Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mariamu Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaondoa popo waliopo maeneo ya Upanga ili kulinda afya za wakazi wa maeneo hayo?

Supplementary Question 1

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nampongeza sana; lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imeonesha wazi kwamba wameweka hiyo dawa. Hata hivyo, tatizo la popo katika maeneo ya Upanga, Sea View, Leaders Club, Kinondoni, Oysterbay, Masaki, Msasani Peninsula na maeneo mengine ya ukanda wa pwani linaongezeka siku hadi siku na kusababisha popo hao mpaka wanavunja vioo vya madirisha kwenye nyumbani.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza hiyo dawa ili popo hawa waweze kuondoka na kuwaondolea adha wananchi wa maeneo hayo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa changamoto inayowapata wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam katika maeneo ya Upanga na mengineyo, pia inawakuta wananchi wa Dodoma kuvamiwa na nyuki katika maeneo mbalimbali hasa maeneo ya Area D katika majengo ya TBA, Makole yote pamoja na maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma nyuki wanavamia na kuhama hama hovyo hovyo;

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaondolea wananchi wa Jiji la Dodoma adha ya kuvamiwa na nyuki?

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye swali la msingi, hatua ya kwanza ya kukabiliana na popo hawa ilikuwa ni kufanya utafiti wa kujua kiwango cha ukubwa wa tatizo na aina ya dawa ambayo inaweza kutumika ili kukabiliana na changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, utafiti huu umekamilika, sasa jukumu lililopo mbele yetu ni kuhakikisha kwamba wadau wote wanaohusika na kukabiliana na jambo hili, zikiwepo Halmashauri zetu zinachukuwa hatua ya kuhakikisha tunasambaza dawa hizi kwa wananchi ili tuweze kukabilianana tatizo hili. Niombe wadau wote wanaohusika tushirikiane ili tuweze kuondokana na tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la tatizo la uvamizi wa nyuki kwenye Mkoa wa Dodoma. Nitumie fursa hii kuwaagiza wataalamu wetu wa idara ya nyuki kushirikiana na wenzetu wa jiji la Dodoma ili kufanya tathmini ya haraka na kuona ukubwa wa tatizo hili na kuchukua hatua za haraka za kuangamiza nyuki hawa, ahsante sana.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri na kumpongeza, tunafanya kazi vizuri kwa pamoja na nimpongeza kwa majibu mazuri sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuongezea majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa upande wa popo, tayari tumeagiza dawa nyingine za majaribio ikiwemo Pepzol na Super Dichlorvos ambazo zinapatikana Marekani na Kenya. Imeonekana kwamba dawa hizo zikitumika ndani ya miezi miwili mpaka mitatu popo hao wanaweza wakatoweka.

Mheshimiwa Spika, pia nitoe rai kwa Halmashauri zetu za Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri nyinginezo katika maeneo ya miti ya barabarani waweze kununua dawa hizo ili waweze kupiga kwa ajili ya kuweza kufukuza na kudhibiti popo hao.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa Jiji la Dodoma kuhusu suala la nyuki, kama ambavyo Naibu Waziri ameeleza, nako pia tutoe rai kwa Halmashauri ya jiji Dodoma nao watenge fedha ili waweze kununua dawa hizo ili pale tutakapokuwa tumepata tathmini ya kuweza kujua ni dawa gani zinaweza kufanya kazi vizuri katika kudhibiti basi waweze kununua dawa hizo na kuweza kutumia.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia taasisi ya TAWIRI tutaendelea kushirikiana na wananchi pamoja na taasisi katika kuhakikisha kwamba tunadhibiti tatizo hili. Tuombe ushirikiano kwa wale wenye makazi pia waweze kununua dawa hizi katika maduka mbalimbali yanayozalisha dawa hizi. (Makofi)

Name

Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaondoa popo waliopo maeneo ya Upanga ili kulinda afya za wakazi wa maeneo hayo?

Supplementary Question 2

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na popo katika Mkoa wa Dar es Salaam, kuna tatizo kubwa la kunguru ambao wamekuwa wakitapakaa kila mahali, wanajerui watoto; na hasa katika fukwe, ambako wamekithiri, na hivyo kuharibu utalii wetu. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanadhibiti kunguru hao?

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kujibu swali la nyongezala la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na tatizo la kunguru katika maeneo mbalimbali nchini. Serikali kupitia Wizara imekuwa ikifanya jitihada ya kuja na mipango mbalimbali ya kuweza kuondokana na tatizo hili. Changamoto tunayoiona ni kwamba wenzetu kwenye maeneo ya halmashauri zetu wameliacha jambo hili kuwa ni jambo la Wizara peke yake. Tunawaomba sana wadau wenzetu katika maeneo ya halmashauri, kwa kutumia teknolojia iliyoandaliwa na Wizara tushirikiane ili kupambana na tatizo hilo. (Makofi)