Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza: - Je lini Serikali itaanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya kada ya kati?

Supplementary Question 1

MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu ya Serikali, aidha nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wahitimu wengi wa elimu ya juu wanategemea sana kuajiriwa tofauti na wahitimu wa kada ya kati ambao wanaweza kujiajiri wao wenyewe. Ukweli ni kwamba ajira hazitoshelezi kuajiri wahitimu wote.

Je, Serikali haioni haja ya kuwawezesha wanafunzi wa kada ya kati waweze kupatiwa mikopo ya kugharamia elimu yao kama vile wanavyopatiwa wanafunzi wa elimu ya juu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Je, Serikali inamkakati gani wa kuboresha mitaala ya elimu ili kuweze kuwa na mafunzo ya msingi ya kuanzisha na kuendeleza biashara ili hawa wahitimu wa elimu ya juu watakapokosa ajira basi waweze kujiajiri wao wenyewe? (Makofi)

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Katimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye majibu ya msingi, upande wa utoaji wa mikopo nimesema kwamba Serikali inaendelea kujipanga lakini nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, wenzetu wa Benki ya NMB tayari imeshaanza utaratibu huo wa utoaji wa mikopo kwa upande wa elimu ya kati ambapo kwa mwaka huu wa fedha imeweza kutenga zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya utoaji wa mikopo, nasi kama Serikali tunaendelea na uratibu wa jambo hili ili tuweze kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwamba Serikali inatoa ruzuku ya kutosha kabisa kwa sababu kwenye vyuo vyetu vya kati wanafunzi hawa kila mwanafunzi mmoja anagharamiwa zaidi ya shilingi milioni moja kwa mwaka kwa ajili ya kusaidia vilevile na kupunguza gharama za ada.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anataka kufahamu mikakati ya Serikali juu ya maboresho ya mitaala pamoja na sera. Nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge tunaendelea na utaratibu wa maboresho wa sera pamoja na mitaala, tumeshapata rasimu ya kwanza ya maboresho hayo na miongoni mwa maeneo ambayo tumeyatilia mkazo sana ni katika stadi za fedha pamoja na biashara ili wanafunzi wetu watakapotoka katika vyuo hivi aidha waweze kujiajiri au kuajiriwa.