Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Issa Jumanne Mtemvu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Primary Question
MHE. ISSA J MTEMVU aliuliza: - Je, nini mkakati wa kushughulikia malalamiko ya ajira za Kada ya Afya na Elimu kutolewa kwa waombaji wanaotoka baadhi ya maeneo?
Supplementary Question 1
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ningeomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa waombaji wengi wanasifa za kitaaluma za jumla zinazofanana kwa sababu wamesoma katika vyuo au shule za pamoja hapa nchini, lakini bado malalamiko yapo mengi kwa sababu hamna nafasi wanazopata katika ajira katika Wilaya kadhaa.
Je, Serikali sasa iko tayari kutoa orodha za kiwilaya wakati inatoa hizo ajira ili waonekane wale katika kila Wilaya waliopata nafasi?
Swali la pili, kwa kuwa hapa Bungeni Serikali ilisema mwezi wa pili kwamba wale wote sasa ambao wapo kwenye database waliofika katika hatua ya mahojiano au oral watapelekwa kwenye vituo au watapangiwa moja kwa moja katika vituo, lakini practice kwa sasa inaonesha si hivyo, kuna watu wanachomekwa chomekwa.
Je, Serikali iko tayari kutoa orodha ile ambayo iko kwenye database ili wananchi waweze kuona wanaopangiwa kwamba ni wale ambao wako kwenye orodha? (Makofi)
Name
George Boniface Simbachawene
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibakwe
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA N AUTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba waombaji wengi wana sifa zinazofanana na kwa kweli wamesoma kwenye vyuo vyetu lakini changamoto tunayoipata hapa ni kwamba pamoja na sifa hizo lakini nafasi ni chache, kwa hivyo namna pekee ya kuweza kuwapata hawa wanaotakiwa, mathalani nafasi zinaweza zikatangazwa labda 200, waombaji wakawa 1,000, namna pekee ya kuwapata hawa 200 ni lazima tu uwashindanishe. Sasa huo ushindani haumaanishi kwamba pengine wengine walisoma ni bora zaidi, ni kama mbio tu za marathon, lakini kimsingi tungetamani wote wanaoomba wapate lakini nafasi ni chache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo kutoa orodha au kuweka utaratibu wa mfumo wa kiwilaya na wenyewe bado tunaendelea kuutafakari kama nilivyosema kwenye majibu yangu wakati tunahitimisha bajeti yetu kwamba tutajitahidi ku – design mfumo ambao utawabaini waombaji na maeneo wanayotoka ili tuweze kutafuta hicho ambacho kilisemwa sana kwa sauti kubwa na Waheshimiwa Wabunge juu ya hisia za upendeleo wa kimaeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili tunaendelea kulifanyia kazi na mpaka sasa tumeunda timu inajaribu kuchakata tuone namna gani bora siyo jambo jepesi, ukilisema hivi kama jepesi lakini kiuhalisia ni ngumu kutengeneza mfumo utakaobaini maana yake hatufuati kabila. Kwa sababu mwingine anatokea mahala kulingana na asili alikokulia au anaomba akiwa yuko Dar es Salaam hatokei Kibakwe lakini anaomba yuko sehemu nyingine, je unamuwekaje? sasa hilo nalo tunaendelea kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba wale waliokwishafanya usaili na mfumo wetu wa usaili ni wa aina mbili, kwanza ni wa kuandika na mwingine ni usaili wa kuulizwa maswali ya papo kwa papo. Sasa wanapotokea watu wamefika kwenye hatua ya pili maana yake wamejitahidi kufanya vizuri na pale napo utampata wa kwanza mpaka wa mwisho lakini uhitaji pengine ni wachache wanaobaki ndiyo Mheshimiwa Mbunge anasema kuwepo na uwazi ili wajulikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie kwamba tutajitahidi sana kuweka uwazi huo ili wajulikane, ili wanapochukuliwa wao wenyewe wadhihirishe kwamba kweli alikuwa wa kadhaa na waliochukuliwa na yeye ameweza kupata fursa ili tuondoe haya manung’uniko.
Name
Amandus Julius Chinguile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Primary Question
MHE. ISSA J MTEMVU aliuliza: - Je, nini mkakati wa kushughulikia malalamiko ya ajira za Kada ya Afya na Elimu kutolewa kwa waombaji wanaotoka baadhi ya maeneo?
Supplementary Question 2
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa nchi yetu kwa sasa ina wahitimu kila kona, na kwa sasa kwa sababu mfumo ulioko wa kuomba ajira una changamoto na una manung’uniko mengi.
Je, Serikali iko tayari sasa kupitia mfumo huu wa sasa ili kupeleka kwenye kila Jimbo idadi sawa ambayo itakwenda kutibu sasa tatizo hili la manung’uniko ambalo kwa kweli kila kona lipo? (Makofi)
Name
George Boniface Simbachawene
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibakwe
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA N AUTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili halitofautiani nalile lililoulizwa na Mheshimiwa Mtemvu, tofauti ni kwamba Mheshimiwa Mtemvu kasema Wilaya lakini Mheshimiwa Mbunge kasema Jimbo. Kama nilivyosema tunaendelea kufanya utafiti kwa kutumia mifumo lakini na uhalisia wa jambo lenyewe kama tunaweza tukalitekeleza katika usahihi sana kinyume na utaratibu wa sasa wa kushindanisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna upungufu kwenye kushindanisha au kama hakuna uwazi wa kutosha kwenye kushindanisha inaweza ikawa kazi nyepesi zaidi kushughulikia kuliko kutafuta mfumo utakaoweza kuja na majawabu haya. Hata hivyo, katika jibu langu la msingi nimesema kwamba tutajitahidi kuandaa, tumeunda timu ambayo inaendelea kufanya utafiti hata sasa wako kazini watatuletea majawabu ya namna gani tunaweza kufanya yote mawili mfumo na uhalisia ili tuweze kuona manung’uniko haya yanakwisha kabisa. (Makofi)
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Primary Question
MHE. ISSA J MTEMVU aliuliza: - Je, nini mkakati wa kushughulikia malalamiko ya ajira za Kada ya Afya na Elimu kutolewa kwa waombaji wanaotoka baadhi ya maeneo?
Supplementary Question 3
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Mimi nimemsilikiza sana Mheshimiwa Waziri na nimemuelewa lakini nataka niiambie Serikali kwamba akina Simbachawene kule Sikonge wako wengi tu na akina Lusinde na wakina Mpangala. Kwa hiyo, suala siyo kabila au asili ya mtu, suala ni anuani. Kwa nini anuani zile zisitumike kuweka wazi kwamba huyu anuani yake ni P.O.Box 8 – Sikonge, ukawa na watu labda 20 ambao umewaajiri kutoka Sikonge ukaonesha pale, kwa nini isiwe rahisi namna hiyo badala ya anavyofikiria ukabila na mambo mengine? (Makofi)
Name
George Boniface Simbachawene
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibakwe
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA N AUTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema kwenye jibu langu la msingi, nataka aniseme tu Mheshimiwa Kakunda alichokisema ni kwamba tuende kwenye anuani. Tukienda kwenye anuani pia kuna confusion bado, bado utaiona tu confusion kwa sababu utaichukua anuani, unataka kumchukua mtu aliyetoka kwenye Jimbo anakotoka Mheshimiwa Kakunda, lakini utatumia chuo alichosoma, utatumia mahali alikokulia, utatumia anuani alikoombea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, so kuna mambo mengi ya kuyaangalia ndiyo maana tunasema huo mfumo tunaouangalia na ushahidi tunaoungojea wa kitaalamu na utafiti unaofanyika utatusaidia zaidi kuliko hapa sasa hivi nikisema tutafata utaratibu huu. Nadhani mtuachie Serikali tulifanyie kazi tunaweza tukaja na kitu kizuri zaidi. (Makofi)