watanzania wetu na mimi na Serikali tunaamini hivyo.
Mheshimiwa Spika, juu ya swali la pili la upatikanaji wa wanufaika. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kweli kwamba baadhi ya maeneo kumetokea changamoto juu ya utambuzi wa wanufaika katika miradi hii ya TASAF, Serikali imekwishayafanyia kazi katika baadhi ya maeneo na tunaendelea kutambua katika yale maeneo yenye changamoto, nataka nikuhakikishie katika Jimbo lako la Nkasi Kaskazini nako pia timu ya TASAF itafanya kazi, nasi tunategemea zaidi ushirikiano kutoka kwako Mheshimiwa Mbunge ili kuweka mambo ya wanufaika vizuri kwa sababu nia ya Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba wanufaika wote au walengwa wote wa TASAF wanafikiwa na kufikia malengo yao. Ahsante.
Name
Husna Juma Sekiboko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: - Je, kwa nini wanufaika wa TASAF wasilipwe mkononi badala ya kupewa kwa njia ya simu na benki?
Supplementary Question 2
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Wapo wanufaika waliowahi kunufaika na TASAF nazungumzia wazee, vikongwe ambao hawana wasaidizi walio katika Wilaya ya Korogwe, ambao wametemwa na mfumo wa TASAF.
Je, Serikali haioni kama imewaonea wazee wale kuwaondoa kwenye mfumo ingali bado hawawezi kujikimu maisha yao?
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sekiboko, Mbunge wa Tanga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, utambuzi wa wanufaika wa TASAF ni utambuzi shirikishi ambao unaanza ngazi za vijiji na ngazi hiyo tunaamini kabisa kwamba kila mmoja anamtambua na kumjua mwenzake. Utambuzi ndani ya level ya Serikali ni level ya uhakiki tu. Tunachokiangalia kama Serikali ni zile taarifa ambazo zinatoka katika kijiji ambacho wahusika hawa au wanufaika wanatokea. Kwa hiyo, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge siyo nia ya Serikali kuwadhulumu watu au kuwanyima wanufaika haki yao.
Mheshimiwa Spika, natoa angalizo sana kwa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Halmashauri zetu, kuhakikisha kwamba wanufaika wote wanaotakiwa kuingia kwenye mfumo wa TASAF wanaangaliwa na kutambuliwa ili Serikali iweze kufikia malengo yake ya kuwasaidia Watanzania wenye uhitaji katika mfumo huu mzima wa kunyanyua maisha ya wale ambao wanaonekana wanahitaji kuingizwa katika mfumo wa TASAF ili kuwawezesha kiuchumi.
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: - Je, kwa nini wanufaika wa TASAF wasilipwe mkononi badala ya kupewa kwa njia ya simu na benki?
Supplementary Question 3
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafsi.
Mheshimiwa Spika, ninataka kujua kwamba, kwenye vijiji vyetu kuna watu ambao walipaswa kuwa na sifa kupata huduma ya TASAF na viongozi wengi wa vitongoji na vijiji wameweka watu ambao hawana sifa. Nini mpango wa Serikali kufanya auditing kuhakikisha kwamba watu wote ambao wanapaswa kuingizwa kwenye mfumo wanaingizwa na wale ambao hawapaswi kupata hiyo huduma watolewe katika huduma hiyo?
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika swali lililoulizwa na Mheshimiwa Sekiboko, naomba kurudia tena mbele yako na kulieleza Bunge lako na Watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, mfumo wa utambuzi wa wanufaika wa TASAF ni mfumo shirikishi ambao unaanzia kwenye ngazi za vijiji vyetu, kwa hiyo ninachotegemea kutoka kwa wananchi ambao watashiriki mkutano wa utambuzi ni kuweza kuwatambua watu wote wanaotakiwa kushiriki katika mfumo huo.
Mheshimiwa Spika, nataka nitoe taarifa ndogo, tumewahi kufanya ziara katika baadhi ya Wilaya, tumekwenda pale tukakutana na kituko cha mwaka. Watu wanakataa watu walioingizwa kwenye mfumo wa TASAF ndiyo haya ambayo Mheshimiwa Waitara anayasema. Nataka nirudie tena mfumo huu ni mfumo shirikishi na nitoe wito kwa wananchi wote katika maeneo yote, mnapoitwa katika mikutano ya TASAF hebu jaribuni kushiriki ili kuondoa ubabaishaji wa baadhi ya watu ambao wanachomeka ndugu zao na watu wasio na sifa katika mfumo huu na kudhulumu wale watu wenye sifa, wanaostahili kuingia katika mfumo wa TASAF. (Makofi)
Name
Charles Muguta Kajege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwibara
Primary Question
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: - Je, kwa nini wanufaika wa TASAF wasilipwe mkononi badala ya kupewa kwa njia ya simu na benki?
Supplementary Question 4
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nashukuru majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini zoezi zima la utambuzi katika Jimbo la Mwibara lime – collapse.
Je, ni lini Serikali itafanya tena zoezi hilo upya?
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mwijage, Mbunge wa Mwibara, samahani kwa kukuchanganya majina nimekuita Mheshimiwa Mwijage badala ya Mheshimiwa Kajege. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika eneo lako la Mwibara nikiri kwamba mimi kama Naibu Waziri sijapata taarifa za kina juu ya wapi tatizo lilitokea na nini kilitokea mpaka zoezi zima likasimama, lakini ninaomba nilichukue hilo jambo na baada ya kumaliza session hii ya maswali na majibu tukutane na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kujadili kwa kina tuone nini kinafanyika na wapi walikosea ili tuende tukasahihishe tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, naendelea kusisitiza tena kwamba ni nia ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba wanufaika wote wa TASAF tunawafikia na kuwatendea haki katika kupata wanachostahili. (Makofi)
Name
Hussein Nassor Amar
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyang'hwale
Primary Question
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: - Je, kwa nini wanufaika wa TASAF wasilipwe mkononi badala ya kupewa kwa njia ya simu na benki?
Supplementary Question 5
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kuambatana nami baada ya Bunge hili, kwenda Wilayani Nyang’hwale kuonana na akina mama wakongwe zaidi ya 80 ambao wameorodheshwa na zaidi ya miaka mitatu hawajapata stahiki yao? (Makofi)
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nipo tayari na tutaongozana ili kwenda kuwatambua na tuzungumze kwa pamoja. Siyo tu utambuzi wa hawa, lakini pia suala zima la changamoto zilizopo katika eneo lake la utawala kuhusiana na mradi wetu huu wa TASAF. (Makofi)