Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abdallah Dadi Chikota
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, ni lini kutakuwa na kiuatilifu kimoja cha magonjwa kwenye zao la korosho?
Supplementary Question 1
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kumekuwa na ongezeko au utitiri wa viuatilifu vita kwenye zao la korosho; je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kutoa elimu kwa wakulima wakati wa ugawaji wa viuatilifu hivi?
Swali la pili, naipongeza Serikali kwa kuanza mfumo wa usajili wa wakulima wa korosho ili kutoa pembejeo na viuatilifu kwa wakulima lakini kuna kundi kubwa la wakulima ambao mpaka sasa hawajasajiliwa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya usajili kwa wakulima hao?
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la utitiri wa viuatilifu, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi viuatilifu hivi huwa vinatokana na aina ya magonjwa vilevile wadudu waharibifu ambao wanapelekea matumizi ya viuatilifu hivyo. Jambo kubwa ni kwamba kama Serikali kupitia kituo cha utafiti cha TARI-Naliendele pamoja na Bodi ya Korosho tutaendelea kutoa elimu kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu hivi ili mwisho wa siku viweze kuleta tija na tuongeze uzalishaji wa zao la korosho.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili kuhusu usajili wa wakulima. Zoezi la usajili wa wakulima linaendelea. Ni kweli wapo baadhi ya wakulima bado hawajasajiliwa, tunaongeza nguvu kupitia bodi kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya rasilimali watu ambao watasaidia kufanikisha zoezi la usajili huo wa wakulima ili wakulima wote waweze kusajiliwa na wapate viwatilifu kwa wakati kwa sababu hivi sasa ni takwa la lazima kwamba wakulima tuwe tumewasajili ili waweze kupata viuatilifu kwa urahisi.
Mheshimiwa Spika, hivyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, tunaongeza jitihada kubwa kuhakikisha kwamba zoezi hili linakamilika kwa wakati.
Name
Salma Rashid Kikwete
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mchinga
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, ni lini kutakuwa na kiuatilifu kimoja cha magonjwa kwenye zao la korosho?
Supplementary Question 2
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na kusema kwamba tusitoe pongezi naomba uniruhusu nitoe pongezi kwa Serikali kuhusiana na suala zima la zao la mbaazi. Mbaazi tulikuwa tunauza kilo mpaka shilingi 100 lakini kwenye mnada wa mwisho tumeuza shilingi 2,130. Haya ni mafanikio makubwa sana.
Mheshimiwa Spika, swali langu kwa Serikali, je, bei hii itakuwa ni endelevu ili kuhakikisha kwamba wakulima wanaongeza uzalishaji wa zao hili?
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba wakulima wanaendelea kunufaika na kilimo. Tutahakikisha tunaendelea kuweka miundombinu rafiki ili bei hii iendelee kumnufaisha mkulima na hasa wakulima wa mbaazi kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved