Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ameir Abdalla Ameir
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
House of Representatives
Primary Question
MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR aliuliza: - Je, Balozi za Tanzania zinatumia vipi fursa ya kukua kwa Kiswahili duniani kutafuta ajira kwa Watanzania?
Supplementary Question 1
MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Tumeshuhudia hivi karibuni nchi ya Afrika Kusini wametangaza uhitaji wa walimu wa lugha ya Kiswahili katika nchi hiyo; je, Serikali sasa inatumiaje fursa hii katika kuhakikisha kwamba walimu wetu waliobobea katika lugha ya Kiswahili wanafaidika na fursa hii hususan walimu kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Miongoni mwa Balozi ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika kuikuza lugha ya Kiswahili ni Ubalozi wa Tanzania nchini Italy, tayari wameshasajiisha Vyuo Vikuu vitatu ndani ya nchi hiyo, vinafundisha lugha ya Kiswahili, kikiwemo Chuo Kikuu cha Torino, Chuo Kikuu cha Roma na Chuo Kikuu cha Napoli. Vilevile nauliza swali; je, Serikali haioni haja kwamba Balozi zetu ambazo zinatuwakilisha katika nchi mbalimbali ziweze kufuata modality hii ya Ubalozi wa Italy nchini Tanzania, ambapo kwa muda mfupi tu tunaweza tukafaidika kwa hali ya juu? Ahsante. (Makofi)
Name
Geophrey Mizengo Pinda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna uhitaji wa Serikali ya Afrika Kusini kuanza kufundisha Kiswahili. Hizi ni juhudi za Serikali vile vile kwa ushirikiano na Serikali ya Afrika Kusini. Kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, kimsingi walimu wetu wamenufaika na hizi fursa na wanapelekwa kwa kasi sana kwa sababu ni matangazo yanakuwa ya hadhara kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Balozi zetu kuiga mfano wa Italy, tumepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tunasisitiza kabisa kabisa. Yapo mambo mengi ambayo katika hali ya kawaida sisi kama Watanzania tunatakiwa kujivunia, Kiswahili chetu kinauzika duniani kote. Tuna redio zaidi ya 13 nje ya Tanzania ambazo zinatumia Kiswahili. Kwa mfano, tuna Idhaa ya Kiswahili ya BBC, tuna Sauti ya Amerika, tuna Redio Japani, Tuna Sauti ya Ujerumani, tuna Sauti ya Umoja wa Mataifa, tuna Redio China na nchi zetu zote hizi za Afrika Mashariki zote zinatumia Kiswahili katika baadhi ya matangazo yake. Kwa hiyo, ni sisi Watanzania kujitangaza katika mazingira yote tunapokuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naziomba Balozi zetu huko nje zianzishe majukwaa mbalimbali yakiwepo matamasha ya Kiswahili katika nchi wanazotuwakilisha ili kukitangaza Kiswahili katika uhalisia wake.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved