Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Primary Question

MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha maslahi ya Wathibiti Ubora wa Walimu nchini ili kuinua ubora wa elimu?

Supplementary Question 1

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naipongeza sana Serikali kwa majibu mazuri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa ziko fedha za uchangiaji wa elimu zinazotolewa na Serikali kupitia kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Wakuu wa Vyuo kwenda kwa Wadhibiti Ubora, fedha hizi zimekuwa na usumbufu mkubwa sana, lakini zimekuwa kero kubwa sana kwa Wakuu wa Shule pamoja na Wadhibiti Ubora. Serikali haioni haja sasa kwamba umefika wakati wa kubadilisha miongozo yake na sheria ili fedha hizi zitoke moja kwa moja Hazina na kwenda kwa Wadhibiti Ubora? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Wadhibiti Ubora wanafanya kazi yao vizuri sana; Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuwajengea uwezo ili kuongeza ufanisi wa kazi katika majukumu yao? Ahsante sana (Makofi)

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu ya swali la msingi, Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali kuhakikisha kwamba Wadhibiti Ubora wanakuwa kwenye mazingira salama ya kufanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyosema kwamba tunakwenda kubadilisha muundo wa kada hii ya Wadhibiti Ubora na sasa tunakwenda kuondoa ile Udhibiti Ubora ngazi ya kanda na kupeleka katika ngazi ya mikoa na katika kufanya hivyo tunasogeza huduma karibu zaidi ya wananchi na vilevile tunaimarisha utendaji kazi kwa ufanisi mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanya haya yote, tutahakikisha vilevile katika eneo hili la uchangiaji tunaenda kulifanyia kazi ili liweze kushuka moja kwa moja kwenda Ofisi za Wadhibiti Ubora badala ya kwenda kwa Walimu Wakuu au kwenda shuleni kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili la utendaji kazi, tumekuwa na utaratibu wa kuhakikisha kwamba Wadhibiti Ubora wanapata mafunzo ya mara kwa mara ili kuwajengea umahiri na kuwawezesha kufanya shughuli zao za kila siku kwa ufanisi, nakushukuru.