Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Michael Mkundi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Primary Question

MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Je, nini mkakati wa Serikali kuvifanya vivutio vya mapango ya Handebezya na jiwe linalocheza kuwa na tija kwa Taifa?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Natumia nafasi hii kuipongeza Wizara na Serikali kwa ujumla kwa jitihada zinazofanywa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Napongeza Wizara kwa kutumia TTB na kuratibu ziara ya waandishi wa habari kwa ajili ya kubaini vivutio hivi. Hata hivyo, huwezi kutenganisha utalii na rika mbalimbali kwenye eneo husika kwa maana ya watu wazima, wazee, rika la kati na watoto katika kubaini na kuendeleza utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ziara hii imefanikiwa, lakini bahati mbaya sana kuna rika la watu wazima, kuna kikundi cha KUMIDEU na vinginevyo ambavyo vinafahamu zaidi utamaduni, mila na desturi za watu wa Ukerewe, walitakiwa kuhusishwa. Nini sasa mkakati wa Serikali ili wakati mwingine vikundi kama hivi vishirikishwe ili kupata uhalisia wa vivutio vya utalii vilivyopo pale Ukerewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali, lakini tunakosa kiungo kinachoweza kuratibu mambo haya ya utalii. Halmashauri zetu zingeweza kutoa msaada mkubwa sana, lakini bahati mbaya sana hazina watu specific wanaoshughulika na utalii zaidi ya utamaduni. Je, ni nini mkakati wa Serikali sasa kuhakikisha Halmashauri zetu zote zinakuwa ama na idara au na vitengo vinavyohusika na utalii ili kuweza kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais katika kukuza Sekta ya Utalii? Nashukuru. (Makofi)

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ulimwenguni kote, custodian wa mila na desturi ni Machifu wakienda sambamba na wazee wa mila na desturi. Kwa bahati mbaya kwenye halmashauri zetu kumekuwa na upungufu wa kubaini makundi haya ya wazee wa mila na desturi. Natoa rai kwa halmashauri zetu, ziwe na mikakati ya kuwatambua wazee wa mila na desturi ambao ndio custodian wa tamaduni zetu ili tunapofanya jukumu la kutambua na kutangaza vivutio vilivyopo kwenye maeneo yetu, basi wazee hawa waweze kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa halmashauri zetu, zijielekeze kwenye kutambua maeneo yote yenye sifa za kiutalii, wawasiliane na Wizara ili maeneo haya yaweze kusajiliwa tuweze kuweka mpango mkakati wa pamoja wa kutangaza maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili la uhaba au kukosekana kwa kiungo, kwa kukosekana wataalam kwenye halmashauri zetu. Mamlaka ya ajira ya watumishi kwenye ngazi ya halmashauri, ni Wizara ya TAMISEMI. Naomba sana halmashauri zetu zijielekeze kwenda kuomba vibali vya ajira kwa TAMISEMI ili jambo hili liweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kwa kutambua gap lililopo, Wizara ya Maliasili inao wataalam kwenye kanda zetu. Kwa mfano, kwenye Kanda ya Ziwa Victoria, tunao wataalam wetu wawili walioko Mwanza, Kanda ya Kusini, tunao wataalam watatu wapo Iringa, Kanda ya Kaskazini, tunao wataalam sita wapo Arusha, Kanda ya Pwani, tunao sita wapo Dar es Salam lakini vilevile hapa Makao Makuu tunao wataalam. Tunaomba halmashauri zetu ziwatumie wataalam hawa wakati wakijiandaa kupata vibali vya ajira kutoka TAMISEMI.