Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: - Je, Serikali inatambua gunia kuwa kipimo au kifungashio kwa mujibu wa Sheria?

Supplementary Question 1

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza; kwa kuwa sasa Serikali imekiri kwamba gunia sio kipimo ni kifungashio. Je, Serikali iko tayari sasa kutoa waraka na kupeleka kwa Wakala wa Vipimo na Halmashauri zote nchini kuzuia tabia ya kushusha magunia katikati ya safari na kuanza kuyapima barabarani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuna mazao kama mbogamboga, matunda na viazi yamekuwa yakipimwa kwenye soko kwa kilo, lakini shambani yamekuwa yakipimwa kwa magunia. Je, Serikali iko tayari sasa kutoa kipimo cha awali kwa ajili ya mazao ya aina hiyo, namna ambavyo yanaweza kupimwa yakiwa shambani?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kutoa concern ya wenzetu wa Halmashauri na Wakala wa Vipimo kukagua magunia au mazao yanayopita katika sehemu mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumeshasema kwamba, kama wananchi wameuza kwa vipimo na kukawa na uthibitisho wa kwamba mazao yale kama either yamefungashwa katika magunia au katika vifungashio (vibebesheo) vyovyote kama vina uthibitisho kwamba yameuzwa kwa vipimo, wale wanaokagua aidha Wakala wa Vipimo au Halmashauri watumie zile risiti au vielelezo vyovyote (evidence) ili ziwe ni sehemu ya kupunguza usumbufu kwa wananchi, wakulima au wafanyabiashara wanaposafirisha mazao badala ya kupima kila gunia kwenye maeneo ya ukaguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na suala la mbogamboga. Haya bado ni maelekezo, katika mazao yote kwamba, katika maeneo mengi tunahamasisha wakulima wajiunge katika Vyama vya Msingi au wauzie kwenye masoko ambako kule sisi tumeshaelekeza Wakala wa Vipimo wapeleke mizani ili itumike kupima uzito wa bidhaa inayouzwa badala ya kutumika vifungashio vya namna yoyote ile ambavyo havitumii vipimo sahihi, nakushukuru sana.