Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Innocent Sebba Bilakwate
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyerwa
Primary Question
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:- Je, Serikali ipo tayari kujenga kilometa moja ya lami nyepesi Mabira Station ili kuboresha mazingira mazuri kwa wafanyabiashara?
Supplementary Question 1
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naishukuru Serikali kwa majibu angalau yenye matumaini.
Swali langu la kwanza; barabara ya Rulama -Kanyantama - Ruita mpaka Mabira barabara hii inaunganisha kata nne; Kata ya Kibale, Businde, Kamuli mpaka Mabira na inaunganisha Tarafa mbili na ni muhimu sana kuna wakulima wengi. Ni lini barabara hii itatengewa fedha iweze kutengenezwa ili iweze kupitika kipindi chote?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ni lini barabara ya Nkwenda mpaka Mabira itapandishwa hadhi iwe chini ya TANROADS kwa sababu inahitaji fedha nyingi na ni muhimu sana kwa wananchi wa Kyerwa?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Bilakwate, kwanza nitumie nafasi hii mbele ya Bunge lako tukufu kumwarifu Mheshimiwa Bilakwate kwamba ombi lake kama mwakilishi wa Wanakyerwa la fedha kwa ajili ya barabara ya Kasoni - Mkuyu tayari pesa hiyo imepatikana na muda si mrefu Mheshimiwa Mbunge mkandarasi atapatikana ili kuingia site na kuanza ujenzi wa barabara hii kama alivyokuwa ameiomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye maswali yake; hii barabara ya Ruhama – Kanywaa – Ntama - Ruhita ambayo inaunga kata nyingine na Kata ya Mabira tayari andiko lilikuwa limewasilishwa na Meneja wa TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Kagera lilishawasilishwa Makao Makuu ya TARURA na walikuwa wameomba shilingi milioni 700 kwa ajili ya ukarabati wa barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kadri ya upatikanaji wa fedha TARURA itapeleka fedha katika Mkoa wa Kagera kwa ajili ya utengenezaji wa barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili barabara ya Nkwenda inayokwenda Mabira kupandishwa hadhi na kuwa barabara ya TANROADS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za kisheria ziko wazi, ni lazima wao wenyewe katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa waanze na vikao vyao ikiwemo DCC ikitoka DCC waipeleke katika RCC halafu kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa na baada ya Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wanawasilisha ombi lile kwenda kwa Waziri mwenye dhamana ya barabara yaani Waziri wa Ujenzi ndipo barabara hiyo iweze kupandishwa hadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi naomba niwaase waanze mchakato huo kwa ajili ya kuwasilisha kwenda kwa Waziri wa Ujenzi.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved