Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Primary Question

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka Meli ndogo ya abiria Muleba pamoja na kutumia meli ya MV Victoria kujaribu masoko ya nchi za Uganda na Kenya?

Supplementary Question 1

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE : Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, gati la kuegesha meli katika Kisiwa cha Godzba baada ya maji kushuka ya Ziwa Victoria, kuegesha meli za Songoro Marine na hiyo Clarias imekuwa ni shida. Serikali mnaonaje haraka mtujengee gati lile liweze kuhimili kupokea meli zetu maji yanapopanda na kupwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza; visiwa vya Ikuza bandari ya Magarini, Mazinga, Bumbile Kerebe havijahusishwa kwenye mpango wa Serikali ulioutaja. Je, ni lini Serikali itaangalia gati za visiwa hivyo na kuweza kuzitekeleza kusudi Muleba nzima iweze kukamilika?

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Charles John Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika gati hili la Godzba kuna changamoto ya maji kushuka na hivyo kusababisha gati hilo kutotumika ipasavyo na meli hizi. Kwa maana hiyo, Serikali inatoa maelekezo kwanza kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini kutuma timu ya wataalam ili kulirekebisha gati hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa hatua za awali kwa kuwa wenzetu wa MSCL wana-floating dock tatu (tishari), nataka moja ije eneo hili la Godzba ili lianze kufanyakazi wakati meli hii inafanya kazi eneo hili na tishari nyingine itaenda katika kisiwa cha Gana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anataka kujua ni lini tutapeleka huduma katika visiwa vya Kerebe Bumbile, Kyamkwikwi, Godzba na maeneo mengine. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa meli hii ya MV Clarias tayari tumeshakamilisha matengenezo yake jana na tunategemea ndani ya wiki hii, namuelekeza mkurugenzi wa TASAC atume timu yake ya wataalamu ili wakajiridhishe na hatimaye meli hii ianze kufanya kazi. Kwa maeneo ya visiwa ambavyo umevitamka Mheshimiwa Mbunge nako tutaanza kupeleka huduma kama ambayo inafanya sasa maeneo mengine. Ahsante.

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Primary Question

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka Meli ndogo ya abiria Muleba pamoja na kutumia meli ya MV Victoria kujaribu masoko ya nchi za Uganda na Kenya?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ziwa Tanganyika ukianzia Kigoma mpaka Kalambo tulikuwa tukitegemea meli ya MV Liemba pamoja na MV Mwongozo, ni muda mrefu sana hatuna usafiri wa meli.

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya kuhakikisha kwamba inapatikana meli kwa ajili ya kusafirisha abiria na mizigo? (Makofi)

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Ziwa Tanganyika tuna changamoto za meli, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuelekeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, sekta ya Uchukuzi kwamba mwaka huu wa fedha tunakwenda kusaini mikataba minne ya ujenzi wa meli tatu pamoja na chelezo kubwa katika Ziwa hili la Tanganyika kwa maana ya meli tatu, meli mbili zitakuwa Ziwa Tanganyika na chelezo na meli moja itakuwa Ziwa Victoria. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wote wa ukanda wa Kigoma kwamba kwa meli hii ya MV Liemba ambayo tayari tupo hatua za mwisho za kumpata Mkandarasi pia itakarabatiwa.