Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Mary Machuche Mwanjelwa
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mbeya Mjini
Primary Question
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA aliuliza:- Kila jamii ina mila na desturi zake; hapa nchini wanamuziki wamekuwa hawavai mavazi ya staha au utu wa mwanamke umekuwa ukidhalilishwa kutokana na kuvaa nguo zinazoonesha maungo yao. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti mavazi yasiyo na staha kwa wanamuziki wa kike?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nilikuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
La kwanza, mwanamke ni tunu katika uumbaji wa maisha ya mwanadamu na kwa kuzingatia mila na desturi zetu za Tanzania nilikuwa nataka kujua Serikali inawashirikisha vipi viongozi hawa wa dini wakishirikiana na wasanii hao pamoja na majibu yake aliyotoa juu ya elimu kwa umma na umuhimu wake?
La pili katika Serikali ya Awamu ya Nne iliyopita Waziri husika alikuwa ameunda Kamati ya Vazi la Taifa ambalo nchi zawenzetu wengine wa hapa Afrika, ndio kutambulisha Utaifa wao nilikuwa nataka Mheshimiwa Waziri atueleze jambo hili limefikia hatua gani na mikakati yake endelevu? Ahsante.
Name
Nape Moses Nnauye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Answer
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, la kwanza juu ya ushiriki wa viongozi wa dini na makundi mengine katika jamii katika kuhakikisha sanaa yetu inatumika vizuri na haimdhalilishi mwanamke.
Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba kwanza ni kweli kwamba mwanamke ni ana hadhi yake katika jamii na hasa katika jamii zetu za Kiafrika na nimpongeze sana Mheshimiwa Mary Mwanjelwa kwa namna anavyopigania hadhi ya mwanamke katika Taifa letu. (Makofi)
Wizara yangu inatoa wito si tu kwa viongozi wa dini hawa wasanii wetu wamo katikakati ya jamii zetu, hawa wasanii ni watoto wetu, ni ndugu zetu na wanaingia kwenye nyumba mbalimbali za ibada na kukutana na viongozi wetu wa dini, natoa wito kila mmoja wetu aone kwamba kuna umuhimu wa kila mmoja kushiriki na kuwahamasisha wahakikishe wanazingatia maadili ya Mtanzania katika shughuli zao za sanaa.
Mheshimiwa Spika, nataka nilihakikishie Bunge lako ikiwa jamii itayakataa matendo yanayofanywa na wasanii, wasanii hawa wataacha kufanya hayo matendo, lakini ikiwa jamii inayashabikia na kuyapenda, wasanii hao wataona ndio fashion na wataendelea kufanya. Kwa hiyo, hata kama sisi tukihamasisha namna gani kama jamii haitayakataa na kuyaona hayafai, kila Mtanzania akaona mwanamke akidhalilishwa amedhalilishwa mzazi wake, amedhalilishwa ndugu yake, haya matendo yatakoma katika jamii yetu.
Kwa hiyo nadhani ni suala la jamii yetu zaidi kuyakataa na kuwatenga kijamii wale ambao wanafanya shughuli za kuwadhalilisha akina mama wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Vazi la Taifa na wakati wa bajeti niliulizwa hili swali na nililitolea ufafanuzi, ni kweli ulifanyika mchakato wa kutafuta Vazi la Taifa hapa lakini tulikuja kugundua kwamba ule mchakato tukiendelea nao mpaka mwisho tunaweza tukajikuta tumetoka na vazi la viongozi na sio Vazi la Taifa. Jamii yetu Watanzania tuna makabila 126 kila kabila lina aina yake ya kuvaa, mnaweza mkaendeleza mkafanya mchakato mkafika mwisho halafu mnakwenda mnawaambia Wamasai waache mavazi yao wachukue hili la kwenu, iko hatari ya kuwa na vazi la viongozi na badala ya kutengeneza Vazi la Taifa. Sasa tukatoa wito kwamba kwa ule mchakato ulipofikia ulipendekeza vazi la kanga kuwa ndio vazi preferable ambalo kwa kweli watu wanaweza wakalitumia. Lakini tunaogopa kufikia mahali pa kutengeneza vazi tukalilazimisha na likabaki kuwa vazi la viongozi.
Mheshimiwa Spika, lakini hata hayo mataifa mengine ambayo yana mavazi ambayo yanaonekana yanawakilisha Utaifa wao hawakufanya mchakato wa kufikia Vazi la Taifa. Ilikwenda ikatokea wakajikuta wana vazi, likapendwa na walio wengi na likarasimishwa. Hapa tukiendelea na mchakato huu tutatengeneza vazi la viongozi na halitakuwa Vazi la Taifa letu.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved