Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ally Anyigulile Jumbe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Primary Question
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza: - Je, ni lini umeme wa REA utafika katika Kijiji cha Ikombe – Kyela?
Supplementary Question 1
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Ikombe ni kijiji ambacho kiko pembezoni sana na ni kisiwa ambacho hakifikiwi kirahisi. Leo hii tunapouliza hili swali wananchi wa Ikombe wamewatuma viongozi wao waje washuhudie majibu haya ya Serikali, wako hapa leo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ETDCO ambao wanasambaza umeme wa REA walianza kazi hii Agosti, 2021 na wamefikia vijiji 21 tu na vijiji vilivyobaki ni 14. Na katika vijiji hivyo 14 bado hata nyaya hazijavutwa wala hakujatokea uwezekano wa kupeleka nguzo na mkataba unaisha ndani ya siku kumi zijazo, swali la kwanza: -
Je, sasa Serikali haioni umuhimu mkubwa wa kushirikiana na TANESCO ili kwa Kyela vijiji hivyo viishe mapema?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni maajabu gani yatatokea kufanikisha ndani ya siku kumi mkataba huu uendelee ufike mpaka watakapofikisha hapo Juni pale Ikombe? Ahsante.
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa spirit ya kutotaja kumuwakilisha Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya muda naomba niendelee.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu mawali ya nyongeza la Mheshimiwa Ally Anyigulile kwa ujumla wake kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna mikataba ambayo muda wake utaisha kabla kazi hazijakamilika, lakini nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapata umeme. Na tunachokifanya ni kukabana na wakandarasi wote wanaopeleka miradi yetu ya umeme kwenye maeneo mbalimbali kuhakikisha wanamaliza kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, lakini sababu nyingine moja inayofanya kazi izidi muda wa mkataba wa awali ni kuongezeka kwa hizo kilometa mbili ambazo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa pesa ya nyongeza kwa ajili ya kuongeza scope. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Ally kwamba kama tulivyosema kabla ya mwezi Juni hicho kijiji kitakuwa kimepata umeme na wananchi wataweza kuutumia katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, na kwa mkandarasi ETDCO yupo zaidi ya asilimia 60 na vijiji 14 vilivyobaki vitakamilika katika huu muda ambao tumejipangia kwa spidi mpya ambayo tuko nayo kwa sasa. Ahsante.
Name
Noah Lemburis Saputi Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Primary Question
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza: - Je, ni lini umeme wa REA utafika katika Kijiji cha Ikombe – Kyela?
Supplementary Question 2
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka au kusambaza umeme kwenye vijiji na vitongoji katika Jimbo la Arumeru Magharibi ambayo imekuwa ni changamoto sana wananchi kupata umeme? (Makofi)
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Noah Saputi, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama Ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upo mradi ambao unaendelea wa upelekaji wa umeme katika vijiji wa REA III Round Two ambao pia unahusika katika kufikisha umeme kwenye vitongji. Lakini muda si mrefu tutaanza Mradi mwingine unaitwa Densification IIC ambao una takribani vitongoji 2,600, nao ni kwa ajili ya kupeleka umeme katika vitongoji.
Mheshimiwa Spika, lakini kama ambavyo tumekuwa tukisema, tunatafuta pesa kwa ajili ya upelekaji wa umeme katika vitongoji vyote 36,000, takribani trilioni sita na bilioni mia tano ili kumaliza tatizo lolote la umeme. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba kwenye vile vijiji vilivyopo kwenye mradi kabla ya Desemba mwaka huu vitaisha na pesa nyingine itatafutwa kufikisha katika maeneo mengine.
Name
Margaret Simwanza Sitta
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Urambo
Primary Question
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza: - Je, ni lini umeme wa REA utafika katika Kijiji cha Ikombe – Kyela?
Supplementary Question 3
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo kubwa la kukatikakatika kwa umeme Wilayani Urambo, Serikali inasema nini kuhusu kumaliza ujenzi wa Kituo cha Uhuru ambacho kitakuwa ukombozi kwetu sisi? Ahsante.
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Sitta, Mbunge wa Urambo, kama Ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Kupoza Umeme cha Uhuru kilichopo katika Jimbo la Urambo kinatekelezwa katika mradi tunaouita Mradi wa Gridi Imara ambao unapokea umeme wa kilovoti 33 kutoka Tabora Mjini na mkandarasi tayari ameshapatikana ameshaagiza vifaa, na kabla ya katikati ya mwaka unaokuja tunatarajia Mradi huu wa Gridi Imara utakuwa umekamilika katika maeneo mengi likiwemo eneo la Kituo chetu cha Kupooza Umeme cha Uhuru kwa ajili ya kuhudumia wananchi walioko hapo na kupeleka Gridi ya umeme mpaka katika Wilaya ya Uvinza kupitia pale Uhuru.
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza: - Je, ni lini umeme wa REA utafika katika Kijiji cha Ikombe – Kyela?
Supplementary Question 4
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, katika Jimbo la Bunda Mjini, hasa kata saba za vijijini, kumekuwa na changamoto ya umeme kutofika kwenye nyumba za wananchi, unaishia senta: -
Je, ni lini sasa mtapeleka nguzo za kutosha ili ile dhana ya umeme vijijini iwe imekamilika?
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya kama Ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hii miradi ambayo tunaitekeleza inalenga kumfikia kila mwananchi. Lakini kwa sababu ya bajeti tuliyokuwa nayo na fedha ambayo haitoshelezi kwa wakati huu kwa maeneo yote, advancement inakwenda taratibu.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mradi wetu wa ku-electrify vitongoji vyote ambapo tunatafuta trilioni sita na bilioni mia tano, tunaamini kwamba kila mtu atafikiwa na umeme na katika miaka mitatu, minne, mitano ijayo, hakutakuwa kuna mwananchi katika kitongoji au eneo lolote ambaye hana umeme kwa sababu hiyo ndiyo azma ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Name
Rose Vicent Busiga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza: - Je, ni lini umeme wa REA utafika katika Kijiji cha Ikombe – Kyela?
Supplementary Question 5
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza: -
Ni lini Serikali itapeleka umeme katika Kata ya Ng'homolwa, Kijiji cha Nkweni?
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rose Busiga, Mbunge wa Viti Maalum Geita, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba naamini kijiji hicho na kata hiyo ipo katika mradi wetu wa REA III Round Two, na kabla ya mwaka huu kuisha kijiji hicho kitakuwa pia kimepata umeme kwenye baadhi ya vitongoji na sasa maendeleo yataendelea kwenye vitongoji ambavyo vitakuwa vimebaki.
Name
Anatropia Lwehikila Theonest
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza: - Je, ni lini umeme wa REA utafika katika Kijiji cha Ikombe – Kyela?
Supplementary Question 6
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Licha ya wananchi wa Kata ya Kibale, Kijiji cha Kigorogoro, lakini pia Businde na Lukuraijo Mkombozi kukatiwa migomba na mikahawa kwa ajili ya kuwekewa nguzo za umeme, ni zaidi ya mwaka mmoja hawajapatiwa umeme; ni lini wananchi hao watapatiwa umeme? (Makofi)
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anatropia Theonest, Mbunge wa Viti Maalum Kagera, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mkandarasi anayepeleka umeme katika Mkoa wa Kagera anaitwa JV Pomina Kwihaya, na yuko kazini anaendelea. Ni kweli alisuasua, katika wale wakandarasi saba ambao tulikuwa tunaona progress zao siyo nzuri na yeye alikuwemo. Lakini tumeweka strategy mpya na ninaamini Waheshimiwa Wabunge wengi wameona tumaenzisha ma-group ya whatsApp kwa ajili ya kupata updates za kila siku.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kabla ya mwaka huu kuisha umeme utakuwa umefika katika maeneo hayo kwa sababu ndiyo makubaliano yetu sisi na wakandarasi wote wanaopeleka umeme katika maeneo ya vijijini.
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Primary Question
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza: - Je, ni lini umeme wa REA utafika katika Kijiji cha Ikombe – Kyela?
Supplementary Question 7
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Ni lini wananchi wangu wa Kata za Pangale, Mpombwe, Tutuo, Sikonge, Mkolye hadi Ipole watapata fidia ambayo wamepisha njia ya kupita umeme?
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakunda kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inajenga laini ya kilovoti 33 ya kupeleka Gridi ya Taifa Katavi ambapo inatokea Kituo chetu cha Tabora inapita Ipole ambako ndiko katika jimbo lake, inakwenda Inyonga na baadaye inafika Mpanda Mjini.
Mheshimiwa Spika, laini yote hiyo ina jumla ya kilometa
380 na pesa zimeshapatikana kwa ajili ya kulipa fidia, na mkandarasi anaingia site karibia kwenye mwezi Julai au Agosti. Kabla ya muda huo fidia itakuwa tayari imelipwa ili Gridi ya Taifa iweze kufika Katavi na wananchi wake wataweza kulipwa fidia ambayo wanastahili kupewa.
Name
Venant Daud Protas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Primary Question
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza: - Je, ni lini umeme wa REA utafika katika Kijiji cha Ikombe – Kyela?
Supplementary Question 8
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kawekapina, Ipululu na Vumilia Kata ya Igalula wanacheleweshewa kupata umeme kwa sababu ya mgogoro wa TANESCO, TRC na REA: -
Je, ni lini mtaumaliza mgogoro huu wa kuvusha nyaya kwenda kwenye vijiji hivyo ili wananchi wapate umeme kwa wakati?
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Venant, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, TANESCO na REA wako tayari na wanayo fedha kwa ajili ya kuvusha umeme kwenye line ya SGR lakini wenzetu wa Wizara ya Uchukuzi walikuwa hawajajua eneo gani watuoneshe kwa ajili ya kupitisha njia na sisi tusingependa tutumie pesa nyingi kupisha eneo temporary halafu baadae kidogo tuhamishie kwingine. Tumekaa pamoja na wenzetu wa TRC watatuonesha sehemu ambayo ni ya kudumu tutakayopitisha miundo mbinu hiyo ili wananchi waweze kupata umeme katika maeneo hayo. Kwa hiyo nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalifatilia na tutalikamilisha kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma.