Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mabweni yaliyoanzishwa na wananchi kwa michango yao katika shule za kata nchini?

Supplementary Question 1

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafsi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara majanga ya moto katika mabweni ya shule zetu. Je, Serikali imefanya uchunguzi gani kujua chanzo ni nini na ni upi mkakati wa Serikali kupambana na janga hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika shule ambazo tayari mabweni yamekamilika kumekuwa hakuna walezi wa watoto au walezi wa wanafunzi katika shule zetu yaani patrons na matrons je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuwaajiri walezi wa watoto katika shule zetu? (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Regina Qwaray, la kwanza hili juu ya majanga ya moto ambayo hujitokeza katika shule za bweni. Serikali kupitia Jeshi letu la Zima Moto na Uokoaji imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali hasa katika shule hizi za bweni juu ya namna bora ya kujikinga na majanga ya moto.

Mheshimiwa Naibu Spika, na tutaendelea kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji kuhakikisha kwamba mafunzo haya yanazidi kutolewa kwenye halmashauri mbalimbali na nitumie nafasi hii mbele ya Bunge lako hili kutoa wito kwa halmashauri za Wilaya zote hapa nchini ambazo zina shule za bweni ziweze kuhakikisha zinashirikiana na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji katika kutoa elimu ya kujikinga na moto katika shule zote za bweni.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la pili la Mheshimiwa Regina Qwaray la mabweni kutokuwa na ma-patron na ma-matron, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika kuhakikisha inaajiri walimu wa kutosha kadiri ambavyo bajeti inaruhusu tunaajiri. Pale ikama itakapotimia tutaanza kuangalia ni namna gani tutaweza kuajiri ma-patron na ma-matron lakini kwa sasa walimu waliopo ndio wanateuliwa kwa ajili ya kuangalia watoto katika shule zile mabweni ambao ndiyo wanaokuwa ma-patron ndiyo wanaokuwa ma-matron.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakaa na wenzetu wa Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kuona ni namna gani bora tunaweza tukapata vibali kwa ajili ya kuajiri ma-matron na ma-patron kwa ajili ya kutimiza ikama na upungufu ambao upo.

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mabweni yaliyoanzishwa na wananchi kwa michango yao katika shule za kata nchini?

Supplementary Question 2

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itajenga Sekondari mpya Kata ya Ketare eneo la Nyaburundu na Kata ya Mihingo eneo la Machimero kwa sababu ni muda mrefu Serikali imeahidi kujenga sekondari hizo?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Getere, lini Serikali itajenga sekondari mpya katika maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge, kwa sasa Serikali inajenga shule mpya katika kila halmashauri hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwa Mheshimiwa Getere pia amepata zaidi ya shilingi milioni 580 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya na tutazidi kutafuta fedha kwa sababu Serikali hii ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele cha kuhakikisha kata zote ambazo hazina sekondari zinajengewa sekondari mpya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira tutakapomaliza ujenzi wa hii shule ya shilingi milioni 580 ambayo iko jimboni kwake tutaendendelea kutafuta fedha nyingine kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari katika kata ambazo amezitaja.

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mabweni yaliyoanzishwa na wananchi kwa michango yao katika shule za kata nchini?

Supplementary Question 3

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa kuna smoke detecters ambao ndio utaaalamu wa kisasa wa kujua kama moto unakuja. Kwa nini Serikali haioni ni muhimu chombo hicho kuwekwa katika kila jengo la shule au taasisi inayojengwa ili waweze kupata alert?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond hili la smoke detectors. Kama nilivyokuwa nimeshazungumza hapo awali tutashikiana kwa karibu na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Zima Moto na Uokoaji kuona sasa ni namna gani tunaweza kuhakikisha majengo yote ya shule zetu yanakuwa ya smoke detectors hasa zile shule za bweni ambazo zina wanafunzi wanaolala pale muda wote.