Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Primary Question

MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: - Je, lini ujenzi wa barabara ya Mangaka hadi Morogoro kupitia Mbuga ya Selous utaanza kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa, Serikali inaniletea majibu siyo sahihi. Barabara niliyouliza mimi ni ya kutoka Mangaka – Nachingwea – Liwale hadi Mahenge, iko ndani ya Jimbo langu la Nanyumbu. Napatiwa majibu ya Wilaya nyingine ambayo mimi sijauliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali iko tayari kurudi ikajipange upya iniletee majibu sahihi ya swali langu? Hilo la kwanza.

Swali la pili, barabara ninayoiuliza mimi ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, alipokuja ndani ya Jimbo langu mwezi Oktoba, 2020. Je, Serikali inatuambia nini juu ya ahadi hii?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba barabara aliyoisema ya kutoka Mangaka – Kilimarondo ambayo inaunganisha na Mkoa wa Morogoro, sehemu ndogo inahudumiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, lakini sehemu kubwa inahudumiwa na wenzetu wa barabara za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana naye kwamba pia yalikuwa ni maelekezo ya viongozi wa Kitaifa kwamba barabara hiyo ijengwe. Kitu cha kwanza ambacho tutaifanya ni kuipandisha hadhi ile barabara – Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami, kuipandisha hadhi ije TANROADS tufanye upembuzi yakinifu na usanifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichosema kuhusu barabara niliyoitaja, ni barabara ambazo zinakwenda sambamba, ukitoka Masasi – Nachingwea kwenda Liwale hii barabara inakwenda sambamba na barabara ya kutoka Mangaka – Kilimarondo kwenda Liwale. Sasa hiyo kwa kuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba itapandishwa hadhi halafu itakuja TANROADS tutafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kuijenga hiyo barabara. Ahsante. (Makofi)

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: - Je, lini ujenzi wa barabara ya Mangaka hadi Morogoro kupitia Mbuga ya Selous utaanza kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 2

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Sumbawanga – Mpanda imetengenezwa kimebakia kipande kidogo cha kutoka Chala – Mpalamawe.

Je, ni lini hiki kipande kitajengwa kwa kiwango cha lami?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kipande hiki alichokisema cha Chala – Mpalamawe, kimsingi ndiyo barabara kuu, lakini kwa sababu Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi yako nje ya barabara kuu, Serikali iliona ni busara barabara ya lami badala ya kujengwa huko porini ipite Makao Makuu ya Wilaya ambayo ndiyo inaunganisha pale Mpalamawe kwenda Mpanda. Mpango ni kuja kuijenga hii barabara kwa kiwango cha lami ili kukamilisha hiyo barabara kuu pia, ahsante. (Makofi)