Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Simai Hassan Sadiki

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nungwi

Primary Question

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza: - Je, kuna mkakati gani wa dharura wa kunusuru athari za mabadiliko ya tabianchi - Nungwi?

Supplementary Question 1

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa sasa ni mwaka wa tatu nimekuwa nikisimama katika Bunge hili kuulizia jitihada zinazochukuliwa na Serikali zote mbili katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi maeneo ya Nungwi lakini majibu tunayopata leo ndiyo kwanza shilingi milioni 650 zimetengwa kwa ajili ya kufanya utafiti. Ninachotaka kujua ni lini utafiti huu utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, shughuli za utalii na uchumi wa bluu zimekuwa zikiathiri sana ukataji wa mikoko katika maeneo ya fukwe za Bahari ya Hindi kule Zanzibar. Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuhakikisha kwamba mikoko inarejeshwa katika uhalisia wake? (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kuchukua fursa hii kumpongeza sana kwa kuwa jambo hili amekuwa akilipigia kelele sana na hatimaye sisi kama Serikali tumeshaandaa fedha kwa ajili ya kuanza angalau tathmini ya awali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa fedha hizi zimeshapatikana naomba kumwambia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa utafiti unaenda kuanza muda wowote. Kama tulivyosema kwamba kuna kuta za aina nyingi, kwa hiyo ni lazima utafiti ufanyike ili tujue ni aina gani ya kuta. Kuna kuta za slope ambazo zinatoa maji mitaani zinapeleka baharini, lakini pia kuna kuta ambazo zinakinga kutoka baharini maji yasije mitaani. Kwa hiyo ni vyema utafiti ufanyike ili tuone ni aina ya kuta na pia tuweze kupima current ya maji ya sea breeze na land breeze, ni aina gani ya huduma ambayo wananchi wanatakiwa wapatiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, kwa upande wa swali la pili, tumechukua hatua nyingi. Moja ni kuendelea kutoa elimu wasikate, wapande na wasichome mikoko ambayo ipo around ufukwe wa bahari. Kubwa zaidi tumeendelea kuhimiza kupitia ilani ambayo inasema kwamba kila Halmashauri kila mwaka lazima ipande miti milioni 1.5. Kupitia miti hii tumehimiza mikoko ipewe kipaumbele ili kunusuru fukwe zetu lakini zaidi kuendelea na ile sera yetu ya soma na mti. Tunataka wanafunzi wa sekondari, msingi, vyuo na vyuo vikuu wapande miti, lakini miti ambayo tumeipa kipaumbele hasa kwa shule za fukwe ni mikoko, nakushukuru.

Name

Juma Usonge Hamad

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chaani

Primary Question

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza: - Je, kuna mkakati gani wa dharura wa kunusuru athari za mabadiliko ya tabianchi - Nungwi?

Supplementary Question 2

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwa vile Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Muungano na Mazingira ndiyo ambayo inashughulika na masuala ya kuratibu na kushughulika na mabadiliko ya tabianchi. Nilitaka kujua je, mnatumia utaratibu gani wa kupokea miradi yote ambayo inatoka Zanzibar kwa ajili ya utekelezaji wa kushughulika na haya mabadiliko ya tabianchi kwa upande wa Zanzibar?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu ni kwamba kwanza tunaandaa maandiko ambayo yanalenga kwenye mradi husika. Kinachofuata sasa ni kufanya tathmini na utafiti wa kujua mradi ulioombwa na baadaye mradi huo unaanza utekelezwaji kama miradi iliyotekelezwa huko Zanzibar.

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza: - Je, kuna mkakati gani wa dharura wa kunusuru athari za mabadiliko ya tabianchi - Nungwi?

Supplementary Question 3

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Hivi karibuni Serikali imetangaza uwepo wa Mvua za El nino. Ni upi mkakati wa haraka wa Serikali kupunguza athari zitakazotokana na mvua hizi ndani ya Jiji la Dar es Salaam na hasa mafuriko ambayo yanasababishwa na Mto Msimbazi?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kipindi cha mvua kubwa mara nyingi kunakuwa na mafuriko makubwa ambayo yanasababisha athari hasa kwenye makazi ya wananchi. Wakati mwingine inafika hatua mafuriko yanagharimu maisha ya wananchi. Namwambia Mheshimiwa kwamba huwa tunachukua hatua nyingi. Moja, ni kuelimisha wananchi; kwa mfano sasa hivi tumeanza kutoa elimu kuhusu Mvua za El nino ambazo zinategemea kuja. Tunawaambia wananchi wasijenge kwenye maeneo au karibu na maeneo ambayo yanajaa maji ili kama wana mpango huo waanze kuondoka mapema ili zitakapokuja mvua wasiweze kupata mafuriko hayo ama mafuriko hayo kuleta athari kwa wananchi. (Makofi)

Name

Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Primary Question

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza: - Je, kuna mkakati gani wa dharura wa kunusuru athari za mabadiliko ya tabianchi - Nungwi?

Supplementary Question 4

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini Serikali itaanza kujenga Mto Msimbazi ukizingatia sasa hivi wataalam wa hali ya hewa wamesema kwamba kuna mvua kubwa inanyesha; je, ni lini wataanza kutujengea ili wananchi wetu wawe salama? (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ujenzi wa Mto Msimbazi umeanza, na nimwambie tu Mheshimiwa kwa kuwa ujenzi huu...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri umeanza au uko katika maandalizi?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hatua tuliyofikia maana yake sasa tunakwenda kuanza.

NAIBU SPIKA: Haya, endelea.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo namwambia Mheshimiwa kwamba uanzaji huu unakwenda kwa hatua. Hatua hizi zinakwenda kadri tutakavyokuwa tunapata fedha. Tutahakikisha kwamba maeneo yote yatajengwa na tutahakikisha kwamba tunapata usalama wa wananchi.